Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Benjamin William Mkapa na Mkewe Mama, Anna Mkapa wakiteta jambo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi baada ya kupita katika wodi kumuona Kiongozi wa Parokia ya Mpendae, Padre Ambrose Mkenda aliyelazwa kwenye Hospitali ya Muhimbili akipatiwa huduma baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi siku ya Krismasi, Desemba 25, 2012. (Picha na Othman Hamisi Ame-Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar)
Habari imeandikwa na Shomari Binda, Musoma via blog post - “ALIYETEKWA ASIMULIA NAMNA VICHWA VYA BINADAMU VINAVYOPAKIWA KWENYE VISADO NA KUWEKWA RANGI JUU” SUALA la watu kutekwa na kukatwa vichwa limechukua sula nyingine baada ya mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Obwanga Jamara mkazi wa Utengi eneo la Ingili chini katika Wilaya ya Rorya kutekwa na watu wasiofahamika na kuamuliwa kupaki vichwa vya binadamu katika visado (ndoo ndogo za plastiki) vya rangi. Akizungumzia kisa cha kutekwa alipokuwa akizungumza na shommibinda.blogspot.com, katika Hospitali ya Mkoa wa Mara alikokuwa amelazwa katika chumba cha ICU kutokana na maumivu makubwa aliyoyapata kutokana kwa watekaji alielezea kila kitu huku akilishitumu Jehi la Polisi kwa kushindwa kufatilia. Alisema alifika katika Kijiji cha Nyankanga akitokea nyumbani kwake Utegi kwa lengo la kukata mti wake wa mbao uliopo kijiji hapo Desema 27 na ndipo alipokutana na dhahama ya kutekwa na kushuhudia maovu makubwa yanayofanywa na watekaji hao. Alisimulia kuwa alipokuwa katika maeneo hayo alikuwa katika maeneo hayo akiwa anatafuta mashine ya kupasulia mbao ambapo huo ulikuwa mti wake wa pili kwenda kuukata na mashine aliipata hapohapo kijijini kwa kukodi. “Nilifika Nyankanga nikiwa natafuta mashine baada ya mtu wa kwanza aliyenikodishia kumkosa na kuanza kuulizia ndipo nilipokutana na vijana wawili ambao walidai wanamfahamu mtu ambaye anayo mashine. Nilichukuliwa na vijana hao na kufika mbele kidogo tulipanda kwenye gari inayodaiwa ndio iliyokuwa ya mtu anayedaiwa kuwa na mashine ili kwenda kuufata nyumbani kwake na kufika njiani niligeuziwa kibao. Nikiwa nimewekwa katikati na wale vijana wawili nilitolewa mfano wa bastora nilipoiona niligundua sio halisi pamoja na sime na kuambiwa nitoe pesa na mfuko wa ndani nilikuwa na shilingi elfu sitini nikatoa na kuwapa,”alieleza. Alisema baada ya kutoa pesa hizo alifunikwa uso wake kwa shati lake alilokuwa amevaa na kuwekwa nyuma ya buti ya gari na kupelekwa mahala kukojulikana ambako alikutana na ukatili mkubwa unaofanywa na watekaji hao. “Baada ya kuzungushwa sana huku nikiwa nyuma ya buti ya gari niliingizwa ndani ya nyumba ambayo siwezi kuifahamu na kuachwa humo na wenyewe kuondoka huku nikiwa bado nimefungwa macho na kusikia sauti ya kike ikilia ndani ya nyumba hiyo. Baada ya muda kupita watu wale walirejea na kunivua kitambaa machoni na kuniwekea box mbele na kuniamulu nifungue na kukutana na vichwa vitatu vya Binadamu na nilivyoviona ni vya watoto kati ya miaka mitatu ama mitano. Huwezi kuamini ndugu Mwandishi ni hatari na Serikali isipo fatilia jambo hili hali itakuwa mbaya sana maana suala hili lipo na mimi nimelifanya kwa mikono yangu mwenyewe baada ya kutekwa. Nilivitoa vile vichwa kwenye box nikishirikiana na Yule dada niliyemkuta mle ndani nakuambiwa niviweke kwenye kisado cha rangi kimoja baada ya kimoja na kisha kuweka udongo wa mfinyanzi huku jua tukiweka rangi na kufunga,”aliendelea kusimulia muhanga huyo. Alisema baada ya kumaliza kufanya kazi hiyo aliyoamuliwa na watu waliomteka walimfunga tena kitambaa machoni na kumtoa ndani ya nyumba na kumpakia nyuma ya buti ya gari na kumpleka kusiko julikana. “Tukiwa njiani huku mimi nikiwa nyuma ya buti ya gari ilisimama na wale watu kushuka na kuanza kuisukuma… inaonekana ilizimika lakini nilisikia watu wakipita barabarani nakusalimiana habari afande July,”aliendelea kusimulia. Alisema baada ya gari kushindwa kuwaka na watu waliokuwa wakisalimiana nao kupita aliwasikia watu hao wakipiga simu kuomba gari lingine na kuambiwa kuwa halipo waangalie