Kama kuna jambo linalowaumiza vichwa watanznia basi ni swali kuwa kwanini kila wanalopanga halifanikiwi? au kwanini wananchi ni masikini licha ya maliasili zilizojaa kila kona yanchi hii? Wakiangalia elimu hoi watoto wanafeli, wakija kwenye afya hakuna kitu, wakienda kwenye kilimo na hata umeme tabu tu kwa kifupi hakuna jipya ni uduni na ubabaishaji mtupu. Katika lindi la mawazo ya namna hii au maswali mengi yasiyojibika tunawatazama viongozi wetu na uwajibikaji wao usiokidhi viwango kiasi kwamba wamepwaya mno , wajuzi wa kuzungumza bila kutenda, ni watu wa blah blah na porojo tu. Kwakweli Tanzania imetawaliwa na wapiga porojo hebu angalia kwenye hiyo kaulimbiu ya “kilimo kwanza”inavyotangazwa na kupigiwa chapuo na viongozi wetu kasha nenda huko vijijini kwenye mashamba utaona hata mabwana shamba hakuna na hizo pembejeo zenyewe za kilimo hakuna, sasa utasema hapo kuna kilimo kwanza au porojo tu? Geukia elimu nddio utashangaa kabisa kulivyooza huko lakini cha ajabu ni kuwa viongozi wetu bado wna ujasiri wa kusimama kwenye majukwaa na kudai kuwa serikali imeboresha elimu, elimu gani? Shule za kata? Si ndio hizi zinatoa sifuri? Nasikia siku hizi zinaitwa mtambo wa sifuri, ajabu sana! Yaani serikali inajenga majengo tupu bila walimu,madawati wala maabara kasha wanaita sekondari halafu wanazidi kuboronga wanafuta mitihani, tuziiteje hizi? Hizi ni porojo za watawala wetu, porojo porojo kila mtu anapiga porojo tu. Njoo kwenye hizo huduma za afya , tunaambiwa kuwa Tanzania bila maralia inawezekana tena kwa mbwembwe kwa matamasha makubwa lakini hivi mtu wa kule kijijini analala chini hana hata hiko kitanda je hiyo neti atachomeka wapi? Au motto wa mtaani analala kwenye vichochoro huyu neti atachomeka wapi? Sasa hizo Zahanati za vijijini kama kweli zinaviwango mbona vifo vya akina mama wajawazito bado vinaendelea? Hakika hizi ni porojo za viongozi wetu! Halafu anaibuka kiongozi mkubwa wa nchi anadai msongamano wa magari jijini Dar es salaam ni ushahidi wa kukua kwa uchumi wetu, hizi sasa porojo, uchumi wetu na nani? Mafisadi? Au Brigedia Al Adawy na Dowans? Uchumi umekua na ombaomba wameongozeka ndiyo magari yameongezeka na umasikini umekithiri , sasa huo uchumi uliokua umemnufaisha nani? Mawaziri na wabunge? Au rais na waziri mkuu? Hizi ni porojo tupu. Serikali nayo imeshindwa kuweka huduma za nishati ya umeme wa uhakika, sasa naona ina mchoko naam! Huu ni mchoko ndio maana kila kwenye hotuba tunapigwa kalenda mpaka mwaka huu au ule tatizo la umeme litakuwa historia halafu mda huohuo umeme ni wa mgao, waziri wa nishati nay eye hana jipya bado watu tunateseka kwa sababu ya kukosa ubunifu na uzalendo , mwenyekiti wa kamati ya bunge ya nishati anataka tuwashe mitambo ya Dowans, watu wanahoji anataka turudi tulipotoka? Hizi kama sio porojo nini basi? Nchi ipo gizani viongozi wanapiga porojo inasikitisha sana. Tabia ya kupiga porojo inaendelea kudidimiza nchi , hata kwenye michezo tunapiga porojo halafu tunataka kucheza kombe la