wavuti
wavuti logo Facebook icon Facebook icon Twitter icon Subscribe RSS
 
Ndiyo, ujumbe umefika, lakini, lugha imenyewa! Haifai kuwa hivi.
Picture
Usahihi ni: Hapauzwi. Utatapeliwa. (picha imepigwa eneo moja huko Tegeta, Dar Es Salaam)
Lipo tatizo kubwa kwa baadhi ya watu wa makabila fulani nchini Tanzania kuhusiana na matumizi ya herufi, 'R' na 'L' au 'H' na 'U' katika matamshi na hata kwenye maandishi. Pia, wapo wale ambao hushindwa kutofautisha kati ya herufi 'S' na 'Z' au 'P' na 'B' ama 'V' na 'F' na 'DH' na 'Z' na kadhalika.

Ingawaje kwa maneno mengine huwa si rahisi kupoteza maana kusudiwa, makosa hayo bado huweza kuleta maana tofauti kabisa na iliyokusudiwa, hasa kwa mgeni au mwanafunzi wa lugha ya Kiswahili.

Kwa mfano, neno 'ukiri' ni tofauti na neno 'ukili' au 'karamu' na 'kalamu'. Vile vile 'kazi' ni tofauti na 'kasi' kama ilivyo 'vuma' ikawa tofauti na 'fuma'. Kadhalika, 'barua' ni tofauti na 'parua' ama 'dhana' na 'zana'.

Matumizi yasiyo sahihi ya maneno hayo humlazimisha msomaji kujua maudhui ya habari kwanza ili kuweza kupata maana kusudiwa. Hii si vyema kwa wageni wanaojifunza lugha tunayojisifia kwayo kuwa ni asili yetu.
 
 
Kusema, 'both adults & students' nadhani ni tafsiri ya moja kwa moja toka Kiswahili, haijakaa sawa. Mlinganisho uliotumika hapo ni wa makundi mawili ya nyanja mbili tafauti. Ni sahihi kulinganisha, 'Adults and Youths' au 'Students and Non-Students' kwa maana 'adult' akiingia darasani anakuwa 'student' vile vile 'student' anaweza kuwa 'adult'... namna gani vipi pale? Ipo haja ya wataalamu wa lugha kurekebisha haya.
Picture
neno sahihi kwa lugha ya Kiingereza ni 'adults' kwa maana ya 'watu wazima' kwa lugha ya Kiswahili
"Classes za Kiingereza..." yaani ni mwendo wa "ku-mix" lugha tu, haijalishi ni shuleni, mtaani, bungeni....!l

Ukiuliza sana utajibiwa, 'lakini si umeelewa?' mmh! Wewe weka bango lako hivyo, kisha washindani waweke lao lililoandikwa kwa ufasaha, hapo ndipo utaelewa maana ya 'akili ya kuambiwa, changanya na yako...".

Ndivyo tutakavyozungumza katika ushindani wa "Isti Afrikan Markiti"? 'ndo twaboronga hivyo halafu soko la pamoja likikolea, twakubali na kulalamika 'wenzetu wanatuzidi sisi hatujui chingereza', il hali wakati wa kukosoana kuwekana sawa, twaishia kuzodoana! Afanaleki! sisi ni sisi tu, chapa mfanowe "nehi".
 
 
Picture
Ipo herufi 'r' katikati ya 'a' na 'k' katika neno la Kiingereza, 'parking' lenye maana ya 'maegesho' kwa Kiswahili. Tutumie lugha fasaha, tusichoke kukosoana tunapokosea. Nami hukosea na hukubali kukosolewa.
 
 
Picture
Neno 'passport' la lugha ya Kiingereza lina maana ya 'pasi' kwa lugha ya Kiswahili. Nadhani walipaswa kuandika, 'passport size photo' kwani sehemu hii kwa uzoefu wa 'vijiwe vya mjini' hapa ni mahala pa kupigia picha kwa ajili ya pasi mbalimbali za utambulisho, asilani, hili si eneo maalum la Serikali kwa kutolea 'pasi'.
 
 
Siyo utani, kejeli au kukebehi, ukweli ni kwamba sijaelewa maana ya tangazo hili. Kwa kuitizama picha napata wazo kwamba tangazo linahusiana na mikanda ya filamu inayoonekana hapo.
Picture
photo credit: Maggid Mjengwa
Hivi kweli lugha ya Kiswahili imeshabadilika na kujaa maneno hivi? Haya maneno tafsiri yake inapatikana kirahisi kweli? Mlengwa katika lugha hii ni kijana wa kijiweni, Mtanzania, Mgeni au mtu gani hasa?