wafanyeje. “Baada ya gari kushindwa kuwaka walinishusha kwenye gari huku nikiwa bado nimefunikwa macho na kupelekwa mahala na kutupwa huku mmoja wao akisema mmalizie kabisa ambapo walinikanyaga kifuani na kichwani na kupoteza fahamu na kujua kuwa tayari wameshaniua,”aliongeza. KUOKOTWA NA POLISI MAKABURINI Obwanga alisema baada ya kupata nafuu katika chumba cha wagonjwa mahututi alisimuliwa na wauguzi hospitali hapo kuwa alifikishwa na askari Polisi na kudaiwa ameokotwa katika makaburi ya Menonite katika Manispaa ya Musoma Desemba 28.Anadai baada ya kufikishwa Hospitalini hapo hakuna askari yeyote aliyefika kwa muda kumchukua maelezo ili wale waliofanya tukio hilo waweze kufatiliwa lakini haikuwa hivyo. “Hadi jana (juzi) Desemba 30 saa mbili usiku ndipo nilipoona askari wanakuja kunichukua maelezo nilitaka kugoma lakini nikaamua kutoa kutokana na kushauliwa na wauguzi baada ya kuwaona Polisi hawatimizi majukumu yao kwa wakati,”alisema. MEYA AZUNGUMZA NA KAMANDA Baada ya kukutana na muhanga huyo kutokana na taarifa za Mwandishi wa Habari hizi, Meya wa Manispaa ya Musoma Alex Kisurura (CHADEMA) alikutana na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mara, Absalom Mwakyoma akiwa na muhanga na kukili kupokea tukio hilo na kuahidi kulifanyia kazi kwa kina. "Tumeongea na Kamanda wa Polisi wa Mkoa na kutuhakikishia suala hilo linafanyiwa kazi kwa nguvu zote na Jeshi na kuahidi kutoa matokeo yake baada ya kukamilisha shughuli nzima," alisema Meya Kisurura. NYERERE ATAKA POLISI WALIPWE Akizungumza kwa njia ya simu na shommibinda.blogspot.com Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini Vicent Nyerere alisema kitendo cha askari Polisi kutokachukua hatua za haraka ni kutokana na baadhi yao kutolipwa mafao yao kwa wakati na kufanya kazi katika mazingira magumu. Alisema zaidi ya askari 230 Mkoani Mara wanadai fedha zao hali inayopelekea kutokuwa na moyo wa kufanya kazi kwa ufanisi na kupelekea kutokea kwa matukio mbalimbali ambayo yanaweza kukabiliwa. ![]() Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa akikabidhi Mbuzi kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Tushikamane Children Care Trust Fund Bw. Gratho Messy Mbele (wa kwanza kulia) na Mkuu wa Shule ya Tushikamane Bi. Euphrosine Mtundu, kama zawadi kwa watoto yatima wa kituo hicho ambapo panapo majaliwa hapo kesho atajumuika nao kupata chakula cha mchana. Anayeshuhudia tukio hilo ni Diwani wa Kata ya Tabata Hajati Mtumwa Mohamedi (wa pili kushoto) ![]() Mstahiki Meya Jerry Silaa akikabidhi ndoo ya mafuta kwa kituo hicho chenye lengo la kuhudumia watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kuwapa mahitaji muhimu kama vile elimu, afya, chakula, malazi, mahitaji ya shule, pamoja na huduma za kisaikolojia na ulinzi dhidi ya manyanyaso. ![]() Viongozi wa kituo hicho wakimshukuru Mstahiki Meya Jerry Silaa. ![]() Meya wa Manispaa Mstahiki Jerry Silaa akibadilishana mawazo na baadhi ya viongozi wa kituo hicho mara baada ya kukabidhi zawadi za vyakula ikiwa ni mchango wake kwa vijana hao katika kusherehekea mwaka mpya 2012/2013. Kila mwaka wakati wa sherehe za mwaka mpya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala yeye binafsi hutoa sadaka kwa wahitaji kwa kumshukuru Mungu kwa kumuwezesha kumaliza mwaka salama. Leo Mstahiki Meya Jerry Silaa ametoa chakula kwa kituo cha Watoto Yatima na watoto Yatima na watoto Waishio Katika Mazingira Hatarishi cha Tushikamane Children’s Care Trust Fund ambapo pamanapo majaliwa hapo kesho atakula chakula pamoja nao. Asasi hiyo ya Tushikamane Children’s Care Trust Fund ilianzishwa mwaka 2001 na kupata usajili wa kudumu mwaka huo huo ili iweze kujiendesha kwa mujibu wa sheria za nchi. “Nafsi ni nyonge” tusameheane, maisha yaendelee. Karibu 2013 kwa ufanisi zaidi @MichuziJr31/12/2012 Wapendwa ndugu,jamaa na marafiki popote pale mlipo,yamebaki masaa kadhaa kuuaga mwaka 2012,ambao kwa hakika ulikuwa na changamoto nyingi za kimaisha,dhoruba za hapa na pale wengi zilitukumba, lakini kwa kudra za Mwenyezi Mungu akatushika mkono akatuinua na maisha yakaendelea. Binafsi