Dunia,bungeni kuna porojo kiasi kwamba bunge linafanywa sehemu ya kupigana vijembe na mipasho halafu na sisi tunaamini iko siku tutakuwa kama wenzetu wa Ulaya na Marekani ambao tayari wamefuta blah blah na porojo kwenye kamusi za vichwa vyao wanafanya mambo kizalendo na kwa kujituma, haiwezekani ! Matokeo ya porojo yanapoonekana viongozi wetu hawachelewi kusikitika na kuhidi kujirekebisha, ona matokeo ya kidato cha nne yalivyowaumbua viongozi sasa wanajifanya wamejifunza hakuna kitu porojo tu , mabasi yanakimbia yanavyotaka wenye jukumu la kulinda usalama barabarani wanapiga porojo watu wanakufa utadhani ni msimu wa ajali. Siku hizi hadi viongozi wa dini wamekumbwa na tabia ya kupiga porojo , badala ya kutetea wanyonge wao wanagombana wenyewe kwa wenyewe, wengine wanaenda mbali zaidi kwa kujigeuza miungu watu wanadanganya masikini na kuwakamua hata kidogo walichonacho na wengine wamejigeuza watabiri wanatabiria watu kufa? Hizi ni porojo tupu. Sasa katika muktadha huu ndio maana najiuliza kuwa nchi hii iliyolewa kwa wingi wa porojo itaendelea vipi? Badala ya kwenda mbele sisi tunarudi nyuma kwasababu ya porojo zisizokwisha na hazina mipaka hata kwenye mambo ya msingi tunapiga porojo au ndio tunategemea kuendelea kwa miujiza ya Mussa? Tafakari! Imeandikwa na: Nova Kambota Mwanaharakati, 0717 709618 au +255717 709618 novakambota@gmail.com www.novakambota.com Tanzania, East Africa, June 30, 2011 Naomba kura yako kwenye category ya Best collaboration/group blog, Best Informative political blog, Best political blog kwenye tuzo za blog Tanzania, kunipigia tembelea www.tanzanianblogawards.com 1 Comment Hakuna ubishi kuwa jamii yetu ya kitanzania inazidi kuwa ya kipuuzi kadri siku zinavyokwenda na kundi linaloonyesha kuzidiwa nguvu na ujinga ni kundi la vijana huku ujinga wao wakiubatiza jina la “mambo ya kisasa” lakini ukitazama kiundani unabaini kuwa ni ulimbukeni wa kupenda tamaduni za kimagharibi na pengine uzuzu wao na mdumao wa ubongo ikiwa ni matokeo ya kutopenda kufikiri. Nimelazimika kutumia maneno makali sana leo kutokana na jambo ninalotaka kulizungumzia hii leo kuwa ni zito sana na hili si lingine bali ni kitendo cha mtanzania mwenzetu mwanadada Bhoke kufanya ngono na mshiriki mwenzake Ernest huko nchini Afrika kusini katika jumba la Big Brother Africa, naam! ni kitendo kilichovuta hisia za watanzania wengi walio ndani ya nchi na walio nje ya nchi, nataka kumshauri Bhoke kama kijana mwenzangu tena hadharani ukizingatia kitendo chake hiko kimeonekana hadharani na zaidi ya yote nataka kumwambia ukweli pasipo kupindisha neno kwa kiwango ambacho na uhakika marafiki zake hawawezi kumwambia kwa kumwonea aibu, mimi nitamwambia leo pasipo kumung’unya maneno. Baada ya kurejea nyumbani Bhoke amenukuliwa akisema kuwa hakutumwa na watanzania Afrika kusini bali alienda mwenyewe , ingawaje mara ya kwanza nilivyosikia upuuzi huu nilidhani ni maswala ya kuuza gazeti tu lakini kutokana na kusubiri kuona iwapo Bhoke mwenyewe atakanusha na