NIMEPATA kusimulia kisa cha kijana aliyehangaika sana kuusaka ukweli. Katika pitapita zake akaliona duka. Kibao kimeandikwa dukani; “Hapa tunauza ukweli”.
Dukani hapo ukweli unauzwa kwa kilo. Bei ya robo kilo ya ukweli imeandikwa, vivyo hivyo, bei ya nusu kilo ya ukweli. Lakini, mwenye duka hakuandika bei ya ukweli mzima, kwa maana ya kilo nzima ya ukweli.
Kijana yule akauliza; “Mie nataka ukweli kilo nzima, mbona hujaandika bei?”
“Alaa, unataka kilo nzima ya ukweli?” aliuliza mwenye duka. “Naam” Akajibu kijana yule.
“Basi, zunguka uje ndani nikuambie bei yake”.
Alipoingia ndani dukani, kijana yule akaambiwa; “Kijana, hatukuandika bei, maana, gharama ya ukweli mzima ni uhai wako. Je, uko tayari kulipa?”
Kijana yule akatimua mbio. Nyuma aliacha vumbi. Hakuwa tayari kulipa gharama ya ukweli mzima.
Yumkini ukweli utakaousema mwanadamu waweza usiwafurahishe wachache, walakini, ukawa wenye kuleta tija, furaha na matumaini kwa walio wengi.
Mimi nitasena hapa ukweli wangu, kuwa Baraza jipya la mawaziri ni mabadiliko ya sura ya Baraza lakini si mabadiliko ya mfumo
Ndugu zangu,
Ujamaa ni imani. Na Wajamaa tuko wengi nchi hii. Kuna tuliojifunza tangu utotoni, kwamba Ujamaa ni imani. Tunajitahidi kuishi kama tulivyojifunza. Kuishi kama tunavyohubiri sasa. Lakini, kama ilivyo kwa imani nyingine, ni jambo gumu, ni mitihani kila kukicha, naam, Uislamu ni mgumu, Ukristo ni mgumu. Hivyo basi, na Ujamaa pia.
Ndugu zangu,
Kama mtego ule wa panya, tutafanya makosa makubwa kama kuna watakaodhani, kuwa haya ya watu kuchinjwa na kujeruhiwa na mapanga yatawakuta watu wa kundi fulani tu. Tukiacha yaendelee, basi, yeyote yule, bila kujali dini, rangi, itikadi au hata wadhifa wake, anaweza kuwa mhanga wa maovu haya. Kama taifa, kwa pamoja tuwalaani wauaji hawa na wanaowatuma.
Pravda Na Izvestia- Ukweli Na Habari!
Ndugu zangu,
Leo ni Siku ya Uhuru wa Habari duniani. Ni siku inayotuhusu sote.
Enzi za Ukomunisti kwenye Soviet Union kulikuwa na magazeti mawili makubwa; Pravda na Izvestia, ikiwa na maana ya Ukweli na Habari.
Na Urusi kulikuwa na utani mitaani; kwamba kwenye Pravda hakukuwa na ukweli wowote ulioandikwa, na kwenye Izvestia hakukuwa na habari!
Na kwa kiasi kikubwa watu wa mitaani hawakutania. Huo ndio ulikuwa ukweli wenyewe. Chama cha Kikomunisti kiliendesha zaidi propaganda. Na tafsiri sahihi ya propaganda ni uongo. Na propaganda maana yake haswa ni uongo unaorudiwa rudiwa sana hadi pale jamii inapoamini kuwa ni ukweli. Kule Soviet Union, kitengo cha propaganda kwenye Chama Cha Kikomunisti kilikuwa na kazi moja kubwa; kusambaza uongo.
Na anayeajiriwa kufanya kazi hapo lazima moja ya sifa zake ziwe ni umahiri wa kusema uongo. Kwamba hata kama kinachoonekana na kila mmoja kuwa ni jiwe, mtu wa propaganda anaweza kusema hilo si jiwe, ni mchanga uliolundikana na kufanya kichuguu. Na atarudia rudia kusema hilo mpaka pale wengine mtakapoanza kuamini kuwa mnaliliona mbele yenu si jiwe ni ' mchanga uliolundikana'!