mpaka dakika hii namshukuru Mungu nikiwa mwenye afya njema kabisa.Maisha ya sasa Wanadamu wengi wamekuwa dhaifu kwa mambo mengi, lakini Mungu ndiyo njia sahihi wa kumtumia katika sala zako kuyashinda majaribu na madhaifu ya Dunia.Yako mengi ambayo naweza nikayaandika hapa lakini bado yasitoshe pia.Nasema asanteni kwa ushirikiano wenu mkubwa kwa namna moja ama nyingine, kama kuna mahali nilikosea,tukakwaruzana kidogo basi "NAFSI NI NYONGE" Tusameheane na maisha yaendelee. Tunahamia mwaka mwingine mpya kabisa 2013,basi na tuendelee na ushirikiano huu tuliokuwa nao kwa mambo mbalimbali yenye kujenga na kuleta tija katika maisha yetu, Mwaka 2013 uwe wa kuhakikisha kweli sote pia tumehamia kwenye mfumo wa kidijitali,tushauriane,tuelemishane tunyooshane njia iliyo sahihi ili kila mmoja kila wakati abaki nafsini mwake mwenye furaha daima,Pia tumtangulize Mungu kila wakati kwa kila jambo ili pia azidi kuzibariki kazi za mikono yetu daima. Kwa Blogaz wenzangu,changamoto nyingi tumekumbana nazo 2012,ikiwemo tatizo kuu la KUKOPY NA KUPASTE.! Na nyinginezo nyingi tuzijuazo zinatusumbua kwa namna moja ama nyingine,basi ni nyema 2013 iwe ya kuzitafutia ufumbuzi,kama si kuzimaliza kabisa basi angalau tuendelee kuzipunguza ili kuzimaliza kabisa, huku suala la kujituma na ubunifu vikiwa ndio ngao kuu ya mabadiliko miongoni mwetu.Ushirikiano tuliokuwa nao umeonesha tuna uwezo mkubwa wa kuisadia jamii inayotuzunguka na hata serikali pia kwa namna moja ama nyingi,basi tusimame kidete kuhakikisha ushirikiano huu hauteteleki ama haupotei kirahisi,badala yake tuiimarishe zaidi kila kona . Natoa shukurani za dhati kabisa kwa makampuni na wadau mbalimbali ambayo/ambao kiukweli yametoa mchango mkubwa kuhakikisha tunasonga mbele na libeneke hili , si vibaya nikiyataja makampuni hayo kuwa ni Serengeti Breweries Ltd,Airtel, Bayport, Msama Promotions Ltd, kampuni ya R&R, Dada Teddy Mapunda, Hoyce Temu, Blogaz wote (bila kinyongo) na wengine waliotupa hatua ya kusogea kwa namna moja ama nyingine, Mungu awabariki sana. Asanteni Nawatakia heri ya sikukuu ya Mwaka mpya. * Tembelea tovuti ya Shirika la Viwango kuona ikiwa takwimu za sensa 2012 zimeongezwa: www.nbs.go.tz Othman Khamis Ame Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar 31/12/2012. Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ina idadi ya watu Milioni 44,929,002 kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti mwaka huu wa 2012. Matokeo hayo yanaonyesha ongezeko la idadi ya watu Nchini Tanzania lililofikia watu Milioni 33,000,000 ikilinganishwa na lile la sensa ya watu la Milioni 12,313,054 baada ya Uhuru . Akitangaza matokeo ya awali ya sensa ya idadi ya watu katika viwanja vya Mnazi Mmoja Mjini Dar es salaam Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema matokeo hayo yanaifanya Tanzania bara kuwa na Idadi ya Watu Milioni 43,625,434 wakati Zanzibar ina watu Milioni 1,303,568. Rais Kikwete alifahamisha kwamba takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania inakadiriwa kufikia watu zaidi ya Milioni 51,000,000 ifikapo mwaka 2016 kiwango kisichokidhi mahitaji halisi ya uchumi na mipango mengine. Dkt. Kikwete alitahadharisha kwamba idadi ya watu imekuwa kwa kiwango kikubwa na ongezeko lijalo linaweza kuwa mzigo mkubwa kwa Taifa ambapo alishauri kuwepo kwa mikakati katika kipindi cha miaka minne ijayo ili kukabiliana na ongezeko hilo. Alizishauri familia kuzingatia zaidi umuhimu wa suala la kuwa na uzazi wa mpango kwa lengo la kuwawezesha wazazi kuwa na uwezo na mbinu za kuzihudumia familia zao. Rais Kikwete aliupongeza Umma, Washirika wa Maendeleo pamoja na Viongozi wa nyadhifa tofauti kwa juhudi zao zilizopelekea kufanikisha zoezi ya sense ya watu na makazi na kuviomba vyombo vya habari vilivyotoa mchango mkubwa katika zoezi hilo kuendelea kuelimisha ummamatumizi bora ya Takwimu za sense kwa kudumisha ustawi wa Jamii. Akimkaribisha Mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa awali wa matokeo ya sense ya watu na makazi Mwenyekiti wa Kamati kuu ya Taifa ya Sensa ambae pia ni Waziri Mkuu Mh. Mizengo