hakufanya hivyo basi hakuna ubishi kuwa Bhoke amesema upuuzi huu ambao bilashaka badala ya kumjenga unazidi kumharibia yeye na mabinti wengine lakini mbaya zaidi unazidi kuwachafua vijana wa taifa hili, naam! Bhoke amefanya upuuzi na sasa ameongea ujinga. Kwanza kabisa Bhoke hana sababu ya msingi ya kujitetea kutokana na kitendo cha aibu alichokifanya, ikumbukwe kuwa alipokuwa Afrika kusini Bhoke alitambulika kuwa anatoka Tanzania na tangu akipanda ndege kuelekea huko hakuna ubishi kuwa alikwenda kuwakilisha nchi yetu kwenye tasnia ya burudani kama wafanyavyo wasanii na wanamichezo wengine hivyo kauli yake kuwa hakutumwa na watanzania haina mashiko na zaidi ni ya kitoto kuliko uhalisia, labda nimwulize Bhoke swali moja tu rahisi, je kwanini Richard aliposhinda alipokelewa kama shujaa? Au kwanini Mwisho naye alipongezwa na watanzania? Au basi iwapo yeye Bhoke angeshinda je angekataa kupokelewa na kupongezwa na watanzania? Kwasababu hawakumtuma? Natoa changamoto kwa Bhoke ajifunze kuongea mambo yenye mantiki sio kutujia na vijisababu vya kitoto ambavyo havijai hata kwenye kiganja. Hivi Bhoke anataka kutuambia kuwa yeye yuko sahihi? Na sisi tunaolaani kitendo chake ni washamba? Au tuna mambo ya kizamani? Au basi nani kamwambia Bhoke usasa ni kujidhalilisha na kutuvua nguo watanzania kama alivyotufanya? Nani kamwambia Bhoke kuwa kufanya ngono hadharani ni jambo linalokubalika kwa mila zetu? Mbona Bhoke anataka kutuchezea akili kwa kutetea ujinga? Tena mchana kweupe! Bhoke anapaswa kutambua kuwa watanzania sio watumwa wa mila za kishenzi za kufanya ngono hadharani za watu wa magharibi? Uzito wa jambo alilolifanya Bhoke hauwezi kuelezewa kwa misamiati wala methali , hata tujitahidi kuupaka mafuta kwa kiasi gani bado utabaki ni utumbo wa aina yake kwa mwaka huu wa 2011 na pia itabaki katika kumbukumbu za watanzania kama aibu kubwa huu ndiyo ukweli ambao naona Bhoke anataka kuupindisha kwa hoja nyepesi mno tena zilizopwaya sana za “sikutumwa na watanzania”. Chukulia mfano video ya Bhoke ya huko Afrika kusini niliulizwa na rafiki yangu aishiye nchini Finland kuwa nimeshaiona? Mimi kwa kuona aibu nikaficha na kusema hapana sijaiona, rafiki yangu hakuchukua muda akanitumia, hiki ndicho alichotufanya Bhoke duniani kote sasa wanamtambua kwa aibu yake hiyo! Watanzania ni watu tuliokuzwa katika utu ikiwa ni pamoja na kuvumiliana na kusameheana ila ni kwa wale waliotayari kukiri makosa yao , kujutia na kuomba msamaha sasa tulitegemea Bhoke ajutie kosa lake na kuomba msamaha kwa watanzania lakini sasa yeye anataka kutupanda kichwani huku akijua wazi kuwa ametuaibisha, hili halikubaliki hata kidogo ni lazima tumkemee vikali tena kwa maneno makali pasipo huruma, baada ya kujidhalilisha yeye na kutuaibisha watanzania sasa Bhoke anataka kutudhihaki? Hili halikubaliki kabisa! Ikumbukwe kuwa Bhoke sio binti tu wa kitanzania bali ni msichana wa kitanzania aliyejijengea heshima kubwa kutokana na harakati zake kuhusu vijana kupitia kipindi cha 