Na ukweli una sifa moja kubwa, kuwa hata ukifichwa chini ya uvungu wa kitanda kwa miaka hamsini ( Nusu karne) , iko siku, utatoka na kutembea hadharani wenyewe. Hautasubiri kuvalishwa viatu.
Yes, get up stand up!
You can fool some people sometimes. But you can't fool all the people all the time- Bob Marley.
Ndugu zangu, Kuna kisa cha mtego wa panya uliosababisha madhara hata kwa wasio panya. Panya kwenye nyumba aliubaini mtego wa panya uliowekwa uvunguni mwa kitanda na mwenye nyumba. Panya yule akamwendea jogoo wa mwenye nyumba. Akamwambia; " Ewe jogoo, kuna mtego umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane namna ya kuutegua kabla haujatudhuru wote". Jogoo akajibu; " Ondoka zako, mie mtego wa panya unanihusu nini wakati sina kawaida ya kufika uvunguni mwa kitanda!" Panya yule akaenda hadi kwa mbuzi wa mwenye nyumba. Akamwambia; " Ewe mbuzi mwema, unajua kuna mtego wa panya uvunguni mwa kitanda cha mwenye nyumba. Tusaidiane mawazo ya kuutegua kabla haujatudhuru sote". Mbuzi akajibu; " Hivi tangu lini ukaniona nikiingia chumbani kwa mwenye nyumba? Mtego huo wa panya haunihusu mie mbuzi". Panya akaenda hadi kwa ng'ombe wa mwenye nyumba. Akamwambia; " Ewe ng'ombe wa bwana, kuna mtego wa panya umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane mawazo namna ya kuutegua kabla haujatuletea madhara" Ngombe akajibu akionyesha mshangao; " Sijapata kusikia jambo la ajabu kama hilo. Yaani, mie ng'ombe nidhurike na mtego wa panya ulio uvunguni mwa kitanda! Hilo halinihusu." Basi, ikatokea siku moja, nyoka akaingia chumbani kwa mwenye nyumba. Katika kutambaa kwake uvunguni mwa kitanda, mkia wa nyoka ukanasa mtegoni. Kishindo kilisikika. Mwenye nyumba alikwenda kwa furaha akiamini hatimaye panya aliyekuwa akimsumbua sasa amenaswa. Hapana, ni nyoka aliyenaswa mkia. Na ni mwenye hasira pia. Akamng'ata mguu mwenye nyumba. Sumu kali akamwachia. Mwenye nyumba akafa. Jirani wakafika msibani. Siku ya kwanza watu walikuwa wachache. Wakahitaji kitoweo . Akakamatwa jogoo wa mwenye nyumba achinjwe. Siku ya pili watu wakaongezeka. Kilihitajika kitoweo pia. Akakamatwa mbuzi wa mwenye nyumba ili achinjwe. Na siku ya maziko watu wakawa wengi zaidi. Akakamatwa ng'ombe wa mwenye nyumba ili achinjwe. Ni jogoo, mbuzi na ng'ombe wa mwenye nyumba walioamini kuwa madhara ya mtego ule wa panya yasingewahusu wao. Walikosea. Panya alikuwa sahihi, na wala mtego haukumdhuru panya! Naam, Watanzania tunazidi kupokea habari mbaya za matukio ya mauaji ya kutisha. Vuguvugu la mapambano ya kisiasa linasemwa kuwa ni moja ya sababu za matukio ya mauaji na hata watu kujeruhiwa kwa mapanga. Na vuguvugu la mapambano ya kisiasa halipawi kuandamama na vitendo vya mauaji au kujeruhiana kwa mapanga, bali, liwe ni vuguvugu la mapambano ya hoja. Kule Nyamagana tumeshuhudia wabunge wamepigwa mapanga. Na jana kiongozi wa Chadema pale Usa River amechinjwa kama kuku. Inasikitisha sana kuona vitendo hivi vya kinyama vinazidi kuongezeka. Inasikitisha pia kuwa polisi wanashindwa kwa haraka kuwatia nguvuni wahusika wa mauaji na kuwafikisha mahakamani. Labda idara za upelelezi wa kipolisi zinahitaji kuimarishwa zaidi. Na huu ni wakati, kwa