Peter Pinda alisema asilimia 90% ya gharama za zoezi zima la sense limesimamiwa na Serikali yenyewe. Mh. Pinda alisema Kiwango hicho kimepindukia asilimia 20% ya gharama za sensa ikilinganishwa na Sensa ya mwaka 2002 ambapo zaidi ya asilimia 70% zilitumika katika zoezi hilo. Akitoa salamu wakati wa uzinduzi wa matokeo ya awali ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 mwenyekiti Mwenza wa kamati kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema matokea ya sense yatakuwa na maana katika Taifa pale Taarifa zake zitakapotumika kikamilifu katika kupanga maendeleo ya Nchi. Balozi Seif aliwaomba washirika mbali mbali zikiwemo Taasisi za Serikali, Sekta binafsi, washirika wa maendeleo na Wananchi kuzifuatilia takwimu za sense kwa kuzitumia katika kupanga mipango ya maendeleo katika maeneo yao ya kazi. Alisema hatua hiyo itasaidia kufanikisha malengo ya mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Tanzania (MKUKUTA) na mpango wa kukukuza uchumi na kupunguza umaskini Zanzibar (MKUZA). Mwenyekiti huyo mwenza wa Kamati Kuu ya Sensa Tanzania Balozi Seif amewashukuru Viongozi wote wa juu, kati, Wananchi pamoja na washirika wa maendeleo kwa kuitikia wito wa serikali zote mbili wa kuwataka washiriki katikamzoezi la sensa ya mwaka 2012. Naye kwa upande wake mwakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa Nchini Bibi Maryam Khan alisema Taasisi za Umoja huo zitaendelea kusaidia kitaaluma na uwezeshaji katika kuona Mataifa wanachama yanafanikiwa katika utekelezaji wa Mipango yao ya Maendeleo. Bibi Maryam Khan alisema sensa ndio msingi muhimu inayotoa mwanga wa mipango ya maendeleo kwa kuimarisha miundo mbinu na kuipongeza Tanzania kwa juhudi zake za kujiletea maendeleo kwa kutambua umuhimu wa kujua idadi ya watu wake. Mapema Kamishna wa Sensa Tanzania Hajat Amina Mrisho alisema watendaji wa kamati ya sensa watahakikisha machapisho yote ya sensa yatatolewa na kuchapishwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Hajat Amina ameelezea faraja yake kutokana na watendaji wake kutimiza ahadi ya kutangaza matokeo ya sensa kama ilivyojipanga na inajivunia ufanisi mkubwa iliyoupata katika zoezi zima la sense ya watu na makazi ya mwaka 2012. “ Katika kipindi kifupi tumeweza kutoa matokeo ya awali ya sense ambapo inaonyesha umahiri mzuri walionao watendaji wa sense. Uzoefu wa Kitaifa na Kimataifa mara nyingi unaonyesha kuchelewa kwa matokeo ya takwimu za Sensa”. Alifafanua Hajat Amina Mrisho. --- via ZanziNews blog Mwaka 2012 ndio huoo umetokomea, ni vizuri kuangalia yaliyopita ili kujitayarisha na yajayo. Muziki wa nchi yetu ulitawaliwa na muziki wa Bongoflava, Taarab, muziki wa bendi, matarumbeta, muziki wa Enjili, na muziki wa kiasili. Si siri kuwa muziki wa Bongoflava ndio uliokuwa ukitawala katika vyombo vya habari na sehemu nyingi za maonyesho ukifuatiliwa na muziki wa Taarab na muziki wa enjili. Katika muziki wote huu jambo lililokuwa wazi ni kuwa waimbaji ndio waliokuwa wakipewa kipaumbele katika tasnia hii. Waimbaji katika aina zote za muziki uliotajwa hapo juu ndio waliotajwa na kupewa sifa kwa ubora wa muziki. Kumekuweko na mashindano kadhaa ambayo yote yamejikita katika kutafuta vipawa vya waimbaji japo mara nyingi yamejitambulisha kama mashindano ya kusaka vipaji mbalimbali. Hakuna ubishi muziki wa dansi na muziki wa asili ndio muziki uliopewa muda mchache sana katika vyombo vya habari. Na hata katika muziki huo, bendi ambazo zimejikita kufuata mipigo ya Kikongo vilipewa nafasi zaidi ya bendi ambazo zimejichagulia njia nyingine za muziki wao. Kuna sababu kadhaa ambazo zimefanya muziki wa bongoflava kuchukua nafasi zaidi katika vyombo vya habari, la kwanza ni uwingi wa kazi za bongoflava zinazorekodiwa. Karibu kila mji una studio ya aina moja au nyingine, na katika studio hizo kazi nyingi zaidi zinazorekodiwa ni aina hiyo ya muziki, hivyo kutokana na uwingi wa kazi hizo ni wazi kabisa ndizo ambazo zitaendelea kutawala anga la vyombo vya habari, na pia ni kutokana na mfumo wa vyombo vyetu vyote kujikita katika mfumo wa aina fulani tu za muziki. Kwa mtizamo