Nadhani neno 'mtaharam' aliataka kuandika, 'mtaalamu'
Je, neno 'kupwenti' alitaka kuandika, 'ku-point' ama neno hili tayari lina maana tafauti?
Na neno 'muvu' ni Kuswahilisha neno la Kiingereza, 'move' ama maana kusudiwa ni nyingine?

Pengine wakati  mwingine mambo mengine yanahitaji kupuuziwa kwa kuwa  'hayanihusu', wale yanaowahusu watakuwa wameupata ujumbe. Tatizo nililo nalo, akiniuliza mtu mwingine maana ya ujumbe huo nitamjibu vipi? Pengine nitabaki tu kumwambia 'sijui' au 'nadhani' kama nilivyonyambulisha hapo juu, na pengine nitamweleza tu kuwa, 'kwa hilo, mimi kama wewe nimetoka kapa'. Mbaya zaidi ni ikiwa atakuwepo mgeni au mtalii akapekenyua kamusi yake na asione maneno hayo, kisha aniulize maana yake, pengine nitamjibu, 'lugha ya wahuni hiyo' au 'lugha nisiyoijua maana yake' na sidhani kama inawakilisha kabila lolote.
 
 
Picture
credit: Maggid Mjengwa blog
Nimefahamishwa, "hii GH ipo Ifakara, ni nzuri na huduma poa kabisa, ila kwa hiyo 'ICE' no comment".

Wito wangu ni kuwa tujitahidi kuandika lugha mojawapo kwa ufasaha. Hata mgeni anayezungumza Kiingereza anatarajia kusoma Kiswahili fasaha ndipo aweze kutafsiri kwa kamusi aweze kupata maana kusudiwa. Ikiwa unaweza kuandika Kiingereza fasaha, basi fanya hivyo, la inashindikana, basi tafuta mtafsiri. Hiyo itaisaidia biashara yako kukua. Tujifunze kutokana na makosa haya na tuwasaidie wengine kurekebika.
 
 
Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, George Mkuchika ametoa tamko Bungeni lenye faraja kwa wanazuoni na  wadau wa lugha ya Kiswahili akiungwa mkono na Mheshimiwa Spika wa Bunge.
 
Kwa ujumla mheshimiwa Waziri na Spika wa Bunge kwa pamoja wameonyesha umuhimu wa Serikali na asasi zake kudumisha utamaduni wa kutumia lugha ya Kiswahili katika  fomu na shughuli zote rasmi pamoja na  mawasiliano yote ya Kiserikali.
 
Wakati hayo yakiendelea, ni muhimu Wanazuoni  na  wadau wote wa lugha ya Kiswahili tuungane na Serikali katika kuondokana na dhana la kuwekeza kwenye maendeleo ya lugha za kigeni.
 
Asasi za maendeleo ya lugha ya Kiswahili ziongeze uhamasishaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika maeneo yote muhimu yaliyotajwa na mheshimiwa waziri  na media zote ziachane na kabisa na matumizi ya 'KISWANGEREZA' katika utendaji wao wa kila siku.
 
Wenu kwa staha;
Ray Ephraim Ndewingiya Njau
Mdau na mtetezi wa Kiswahili
Dar es Salaam, Tanzania.
 
 
Shule ya Bloomington High huko nchini Marekani imeongeza rasmi lugha ya Kiswahili katika lugha  kuu tano za kigeni. Suala hili limenifanya nijiulize sababu hasa ya kufanya hivi na hatimaye nimejiaminisha kuwa, lengo la kufanya hivi huenda ni kutaka vijana na watu wa Taifa la Marekani kuelewa lugha mbalimbali za dunia kadiri wanavyoweza ili waweze kuwasiliana na watu wa mataifa mbalimbali kwa urahisi zaidi. Pengine laweza kuwepo lengo lililojificha la kuwataka raia wake wajifunze lugha mbalimbali, lakini ukweli haupingiki ya kuwa haiwezekani kumzuia mtu kujifunza lugha nyingine ikiwa amekusudia, nasi cha msingi  tunachoweza kukifanya ni kujifunza lugha zao ili kuweza kuwasiliana na watu wengi zaidi katika shughuli mbalimbali.