Watanzania, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, kidini au rangi, tukemee kwa sauti moja vitendo hivi viovu. Kamwe tusikubali ikawa ni vitu vya kawaida. Ni wakati sasa kwa wananchi wakiongozwa na viongozi waandamizi wa vyama vya siasa. Viongozi wa kidini na wanaharakati wa haki za kibinadamu, kusimama kwa pamoja, na kwa kauli na vitendo, kulaaani maovu haya na mengineyo yenye hata kupelekea roho za wanadamu wenzetu kutoweka. Hakika, kama mtego ule wa panya, tutafanya makosa makubwa kama kuna watakaodhani, kuwa haya ya watu kuchinjwa na kujeruhiwa na mapanga yatawakuta watu wa kundi fulani tu. Tukiacha yaendelee, basi, yeyote yule, bila kujali dini, rangi, itikadi au hata wadhifa wake, anaweza kuwa mhanga wa maovu haya. Kama taifa, kwa pamoja tuwalaani wauaji hawa. Na hilo ni Neno Fupi la Usiku Huu. Maggid Mjengwa, Iringa. 0788 111 765 mjengwablog.com
Ndugu zangu, Katika dunia hii mwanadamu huwezi kumchagua jirani yako. Jirani yako ni jirani yako. Msiba wa jirani ni msiba wako pia, unakuhusu. Maana, kuna wanaohoji JK kuacha mambo ya nyumbani na kwenda kushiriki maziko ya Bingu wa Mutharika. Silioni kosa katika hilo. Na hata kama JK angeamua kutokwenda mazikoni Blantyre, bado, asingekwepa lawama. Maana, kuna ambao wangemlaumu JK kwa kutozingatia mila na desturi zetu Waafrika; kushiriki kwenye kumzika jirani yako. Tukumbuke, kuwa Wamalawi si tu ni jirani zetu, ni ndugu zetu pia. Kuna Wanyasa wengi wa Malawi katika nchi hii waliochanganyika na makabila yetu. Na tunaambiwa, kuwa siku ya mkesha wa Uhuru wa Malawi, Watanzania wengi kando ya Ziwa Nyasa nao walikesha wakishangilia. Uhuru wa Mnyasa ni Uhuru wetu. Msiba wa Mnyasa, ni msiba wetu. Mengineyo... Nchi yetu inapita sasa kwenye kipindi kigumu sana. Tusishushe chini kiwango cha mjadala. Kubaki kumjadili JK na safari kwenda kutuwakilisha mazikoni ni kushusha kwa makusudi kiwango cha mjadala. Kwa makusudi tutakuwa tumeacha kujadili hoja za msingi ikiwamo hii ya kashfa za ufisadi wa kutupwa uliodhihiri bungeni na unaotutaka tuweke shinikizo kwa wahusika kuachia ngazi na hata kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Maana, anayeliibia taifa ni mhalifu tena zaidi ya mwizi wa kuku. Huyu ni jambazi. Kumwacha aendelee kukalia ofisi ya umma ni sawa na kumsusia mlevi bia, au kumpa fisi kazi ya kulinda bucha. Tuliko sasa ni kubaya. Tunakokwenda kutakuwa ni kubaya sana kama hatutachukua hatua sasa. Nimeona asubuhi ya leo kwenye runinga ( Channel Ten) utetezi wa ajabu kutoka kwa Waziri wa Uchukuzi Bw. Omar Nundu. Nundu anadai hawezi kujiuzuru kwa kutoa hoja ambazo kimsingi zinamtaka aachie ngazi haraka iwezekanavyo ili abaki na heshima kwa jamii kama bado anayo. Anatwambia Watanzania kuwa amekuwa 'akizungukwa' na Naibu wake Athuman Mfutakamba. Ndio, Waziri Nundu anapojitetea kwa Watanzania kwa kusema haelewani na Naibu wake na kuwa kampuni ya Kichina ilimpeleka Naibu wake China, Mauritania na Equatorial Guinea bila kibali chake inatosha kuonyesha kiwango cha juu cha ukosefu wa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika baraza la mawaziri . Sioni ni kwa namna gani maelezo ya Nundu yanaweza kumlinda mbali ya kuonyesha ulazima wa kuwajibishwa kwake haraka iwezekanavyo. Ndio huwezi