wangu heka heka za muziki wa Enjili zilipungua 2012. Yale matamasha makubwa ya muziki huo yalipungua sana, na hata nyimbo za kushtua jamii hazikuwa nyingi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Muziki wa Taarab haujaleta mabadiliko kimuziki, mengi yaliyofanywa katika 2012 ni marudio tu ya ubunifu uliofanyika nyuma. Kama vile uanzishwaji wa kucheza show katika taarab, upigaji wa gitaa na kuliachia pekee yake kama ilivyokuwa kwa bendi kuachia gitaa la rhythm miaka kabla ya tisini na zile video za kucheza mbele za viwanja vya hoteli. Kumekuweko tu ubunifu wa misemo na mipasho, jambo tena ambalo limesababisha kuenziwa zaidi kwa waimbaji tu katika fani hiyo pia. Bendi ziko katika wakati mgumu, wakati wanamuziki wengi wa bendi wakilalamika kuwa muziki wa bendi haupigwi, kumekuweko na jitihada ndogo za bendi kurekodi nyimbo mpya, maelezo mengi yamekuwa ni kuhadithia enzi ambapo muziki wa bendi ulitawala na kuona kama hiyo ni sababu tosha ya muziki huo kurushwa hewani. Bendi chache zilizorekodi hazijaja na nyimbo zilizoweza kuteka umma wa wa Tanzania na hivyo kusababisha muziki huu kukosekana katika anga za muziki. Matangazo mengi ya muziki wa dansi yamekuwa ni kutangaza rap mpya au kupatikana kwa msanii mpya, lakini kiujumla hakujakuwa na kitu kipya katika muziki wa bendi. Muziki asili pia umekosekana kwenye vyombo vya habari kwa kuwa si vikundi vingi vya muziki huu vyenye uwezo wa kulipia gharama za studio ambao muziki huu unastahili kurekodiwa. Studio nyingi zimejengwa kwa ajili ya muziki wa aina ya Bongoflava tu, zile studio za kuweza kuruhusu kundi la muziki wa asili kurekodi gharama yake huwa ni kubwa sana. Kundi la Makirikiri lilitakiwa kuwa elimu tosha kwa wasanii wa muziki wa Kiasili, kuwa na muziki huo ukifuata taratibu nzuri ya kurekodiwa unauza vizuri sana, bahati mbaya kuna vikundi sasa vimeacha muziki na ngoma zao, vinaiga uchezaji wa Makirikiri. Pengine watu watasema nimesahau muziki wa kwaya, sijausahau, kwa kweli muziki huu umebaki hasa kwenye muziki wa Enjili. Hapo zamani ulikuwa ukitumika sana kwenye siasa na kampeni , lakini kwa mwaka 2012 hali imekuwa mbaya kwa muziki huu. Pamoja na kuwa wengine wangeweza kusema tunasonga mbele katika muziki, kwangu mimi naona tunarudi nyuma kitaaluma. Tasnia inaingiza pesa nyingi zaidi, na hata kuna wasanii walioingiza pesa nyingi sana, lakini kwangu hilo si kipimo cha maendeleo katika tasnia hii. Kama nilivyoanza kusema washika maikrofon wamekuwa ndio alama ya muziki wa Tanzania. Muziki ni zaidi ya kuimba. Katika kuimba sauti nzuri ya muimbaji ni muhimu, na ninashukuru kwa hilo tunao waimbaji wazuri wengi sana, lakini ule muziki unaomsindikiza muimbaji ni muhimu sana kwani ule hauna mipaka wala lugha, na ndio unaoweza kutufungulia mlango wa soko la kimataifa. Wengi tunapenda sana muziki wa kutoka Kongo, Nigeria, South Africa, pamoja na kuwa hatujui hata moja wanaloliongelea tunaupenda muziki huo kutokana na mpangilio wa vyombo vyao. Kutokujali wapigaji katika mfumo wa nchi yetu ndio unatupelekea kuwa watu wa ‘copy and paste’ wa upigaji wa muziki wa nchi nyingine. Ukiorodhesha nyimbo zote zilizotikisa nchi hii kwa mwaka 2012 utagundua asilimia kubwa ya muziki uliotumika ulikuwa ni wa kunakili kutoka muziki wa nchi nyingine, Nigeria, Congo na Afrika Kusini ndio wamekuwa waalimu wetu wakuu. Ushauri kwa maproducer wa Bongoflava, kuangalia pia muziki wetu wa asili humu ndani ya nchi ili tuje tumalize 2013 na kitu chetu ambacho Wanaigeria, Wakongo nao pia waige toka kwetu. Inawezekana sana maana wimbo wa Weekend wa Afro70 uliwahi kuweko katika kumi bora 1972, Nigeria. Muziki wa Enjili pamoja na kuwa ndio unaotegemewa kutufundisha maadili, ulikuwa na kasoro moja kubwa nayo ni kukosa maadili kwa kucopy na kupaste. Nyimbo nyingi zilizokuwa maarufu na kuteka hisia za maelfu ya watu zilikuwa ni kuiga moja kwamoja kutoka Afrika ya kusini. Najiuliza je ndio kilichopunguza moto wa muziki huu 2012? Kulikuwa hakuna za kukopi? Wanamuziki wa Enjili kama ilivyo kwa ushauri kuhusu Bongoflava, ni muda wa kurudi nyuma na kutumia raslimali ya utamaduni