5 connect katika kituo cha EATV si hivyo tu kuna baadhi ya mabinti wadogo walikuwa wakimwona Bhoke akiendesha kipindi hiko walijisemeza moyoni kuwa na wao siku moja wangetamani kuwa kama Bhoke naam! Bhoke alikuwa msichana wa kupigiwa mfano miongoni mwa wasichana wenzake na vijana wa kitanzania kwa ujumla. Bhoke nayemjua mimi sio Bhoke huyu anayejibu upuuzi wa kitoto wa “sikutumwa na watanzania” mimi namfahamu Bhoke jasiri ambaye ni aina ya mabinti ambao hata ukienda naye hotelini hataki ofa za bure bali wewe utalipa nusu nayeye atalipa nusu, huyu ndiye Bhoke nayemfahamu mimi ambaye kila jumatano nilikuwa naacha shughuli zangu kumwangalia naam! ni Bhoke niliyetamani siku moja nimhoji au nifanye naye kipindi. Lakini sasa Bhoke anazidi kujibomoa kwenye mioyo ya watanzania, Bhoke anajaribu kutikisa kiberiti afahamu hasira za watanzania, Bhoke anafanya mzaha na mila zetu na hisia zetu. Namtaka Bhoke afikirie tena juu ya kosa lake na matamshi yake nayoyaita ni ya kipuuzi kabisa“sikutumwa na watanzania” natoa changamoto kwa Bhoke ajaribu kuomba ushauri kwa viongozi wake wa dini juu ya kitendo chake na kisha ajipange kwa hoja zenye mashiko na zitakazopooza hasira za watanzania , aachane na porojo za kitoto kama ambazo ameanza kuzitetea badala yake namtaka Bhoke akumbuke yeye ni nani? thamani yake ni nini? na amefanya nini? naam! natoa wito kwa dada yangu Bhoke alitazame kosa lake kwa jicho la tatu na akili ya kiutu uzima……….Tafakari! Alluta continua! Nova Kambota Mwanaharakati, june 23, 2011,Tanzania East Africa 0717 709618 au +255717 709618 novakambota@gmail.com www.novakambota.com Wanafunzi mtoni - hatari: Magonjwa, kuzama! 18/06/2011
Kuwapa walimu "posho"? Nimehesabu ni faulo! 16/06/2011
Juzi nilisoma habari iliyochapishwa kwenye blogu kuhusu Mbunge kuwapa Walimu fedha, kwa jina la "posho". Ingawaje sikupata muda wa kuandika yatokanayo na taarifa hiyo, bado hainizuii kuandika leo niliyowaza. Mazingira na sababu za ziada hasa za kutoa fedha hizo kwa Walimu sina undani wake, hivyo ninatoa mtizamo huu kulingana na kile kilichoripotiwa katika habari hiyo. Nakiri kuwa kuwapa Walimu "posho" ya aina yoyote si kero kwangu, sina "wivu" walimu kupewa "posho" bali, napenda kuona "posho" hizo zinatolewa kwa kufuata utaratibu uliokubalika Kitaifa na usiyoleta manung'uniko kwa waajiriwa wengine, wala kuwapa shinikizo wawakilishi na waajiri wa maeneo mengine kutakiwa kufanya hivyo katika maeneo yao ya uwakilishi/kazi. Mosi, nilipoisoma tu nilisema moyoni, "how cheap"! Kwamba ni udhalilishwaji. Nilisikitika sana kuona Walimu wanapewa shilingi elfu hamsini "kama posho" yao il hali huu si utaratibu wa Serikali. Nikajiuliza, ili kutoa posho, si lazima iwepo sheria au kanuni za Kiserikali zinazoruhusu kufanya hivyo, la sivyo, hii ni sawa na rushwa? Pengine sifahamu sheria hizo, nitafurahi kuelimishwa katika hilo. Pili, nilihesabu hii sawa na rushwa ingawaje wengine huiita kwa jina lisilo na makali, "takrima", kuwashukuru wananchi kwa uchaguzi