kuonyesha kuwa ulijua kilichokuwa kikifanyika, ukabaki kimya mpaka unatwambia hii leo, halafu utake ridhaa ya umma ikuamini kuendelea kukupa dhamana ya kushika nafasi hiyo hiyo. Na wahenga walisema; kwenye msako wa nyani ngedere hawezi kusalimika. Ndio, tutafanya makosa kudhani kuwa ’madudu’ haya yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya CAG yanahusu Wizara tano au sita tu. Hii ni fursa pekee kwa Watanzania kupitia wabunge wao kuendesha ’ msako mkubwa’ wa wote wenye kulitafuna taifa letu tunalolipenda. Ni wakati pia wa kuhakikisha Katiba Mpya tunayokwenda kuitolea mapendekezo yetu itusaidie kuziba mianya ya wezi wa mali ya umma kuendelea kuliibia taifa bila ya hofu ya kufikishwa mahakamani na hata kutiwa magerezani. Ndio, hatuwezi kuenenda kama tunavyoenenda sasa; maana, unapoona Wananchi wanalalamika, Wabunge wanalalamika, Mawaziri wanalalamika, na Rais analalamika, basi, hilo ni taifa la ajabu sana. Taifa la Walalamikaji. Na maradhi ya ' kulalamika' ni ya kimfumo. Ni mfumo mbovu tu ndio unaoweza kuzaa Taifa la Walalamikaji. Turekebishe mfumo wetu kwa kupitia Katiba. Inawezekana. Maggid Mjengwa, Iringa. 0788 111 765 mjengwablog.com
...Amekuzimia Muda Mrefu! Na nyie kina kaka punguzeni kuchagua, kwa mfano huoni kuwa ni risk kuanza kutaka kufanya mapenzi na msichana mapema hii na kwa yule aliyesema kuwa wengine wanakubali kirahisi, sasa kwa nini umuombe tendo la ndoa? Kwanini usifanye urafiki wa kawaida kwanza bila kufanya mapenzi, mkazoeana mkajuana tabia kama ni wa dizaini ya kutaka mali au wa kujenga, kisha ndio mkaenda stage nyingine? Hivi ngoja leo niwape dillema mnayowatwisha kina dada. Kwa mfano dada wa watu keshakaa wee miaka hatokei mtu wa kumuomba uchumba, mara leo hii umetokea wewe unamtaka urafiki na mara unatanguliza kuomba ngono, hapo anakuwa kwenye dillema, akikukatalia utaingia mitini kimoja na yeye kubaki mpweke. Sasa akupe ngono au abaki mpweke? Na pengine huko nyuma alishakutana na kina kaka maguberi yakataka ngono akakataa ana kaachwa solemba! Sasa hapo afanyeje akukubali umtose vile vile kwa kumuona yu rahisi au akukatalie a risk loneliness! Kisha swali la kizushi, kama mtu umempenda kwa nini umtie hiyo mitihani ya kuanza kumuomba ngono? Ndio kujionyesha Urijali au? Na kwa kuwa umeomba mwenyewe kwa nini ukipewa uanze kuwa na mashaka kama si unafiki ni nini? Sasa ulikuwa unaomba ili ukataliwe? Na msichana akikukubalia haina maana kuwa ni mrahisi bali pengine amekuzimia muda ila ameshindwa kukwambia anasubiri golden chance na hiyo umeileta sasa afanyaje? Cha msingi ni kuwa muwazi na mkweli. Mweleze wazi mwenzako, kusiwe na unafiki, kama kuna mpango wa kuoana basi na muwe marafiki kama ni mpango wa kuchezeana basi na mwambie aanze mbele ili asikuzibie wengine wakafikiri una mtu kumbe huna kitu! Lakini pia ukiwa bold wanaume wengine wanashangaa wanataka wao ndio waanze kutangaza ndoa! Bi Mkora, Msamvu. via Mjengwablog.com
Ndugu zangu,
Leo asubuhi wakati nikifanya ' jogging' kwenye mitaa ya Dar es Salaam niliwasikia watu wa kawaida kabisa wakijiuliza na kujadili; " inakuwaje Serikali iwalipe marehemu mishahara huku sisi tulio hai hatuna hata uhakika wa milo miwili ya siku?" Wanauliza watu wa mitaani.