iliyoko kuleta mabadiliko na kukuza soko la muziki huo. Tasnia ya muuziki wa Tanzania katika tafiti moja wapo umeitwa ‘the radio-driven contemporary music industry’. Kwa maneno rahisi, tasnia ambayo imekuwa inaendeshwa na radio. Radio zimekuwa na uwezo wa kumpandisha na kumshusha mwanamuziki, kumtafutia soko, kumzibia soko na kadhalika. Hali hii ikisindikizwa na rushwa ambayo imetapakaa katika jamii yetu, unapata picha kuwa kungeweza kukawa na sura bora au tofauti ya muziki hali isingekuwa ilivyo. Kuna ripoti za watu kutoa hongo nyimbo za wenzao zisipigwe, hongo ili nyimbo zipigwe, visasi vya kuzuia nyimbo zisipigwe na kadhalika. Na katika jamii ambayo imekuwa na kawaida ya kutegemea vyombo vya habari kujua muziki gani mpya na mzuri, uwanja huu si uwanja ulio tambarare hata kidogo. Bahati mbaya inaonekana wenye vyombo hivi wako mbali na ukweli unaoendelea katika vyombo vyao au kwa kutokujua au kupuuza. Janga hili limevikumba hata vyombo ambavyo vinaendeshwa na taasisi za dini. Wanamuziki wa muziki wa Enjili nao pia wanalia kudaiwa rushwa na watangazaji wa radio za Enjili!. Nakumbuka siku niliyopata nafasi kuongea na kiongozi mmoja wa dini ambaye Kanisa lake linaendesha kituo cha radio, nilipata mshangao baada mkuu huyo, kuanza kutetea watangazaji wake badala ya kuamua kufanya uchunguzi wa tuhuma. Umefika muda wa radio kuanza kujigawa kimuziki. Ni kichekesho mji kuwa na vituo vya radio 30 halafu vyote vinapiga aina hiyohiyo ya muziki, wakati kuna aina mbalimbali za watu. Ajabu ni kuwa wenye radio wanajua kuwa katika nchi nyingine unaweza kukuta radio iliyoamua kupiga aina fulani tu ya muziki, Jazz Radio, Country music Radio, Classic Music Radio, lakini hilo limekuwa gumu kwao kutekeleza hapa. Kuwe na utofauti, Wasikilizaji tuko wa aina tofauti. Vyombo vya habari viijitahidi kupata wataalamu husika wa aina tofauti za muziki, muziki unaviingizia vyombo hivyo mabilioni ya fedha, vyombo vya habari viupe heshima yake. Bila muziki hakuna radio. Magazeti yamekuwa mstari wa mbele katika kutangaza aina mbalimbali za wasanii na sanaa. Pamoja na hongera kwa kazi nzuri lakini bado kuna nafasi kubwa ipo tupu, hakuna wataalamu wa uandishi wa habari za muziki. Hivyo habari nyingi za muziki zinaandikwa na waandishi kama wapenzi wa muziki na si wataalam wa uandishi wa muziki, jambo ambalo liko tofauti na uandishi wa michezo kwa mfano soka. Unaweza ukasoma habari ya soka ambapo mwandish atakueleza nafasi za wachezaji, kama ni faulo, ni nini kilisababisha, na kama ni goli lilikuwa ni la kichwa au kona au penalty, hili haliko katika muziki. Utaambiwa tu bendi ilipagawisha, au msanii fulani ateka nyoyo za wapenzi, na maelezo ya juu juu kama yale, kunahitajika kuanzishwa mafunzo ya elimu ya uandishi wa kazi za sanaa. Hili litapunguza hata vurugu kama zilizotawala mwaka huu ya wapiga picha kufikia hata kulala chini ili tu wapate picha ya nguo za ndani za msanii na hayo ndio kuwa maelezo makuu ya onyesho zima la muziki. Ikiwa kulikuwa na mchango wa serikali katika muziki, basi ulikuwa mdogo au ulikuwa ni kwa shughuli maalumu lakini si kwa kutengeneza mazingira ya kuwezesha unafuu kwa wanamuziki kwa ujumla. Idara ya Utamaduni imeendelea kupata bajeti ndogo ambayo imefanya Baraza La Sanaa La Taifa kuendelea kubaki Dar es Salaam tu, likibangaiza kuweko kwa kutegemea kutoa vibali mbalimbali kwa wasanii, na nguvu zake kuonekana Dar es Salaam tu. Na kwa kuwa hakuna Maafisa Utamaduni Mkoa, na Maafisa Utamaduni Wilaya na Manispaa wako chini ya serikali za mitaa hivyo kuwa wizara tofauti na Waziri wa Utamaduni, nguvu za serikali katika utamaduni ni 0. COSOTA chombo ambacho shughuli yake ilikuwa ni kulinda hakimiliki za wasanii na ambacho kilikuwa chini ya wasanii, kwa kinyemela kabisa kimerudishwa katika mikono ya serikali, lakini bado kinakusanya mirabaha 'kwa niaba ya wasanii' huku kukiwa na bodi isiyo na uwakilishi wa wasanii kuanzia 2007. Swali utakusanyaje pesa kwa iaba yangu lakini huniruhusu kujua ni kiasi gani umekusanya, unazitumiaje na ukiulizwa unakuwa mkali!!!!!!? Kuna wasanii wamekuwa wakidai kurudishiwa