Faida za kujifunza lugha za kigeni ni nyingi. Baadhi ya faida hizo ni pamoja na:
  • Lugha inashikilia nafasi ya kwanza kati ya mojawapo ya vyanzo vya hali ya juu kabisa vya mawasiliano.
  • Kujifunza lugha ngeni ni kujua jinsi ya kuwasiliana na watu wa jamii husika ili kukidhi mahitaji kadhaa.
  • Lugha husaidia watu kupata ajira katika maeneo kadha wa kadha kama ualimu, ukalimani, biashara nk.
  • Kuijua lugha ngeni husaidia kung'amua siri za wazungumzaji, aghalabu, siri hizi zaweza kuwa mbaya. Hivyo, mtu anapoifahamu lugha ya watu wengine inakuwa vigumu kumsema kwa siri. Umuhimu huu wa kuijua siri ya mwenzio ndiyo unaohitajika katika ulimwengu huu uliogubikwa na matukio ya uhalifu na ugaidi wa kimataifa hivyo ikiwa kuna watu wana lengo baya na nchi fulani, basi inakuwa rahisi sana kuweza kunyaka maongezi na kufahamu mipango ya kihalifu na hivyo kukabiliana nayo.
Kifuatacho ni kipande cha utambulisho wa mafunzo ya lugha ya Kiswahili katika jimbo la Indiana, Marekani.
The main goal of the STARTALK Swahili student program is to introduce Swahili to Bloomington High schools, initially, as a nonresidential program. In the future we would like to offer it as a residential program and make it available to all Indiana high schools. The program will integrate the 5Cs of the National Foreign language Standards with a focus on the C of Communication and the C of Cultures. This will be a four week program with each week focusing on a particular cultural theme such as greetings, extended family, traditional clothes, food, and story telling. The first week will focus on greetings, introductions and talking about family members. The second week, students will learn about different kinds of food, ingredients required, and how to shop and bargain for them at the market. Week three will introduce students to the art of story telling using children’s stories and folktales. The last week of the four week program will concentrate on clothing with a focus on different uses of the traditional cloth, the kanga, and its sayings for indirect communication. This intensive program will be the equivalent of one semester of Swahili and students will get foreign language credits.

812-855-3323 • aomar@indiana.eduwww.indiana.edu/~afrilang
 
 
Picture
Zoezi la sensa ya kuhesabu idadi ya watu wanaoishi nchini Marekani limeweka historia kwa kuitambua na kuiongeza lugha ya Kiswahili katika orodha ya moja ya lugha za Kimataifa zilizopewa kipaumbele na kuchapishwa rasmi kama mwongozo wa dodoso ili kufanikisha zoezi hili.

Katika video iliyopo kwenye tovuti hiyo ambayo inatoa maelekezo kuhusu dodoso la sensa hiyo, mzungumzaji amekosea kidogo mahala fulani anaposikika akisema, '...masaba' badala ya 'saba' na mahala pengine ametamka, '...masita' badala ya 'sita' lakini kwa ujumla amesoma vizuri na katika lafudhi mojawapo ya Kibantu na inaeleweka. Bofya picha hapo kushoto (au bofya hapa) kutizama video hii. Ikiwa unataka nakala ya mwongozo huo wa sensa, unaweza kuipakua katika tovuti hiyo kwa lugha ya Kiswahili 2010.census.gov/2010census/language/swahili

 
 
Tujifunze Kiswahili sanifu.

(1)    Tunasema “Mahakama hii”
(2)    Tunasema “Mamlaka haya” (Uwezo/madaraka)  “mamlaka hii” (chombo/asasi)
(3)    Tunasema “Wakala huyu” (mtu anayefanya kazi ya uwakala) “wakala hii” (chombo/asasi inayofanya kazi ya uwakala)
(4)    Tunasema “Wawakilishi” (watu wanaowakilisha) “wawasilishaji” (watu wanaowasilisha)
(5)    Neno “Maombi” lina umoja na wingi:     “Ombi” (umoja) “Maombi” (wingi)
(6)    Neno “Saa” halina wingi.  “Masaa” si matumizi sanifu.
(7)    Neno “Wimbo” ni sanifu.  “Mwimbo” si sanifu.

Imeandikwa na:
R. Njau
Mdau na mtetezi wa Lugha ya Kiswahili.
Dar Es Salaam, Tanzania.