Naam, nchi yetu imekumbwa na mafuriko ya habari. Kule bungeni Dodoma kuna moto unawaka. Zimeitishwa sanini 70 ili Jumatatu ipigwe kura ya kukosa imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Ndio, kuna wanaotaka Pinda ang'oke, na labda kutolewa kafara, maana, siamini kama tatizo la msingi ni Pinda, bali ni la kimfumo zaidi. Na jana kuna mbunge wa CCM kayasema makali yafuatayo;
“Mheshimiwa Naibu Spika, inashangaza na kusikitisha kuwa nchi inatafunwa. Wanaofanya haya ni mawaziri wetu. Nchi inakufa na tuelewe kuwa Tanzania sio mali ya CCM, ni ya Watanzania wote.“Mawaziri wetu wamekuwa mchwa, wanaangamiza nchi na leo nitamtaja waziri anayeongoza kwa kutafuta fedha za Watanzania. Ni Waziri wetu wa Fedha, Mustafa Mkulo. Ameuza viwanja, amelidanganya Bunge baada ya kuivunja CHC,”- Deo Filikunjombe ( CCM) Bungeni jana.
Lakini ya jana yalitanguliwa na ya juzi; Mbunge mwanadamizi wa CCM Godfrey Zambi aliyasema makali haya;
" CCM inaweza kung'olewa madarakani katika uchaguzi wa mwaka 2015 endapo kasi ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma itaendelea kama ilivyo sasa"- Godfrey Zambi ( CCM, Mbozi Mashariki).
Kauli za wabunge hao wawili wa CCM zinatoa tafsiri ya kilio cha wabunge wa CCM kuomba msaada kwa anayeweza kuwasaidia. Inatoa tafsiri pia kuwa hicho ni kilio cha wabunge wengi wa CCM. Kwamba hayo ndiyo wanayaongea hata chini chini.
Ndio, wananung'unika na wameanza kuiona adhabu wanayokwenda kuipata kutoka kwa wananchi ifikapo 2015. Wanaona pia, kuwa ' kisungura' hiki kidogo kinachopatikana kila mwaka kinavyoliwa na wajanja na wengine kuachiwa mifupa.
Wabunge wa CCM na wengine wanaona jinsi baadhi ya mawaziri wa kutoka chama chao wanavyojiangalia wenyewe kwa kujikatia zaidi kasungura hako kadogo na hata minofu mingine kuikimbizia kwenye majimbo yao badala ya kuangalia majimbo mengine pia. Hakika, Wabunge wa CCM sasa wanatoa kilio cha kuomba msaada na kilichochanganyika na hasira na hofu ya kupoteza mamlaka ya kuongoza dola ifikapo mwaka 2015. Ndio, kuna wanaokiona chama chao kikielekea kwenye kuzama 2015. Kelele wanazopiga bungeni zimegeuka kama kelele za nyikani, hazisikiki. Wameanza sasa kuwa na ujasiri wa kuzomeana wazi wazi kwenye vikao vyao badala ya kusubiri kuzomewa na wananchi hadharani. Naam, CCM ya sasa inapata tabu hata kwenye kujua namna ya kuitumia misamiati mipya ya kisiasa, maana, kuna wanaojivua gamba, wanaovuliwa magamba na sasa kuna ' wanaojinyambua' magamba wakiwa ndani ya chama- 'Political evolution' ya namna fulani.