COSOTA, ushauri wangu wasanii wakae wajipange na kuelewa vizuri sheria ya Hakimiliki kabla ya kujitwishwa zigo hilo la miba. Katika miezi 6 ya mwisho ya 2012 kumejitokeza spidi kali ya Mamlaka ya Ukusanyaji wa Mapato kutengeneza mazingira ya kukusanya mapato kutokana na mauzo ya kazi za muziki na filamu. Kimsingi kulipa kodi ni wajibu wa kila mwananchi na wasanii ni wananchi pia, lakini taratibu zake ndio zinanipa utata, hasa pale ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikitangazwa kuwa njia hii itasaidia wasanii kwa kupunguza kuibiwa. Sentensi hii inaonyesha wazi anaeiongelea aidha hajui mfumo wa biashara ya kazi muziki, au kwa makusudi anapotosha ili kuficha kitu. Wasanii wengi huwa wamekwishalipwa kwa kazi ambazo zimesambaa na ziko barabarani zinaibiwa, wanaoibiwa ni wasambazaji. Hivyo kulinda kazi hizo unamlinda msambazaji si msanii. Pia kuanza kukusanya kodi kwa kazi hizi kumepewa jina ‘kurasmishwa kwa kazi ya usanii’, kuna mabilioni wasanii wanatakiwa walipwe na watumiaji wa kazi za sanaa, kama radio na TV, mapromota, waajiri na kadhalika hakuna anaeliongelea hilo wala hakuna anaetamka takwimu hizo. Kuna kazi ya kurudisha mitaala ya masomo ya sanaa mashuleni, kurudisha vyuo vya walimu wa sanaa, kurudisha maafisa utamaduni kuwa chini ya Wizara ya Utamaduni kuwawezesha kufanya kazi zao kadri ya sera ya Utamaduni, na mengine mengi ya aina hiyo ndio ningeona kurasimisha kazi za sanaa, lakini kukusanya kodi tu kwa kazi ambazo hata hivyo mikataba yake mingi inautata na kuita urasimishaji si sahihi. Katika nchi nyingi critics au watu ninaoweza kuwaita kiswahili wakosoaji, huwa ni muhimu katika maendeleo ya sanaa, watu hawa hupata heshima kutokana na kuweza kuangalia mapungufu katika kazi za sanaa na kuyasema, jambo ambalo hupelekea wasanii kujirekibisha na kutengeneza kazi bora zaidi. Hapa kwetu kutoa ushauri ni kutafuta matusi, toka kwa wasanii wenye kazi husika, vyombo vya habari na hata sehemu ya jamii, umefika muda wahusika kuchukua uchambuzi kama changa moto za kuboresha kazi. Niliyoyataja hapa yote yako wazi ninachotegemea ni kuona 2013, hatua zinaanza kupigwa kurekibisha, ili wanamuziki wa nchi hii nao wapate nafasi sawa na wengine wa nchi nyingine. John Kitime 31.12.2012 Sinza, Dar es Salaam VOTING FOR NEW SEVEN NATURAL WONDERS OF AFRICA ENDS ON DECEMBER 31, 2012 Tanzania Tourist Board (TTB) wishes to inform Tanzanians and the general public that the competition to vote for entries into the list of SEVEN NATURAL WONDERS OF AFRICA, conducted via the Website, http://sevennaturalwonders.org involving twelve (12) tourist attraction sites on the African continent will come to an end on December 31, 2012. Tanzania was the only blessed country with the most entries in the list: these are Mount Kilimanjaro, the Ngorongoro Crater, and the Serengeti National Park. Tanzania Tourist Board, would like to take this opportunity to sincerely thank all those who voted for Tanzania tourist attractions and requests all those who have not yet casted their votes to seize this opportunity and vote for the entry of all the Tanzania tourist attractions into the list of the NEW SEVEN NATURAL WONDERS OF AFRICA. Issued by the Managing Director TANZANIA TOURIST BOARD ![]() Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Rene Meza Utamaduni wa watanzania kujiunga na huduma za Bima nchini kama njia mojawapo ya kukabiliana na gharama za majanga na matukio mengine ya asili ikiwemo kifo umeaonekana kuongezeka kufuatia kuwepo kwa urahisi wa kukata na kujiunga na bima kupitia simu za mkononi. Kuongezeka kwa utamaduni huo wa kukata bima kunasaidia kuondokana na dhana ya kwamba kukata bima ni sawa na kujitakia majanga jambo mbalo hata hivyo halina ukweli na badala yake bima imekuwa msaada mkubwa kwa wanajamii katika kumudu gharama zitokanazo na majanga na matukio mengine yasiyoweza kuepukika. Kuwepo kwa urahisi huo ni matokeo ya ubia wa kibishara kati ya kampuni ya Bima ya Heritage na Kampuni ya Vodacom Tanzania ambapo sasa mteja wa Vodacom ameewezeshwa fursa rahisi na ya uhakika ya kujiunga na