Zitto Kabwe - Bungeni Aprili 2012 Na Mtego wa Zitto Kabwe kwa CCM?Jana Mbunge Zitto Kabwe ameitega CCM. Ni mtego wa hatari. Saini zile 70 zina maana hii; - Kama wabunge wa CCM hawatachangamkia kutia sahihi zao zikavuka hata mia na hamsini, basi, kuna ujumbe unaopelekwa kwa umma. Kuwa wabunge wa CCM ni maneno tu, hawana dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi. Wabunge wengi wa CCM hawataiepuka adhabu ya umma inaweza kuwa inawasubiri 2015. - Kwa wabunge wa CCM kutia sahihi zao na hata Pinda kupigiwa kura ya wabunge kukosa imani nae ina maana pia kuwa wabunge hawana imani na bwana mkubwa aliyemteua Pinda. Busara haiwataki wabunge wa CCM kufikia hapo. Hilo halina maslahi kwa taifa. Nini kitakachotokea?Kuna matatu; Mosi, Mawaziri wale watano wanaotuhumiwa kwa ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma wanaweza kuepusha aibu kwa Serikali kwa wao wenyewe kutangaza kujiuzulu. Ingawa hili ni gumu kufanyika katika nchi hii, lakini, wakati mwingine kuna lazima ya kufanyika- maana, hapo watakuwa wamemnusuru Waziri Mkuu na aliyemteua. Pili- Likishindikana la kwanza, basi, kabla ya Jumatatu, Waziri Mkuu Pinda awe ameshajiandaa kufanya maamuzi magumu. Kujiuzulu na kulinda heshima yake na ya aliyemteua. Au kutolewe ' Tamko la Serikali' litakalobadili upepo unaovuma sasa bungeni. Tatu: La kwanza na la pili yaweza yasifanyike, na badala yake. Rais anaweza kuyaona yanayotokea sasa bungeni kama fursa ya kufanya mabadiliko makubwa Serikalini mara akitua Dar kutoka ziara ya Brazil. Naam, yumkini pale Diamond Jubilee, kabla ya Jumatatu, kuna watakaopewa kazi ya kusafisha ukumbi na kupanga viti tayari kwa Mkuu wa Nchi kusema jambo kubwa kwa taifa kupitia kwa ' Wazee wa Darisalama'. Na tusubiri tuone. Maggid Mjengwa, 0788 111 765 mjengwablog.com
Ndugu zangu, Sisi wa Kizazi Cha Azimio na wanyuma yetu bado tuna kumbukumbu ya ' Senema za Omo'. Mara moja kwa mwezi ' tabaka la Wafanyakazi' wengi wakiishi Ilala lilikuwa likionyeshwa filamu. Hawa ni wazazi wetu wakati huo. Ilala ni karibu na eneo la viwandani kule Pugu Road. Pale viwanja vya Shule ya Msingi ilikuwa ni moja ya sehemu za wananchi kukusanyika kuangalia senema ya bure. Hakukuwa na televisheni enzi hizo na filamu ya picha zinazotembea kwenye kitaambaa kikubwa cheupe ilikuwa jambo la kuvutia sana. Na kwenye ' Senema za Omo' ndipo tulipokuwa tukionyeshwa matangazo ya biashara pia. Nilikuwa mdogo sana, lakini, moja ya matangazo ninayoyakumbuka sana ni tangazo la Hodorono. Haya ni manukato ya kujipulizia makwapani ama maarufu kwa jina la perfume. Tulionyeshwa abiria anayeingia kwenye basi, na mara abiria mmoja huku akiwa ameshika pua akaanza kutamka kwa sauti; " Hodorono! Hodorono!". Na wengine wakaitikia " Hodorono! Hodorono! Hodorono! Huku wakitokea madirishani. Mwisho kwenye basi akabaki abiria yule aliyeingia. Akaonekana aliyeshangaa asijue kilichowafukuza wenzake. Ujumbe ukawa umefika kwake na jamii, kuwa tutumie Hodorono! Miaka mingi imepita tangu nilione tangazo lile. Katika fikra zangu hizi za ukubwani, tangazo lile si kingine bali ni tangazo la kibaguzi na ambalo halikufaa kuonyeshwa katika jamii. Na siasa zetu za siku hizi nazo zimekuwa za staili ya Hodorono. Ni siasa za kibaguzi unausukumwa na ubinafsi. Tunaona vijana wa leo wameanza kuukataa kwa vitendo ubaguzi huu wa kisiasa. Ni jambo jema. Huko nyuma TANU na baadae CCM viliamini kuwa asiyefikiri kama wao basi si mwenzao. Ni mpinzani, ni adui wa maendeleo. Ni adui wa umma. Ni msaliti. Si mwenzao na alibaguliwa. Alitengwa na pengine kuishia kifungo cha ndani au cha nje kwa kurudishwa kijijini alikozaliwa au asikozaliwa. Huko Mtanzania huyo aliyebaguliwa kisiasa alifikia kuambiwa kuwa kila siku awe anaripoti kwa Balozi wa Nyumba Kumi. Na kutoka kijijini kwake kwenda kijiji kingine ni sharti aombe ruhusa ya uongozi wa kijiji! Na kutoka nje ya wilaya ni sharti apate kibali cha DC! Hii nayo ni historia yetu. Ili tuelewe tulipo na tunakokwenda tuna lazima ya kuipitia historia yetu. Ubaguzi wa kisiasa ni jambo baya sana. Kwamba kuna wanaojiona wao wana haki zaidi kuliko wenzao katika nchi hiyo hiyo ambayo wenzao pia wanaiiita nchi waliyozaliwa. Kwamba wana uwezo wa kuwafanya Watanzania wenzao waishi maisha magumu kwa vile tu wanatofautiana au wanapingana kifikra na walio kwenye mamlaka ya dola au Chama kilicho madarakani. Ubaguzi wa kisiasa huzaa chuki ya kisiasa. Na mara zote, uvumilivu wa wanaobaguliwa na kukandamizwa hufikia kikomo. Na yanapolipuka, basi, huwa kama nusu ya kiyama. Moto huwaka. Hakukaliki. Kule Misri vijana wengi wanajua sasa ni kwanini wazazi wao walihangaika sana kutafuta ajira lakini hawakupata na kuishia kuishi maisha magumu. Wanajua sasa ni kwanini baadhi yao ( Vijana) hawakupata scholarship au ajira baada ya kufuzu masomo yao. Wanajua sasa, kuwa Idara ya Usalama wa Taifa chini ya Hosni Mubarak, familia yake na jamaa zake wa karibu walikuwa na faili maalumu yenye orodha ya majina ya WaMisri, vijana kwa watu wazima, ambao walionekana kuwa ni wenye fikra za kipinzani. Kuna waliochunguzwa tangu wakiwa kwenye mijadala ya vyuo vikuu. Na ambaye jina lake limeingizwa kwenye faili hilo, basi, ataandika kurasa kwa maelfu za barua za maombi ya kazi, na atasaga lami sana hadi soli za viatu ziishe akitafuta ajira bila mafanikio. Serikali ya Hosni Mubarak ilikuwa na mikono mirefu, na miguu pia. Tatizo lilikuwa kwenye 'kichwa cha Serikali'. Kilikuwa kidogo sana, maana hatma ya yaliyomfika Hosni Mubarak ingepaswa kuepukwa na mtu mwenye kichwa kinachofikiri. Kwa vile kilichotokea kingetokea, ilikuwa ni suala la wakati tu. Ndio, Usalama wa Taifa ( Zaidi Usalama wa Hosni Mubarak na Chama chake) ulihakikisha Mmisri ambaye jina lake limo kwenye kitabu chao hapati kazi yeyote ile labda iwe ya kubeba zege ili hali ana digrii ya chuo Kikuu. Nimefurahi sana hii leo kuwasilimulia juu ya tangazo la Hodorono kwenye enzi za utoto wangu. Hakika, ni tangazo la kibaguzi. Na siasa zetu siku hizi zimekuwa za Ki-Hodorono. Ni siasa za kibaguzi. Tunajenga nyumba moja, lakini tunagombania fito. Ni hulka za ubinafsi. Kama nchi , siasa za hodorono zitatupelekea si tu kuvuja jasho na makwapa kunuka, bali kuvuja damu kwa kukatana mapanga. Kwa viongozi tuliowapa dhamana kutotanguliza busara na hekima. Na hilo ni Neno La Leo. Maggid Mjengwa, Dar es Salaam. 0788 111 765 mjengwablog.com