huduma za bima kupitia simu za mkononi kutumia huduma ya M-pesa. Hii ni huduma ya kwanza na ya aina yake inayopatiakana Tanzania pekee. “Tumeshuhudia mageuzi makubwa katika sekta ya bima nchini tangu tulipoanzisha utaratibu wa kukata bima kupitia simu za mkononi huku mteja akifanya malipo ya bima yake kwa njia ya M-pesa, tunaamini ubia huu umekuwa wa faida kubwa kwa jamii.”Amesema Mkuu wa Kitengo cha huduma za bima wa kampuni ya Heritage Tanzania, Bw. Joseph Mardai “Ni wazi sasa upo urahisi na jamii inaanza kuona umuhimu wa bima. Tayari watu kadhaa wameshafanikiwa chini ya mpango huu ambapo kampuni ya Heritage Tanzania imeweza kuwalipa wanufaika wa bima hizo za Upendo na Faraja kiasi cha fedha kusaidia gharama za mazishi kwa urahsi zaidi kupitia M-pesa, hakuna usumbufu wala gharama za ziada.”Ameongeza Mardai Mardai amesema mabadiliko ya kifikra yanayoanza kuonekana hivi sasa nchini kuhusu huduma za bima hasa kwa bima zinazohusisha vifo kutasadia kwa kiwango kikubwa namna jamii inavyoweza kuondokana na hofu na mzigo mkubwa wa kugharamia shughuli za mazishi na matibabu “Hakuna anaependa kuzungumzia kifo lakini tunapogundua kwamba hakuna mwenye uwezo wa kukizuia wala kutambua ni wakati upi kitamfika ni dhahiri tunapaswa kutafakari namna bora ya kupunguza mzigo kwa familia zetu katika kugharimia shughuli za mazishi.” Amesema Mardai Na kuongeza kuwa “Huduma za Faraja na Upendo inatoa namna bora ya kupata suluhisho.” Chini ya utaratibu wa ukataji wa bima kwa njia ya M-pesa mteja anaweza kukata na kulipia bima yake wakati wowote na mahali popote na hata kupokea fidia ya malipo ya bima yake pale tatizo lililokatiwa bima linapotokea ambapo fedha hizo hupokelewa na wanufaika aliowaandikisha kwenye mkataba wa bima. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Rene Meza amesema ubunifu katika Vodacom unaendelea kudhihirisha azma ya kampuni hiyo katika kubadil na kurahisisha maisha. “Tumekuwa na dhamira hiyo ya kuhakikisha teknolojia ya simu za mkononi haishii katika kupiga na kupokea simu au kutuma ujumbe mfupi wa maneno tunataka kuona maisha ya watu yakiwa rahisi na mepesi zaidi kupitia simu zao za mkononi. Huduma hii ya Bima ni uthibitisho mmojawapo wa dhamira inayotuongoza katika biashara.”Amesema Meza “M-pesa imeleta mapinduzi makubwa hapa nchini jinsi jamii inayoishi, hatuna sababu yakurudi nyuma tutaendelea kuongoza katika ubunifu na kuziunganisha huduma mbalimbali katika mfumo wa M-pesa ili kuzileta karibu na wananchi.”Alisema Meza na kuongeza “Tayari kwa sasa biashara nyingi zimeshaunganishwa na mfumo wa M-pesa kuanzia usafiri wa anga, malipo kwenye maduka makubwa – Supermarkets, uchangijaji katika mifuko ya hifadhi ya jamii, malipo ya ving’amuzi n.k.” Hivi karibuni kampuni ya Heritage ililipa wateja wake wawili wa kwanza kabisa tangu kuanza kwa huduma ya bima kwa kwa njia ya M-pesa. Wateja hao ni mke wa Bw. Mathias Mahunda, Bi. Fransisca Mahunda ambae mumewe alikuwa mteja aliyekuwa na Bima ya Upendo aliyefariki dunia Novemba 17, mwaka huu ambae alilipwa kiasi cha sh, milioni mbili. Mwengine aliyenufaika na bima hiyo ni mke wa marehemu Kulwa Mtangaki, Bi. Julieth Mtangaki, ambaye mumewe marehemu Bw. Mtangaki alifariki dunia Novemba 12 kwa ajali na bima yake ya Faraja iliwezesha mkewe kupewa kiasi cha sh. 200,000 kama kusaidia gharama za Maziko. Katika hatua nyengine wateja mbalimbali wa Vodacom wamekuwa wakinufaika na huduma za bima kwa kupatiwa Sh. 200,000 kama promohseni ya kufanya miamala kumi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja. “Kila mteja wetu anaefanya miamala kumi kwa mwezi tunamzawaidia bima ya Sh. 200,000 katika mwezi unaofuata ambayo hudumu kwa kipindi cha mwezi mmoja na anaweza kunufaika na fidia ya bima iwapo atakutwa na umauti ndani ya kipindi hicho cha mwezi mmoja fedha ambazo hulipwa kwa wanufaika anaowapendekeza.”Alisema Meza Mteja hupaswa kuandikisha majina ya wanufaika wake kupitia utaratibu unaoelezwa kwenye ujumbe mfupi wa maneno anaotumiwa kujulishwa kuhusu kuingiziwa kiasi hicho cha fedha (200,000) katika akaunti ya bima. |










RSS Feed