Ndugu zangu, Shujaa wa taifa la India Mahatma Ghandi alipata kutamka; " Bila ya ng'ombe India isingekuwepo". Mwingine angefikiri, Wahindi hawa ni watu wa ajabu sana. Iweje watoto wao wengi wafe kwa njaa kila kukicha huku wakiwaacha ng'ombe takribani milioni 200 wakizurura ovyo mitaani pasipo kuwachinja? Katika hilo tusiwahukumu Wahindi kabla ya kujaribu kuwaelewa. Wahindi hawa wapatao milioni 800 hawawezi kuwa wendawazimu kwa kukubali kuwaacha ng'ombe wao bila kuwachinja. Kuna busara kubwa ya Wahindi kumfanya ng'ombe kuwa "mtakatifu". Sababu kubwa na ya kimsingi ni ya kiuchumi. Karibu asilimia 70 ya Wahindi wanaishi mashambani, ni wakulima. India hukumbwa na mvua kubwa zenye kuambatana na upepo wa monsuni. Kutokana na mvua hizi, mkulima wa India anaweza kulazimika kulima shamba zima kwa siku moja na pengine kuvuna shamba zima kwa siku moja. Hali hii ya hewa hulazimisha kuwepo na uharaka katika utendaji kazi. India haina uwezo wa kutoa matrekta ya kutosha ya kulima na kuvuna kwa idadi hii kubwa ya wakulima wa nchi yao. Hapa ng'ombe anaweza kutumiwa kufanya kazi hii ya haraka. Ng’ombe atavuta jembe la plau, atasaidia katika kuvuna, na hata kusafirisha mazao. Ng'ombe husaidia pia katika kutoa nishati mbadala. Pamoja na ng'ombe kuzurura barabarani, ni nadra sana nchini India, kukutana na vinyesi vya ng'ombe vilivyotapakaa. Kinyesi cha ng'ombe huchukukuliwa kikiwa kibichi, hukaushwa na kufanywa kuwa nishati. Kuna majiko yenye kutumia moto wa kinyesi cha ng'ombe. Kinyesi hutumika pia kama mbolea ya shambani. Fikiri, India ingekuwaje kama Wahindi hawa milioni 800 wangetegemea nishati ya kuni za miti? Kimsingi kinachofanya uchumi wa India ukue kwa haraka ni mioyo ya uzalendo na utaifa wao. Kuna wakati, Rais George Bush alipotembelea India , alipokewa na kuendeshwa kwenye gari iliyotengenezwa India. Msafara wake ulikuwa ni wa magari yaliyotengezwa India. Magari kama Bajaj, Maruti, TATA na mengineyo. Yote haya ni fahari ya India. Ndio, Wahindi wanajivunia India yao na kila kinachotengenezwa kwao. India ni taifa kubwa. wana programu za nyuklia ingawa ili linahitaji mjadala, wana viwanda vya madawa, hospitali zenye ubora, viwanda vya nguo na mengineyo mengi. Kwa miaka mingi, wenzetu hawa wamewekeza katika elimu ya watu wao na kwa lugha yao. Wameanza sasa kuvuna walichopanda. Kwetu sisi Watanzania, hali yetu ya kiuchumi bado duni mno. Ufisadi unalitafuna taifa letu. Tuna lazima ya kukumbushana ukweli huu. Na ili kuunusuru uchumi wetu usiyumbe zaidi, tuna lazima ya kutumia fedha na rasilimali zetu kwa busara kubwa. Ilivyo sasa kuna mengine tunayoiga yenye kututia hasara zaidi. Mathalan, anasa za viongozi wetu wakiwemo wabunge , kuanzia kwenye magari hata safari zao za nje. Wananchi wakiuliza, wanajibiwa; angalieni wabunge wa Afrika Kusini! Wahenga walinena; Usimuige tembo kwa lolote lile. Mengine afanyayo tembo yanatokana na ukumbwa wa maumbile yake. Na hilo ni Neno la Leo. Maggid Mjengwa, Iringa 0788 111 765 mjengwablog.com
|