uliokwisha tangu Oktoba 2010. Naifananisha na rushwa kwa kuwa imetoka kwa Mtu binafsi kwenda kwa wafanyakazi wa serikali, na mtu huyo pia anaweza kutumia cheo cha Ubunge, nayo pia naiona ni rushwa hata ikiwa tayari miezi kadhaa ya uchaguzi imepita na ipo mingi mbeleni kwa uchauguzi ujao. Kumbukumbu hii ya kutoa fedha inatosha kabisa kurejelewa wakati wa uchaguzi ujao kuomba "kuzikumbuka fadhila" hizi kwa wakati huo. Tatu, nimeona kama ufalme unaopingana ndani yake wenyewe. Nasema hivi kwa kuangazia kurunzi la siasa za vyama. Kwamba aliyefanya hivi ni Mbunge anayetokana na chama ambacho ndicho kimeshika hatamu ya uongozi wa Serikali ya nchi nzima. Kwamba, ikiwa yanafanyika haya kwa jina la kuisifu Serikali kupitia Chama fulani, je, ikiwa utaratibu huu si wa Kiserikali, hilo si kinyume na sheria/taratibu? Ikiwa ni ndani ya utaratibu wa Chama na Serikali, je, majimbo mengine na maeneo ya uwakilishi Wabunge wao wameshafanya hivi au wameweka kibodoni fedha za watu? Na, ikiwa wamepewa posho walimu, je, makundi mengine ya wafanyakazi hayastahili kupewa posho nao? Au kipimo cha kupewa posho hasa ni kipi? Kuwa na mshahara mdogo au kufanya kazi fulani? Na kama hivo viwili ni sehemu ya vigezo vya kiwango na aina gani ya posho itolewe, basi kutoa posho haitasaidia, badala yake, vigezo hivyo viwili inabidi kurejelewa ili kuona ni kwa vipi kundi hilo litajiweza bila kupewa posho. Nne, tujiulize, ikiwa jambo hili lingefanywa na chama chochote chenye upinzani wa kisiasa Tanzania, lingetafsiriwaje? Sikatai kuwa vipo vyama pinzani ambavyo vimefanya mambo fulani kwenye majimbo yake, mathalan wapo waliotoa magari kwa ajili ya "ambulance" au "madawati" au "pikipiki" n.k., ambavyo vyote hivyo vimetolewa kwa manufaa ya Wananchi wote na siyo kwa watu wachache au kikundi fulani katika jimbo/eneo la uwakilishi. Mwishowe, najiuliza, je, huu ni mpango endelevu au ni tukio la kustukiza mara moja moja? Nihitimishe, kwamba, kama ambavyo ilipigiwa kelele ya kupinga kitendo cha baadhi ya Wabunge kuchangia nauli, kutoa vyombo vya usafiri na kuwawezesha wananchi wao kwenda Samunge "kwa Babu kupata kikombe", hata ikiwa msaada ulifanyika kwa wananchi wote bila kujali itikadi za vyama, tukahoji utaratibu huu unatuma ujumbe gani kwa watu wa maeneo mengine ambapo wabunge/wawakilishi wao hawana uwezo wa kifedha kuwasaidia wananchi wao wafike Samunge; Vivyo hivyo tuhoji, Je, kuwapa kundi fulani la watu "posho" badala ya kundi matokeo yake kwa jamii nzima ni yapi? Rubuni isitutege na kututenga. Silioni kosa katika utoaji fedha na shukrani/takrima, bali natilia shaka kwenye utaratibu unaotumika. Binafsi nimehesabu hili sawa na udhalilishaji kwa Walimu (ama kundi lolote la waajiriwa/wafanyakazi), utumiaji usio sahihi wa cheo na kitendo cha rushwa aidha kwa kutokujua au kwa kupuuziwa madhara yake na kubeba sifa za matokeo ya kilichofanyika. Ingawaje mimi sijawahi kusoma maswala unajimu wala utabiri naomba leo nitabiri mambo matatu kuhusu maisha ya waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond Bw Edward Ngoyai Lowassa, kwanza nashawishika kuwa Lowassa ametoka familia ya kichifu au wazazi wake walikuwa matajiri, pili Lowassa ni msiri sana na tatu Lowassa anaishi kwa ahadi kuliko nyakati. Kwa kawaida watoto wa kichifu au wa familia za kitajiri ni waoga tena wapo tayari hata kutoa fedha mradi wasikumbwe na dhoruba hata kwenye shule za bweni watoto wa kitajiri ni waoga kwelikweli, kwa jinsi Lowassa asivyopenda matatizo “ajali kazini” hapendi “kupambana jino kwa jino” yaelekea ni tatizo la kimalezi kuliko kisiasa, malezi ya Lowassa aliyolelewa katika familia yake ambayo ni ya kitajiri yamemfanya kuwa mwoga sasa amebaki kulalamika kuwa “anaonewa”. Chukulia sakata la Richmond ambalo lilimwondoa Lowassa kwenye kiti cha uwaziri mkuu, kamati ya bunge iliyoongozwa na Mwakyembe ilileta ushahidi mzito dhidi yake kwa kushindwa kusimamia mawaziri wake vizuri na Lowassa alipotoa ile hotuba yake ya …”nimetafakari sana , nimedhalilishwa sana, nimeonewa sana kwa heshima ya chama changu…………………akaingizia na tuhuma kuwa kamati ya Mwakyembe imelidanganya bunge na akazidi kuongeza utata kwa madai kuwa tatizo ni uwaziri mkuu lakini yote haya yamebaki siri kubwa hayuko tayari kusema kinagaubaga na kutwambia kuwa tatizo lilikuwa uwaziri mkuu au kweli kamati ilidanganya bunge. Halafu yaelekea Lowassa ni mtu anayeishi kwa ahadi kuliko kusoma alama za nyakati , tangu mwaka 1995 iliwahi kuelezwa kuwa Kikwete na Lowassa ni maswahiba wakubwa tena ikaelezwa kuwa iwapo mmoja wapo ataukwaa urais basi mwingine angeteuliwa kuwa waziri mkuu na hili halikupita kwani kufuatia ushindi wa “sunami” wa kikwete wa mwaka 2005 Lowassa akateuliwa kuwa waziri mkuu tena nakumbuka ile hotuba ya Kikwete siku ya uteuzi wake mara baada ya bunge kupitisha jina lake “mtaani watu wanasema ooh Lowassa ni rafiki yangu ni kweli rafiki yangu ila namfahamu Lowassa ni mtendaji mahiri asiyetetereka” haya yalikuwa ni maneno yake Kikwete sasa yaelekea kuwa si hivyo tu bali pia Lowassa aliahidiwa ndiye atakayekuwa mrithi wa Kikwete 2015 lakini licha ya yote yaliyomkuta naona bado kalala kwenye usingizi wa “fofofo” anategemea ahadi badala ya kuenenda kadri ya alama za nyakati zinavyomtaka. Kama mwandishi mahiri wa habari za uchambuzi nchini maarufu kwa jina la Mwanakijiji alivyomshauri Lowassa kupitia makala yake iliyokuwa na kichwa cha “Edward Lowassa uchaguzi ni wako” , katika makala yake hiyo Mwanakijiji anamtaka Lowassa kurudi kwenye ulingo wa siasa za kitaifa na mimi narudia tena kufanya siasa za chinichini kama anavyofanya Lowassa hivi sasa haimjengi chochote bali inabidi arudi rasmi kwenye ulingo wa siasa za kitaifa tena atolee matamko mambo mazito bila woga, nashindwa kuelewa Lowassa anaogopa nini? kwa maana ushahidi wa nguvu na ushawishi wake unaonekana waziwazi mfano licha ya yeye kujiuzulu sambamba na Msabaha na Karamagi hawa wenzake wote “tupa kule” hawasikiki tena ila yeye bado anasikika kwenye vyombo vya habari (japo si kwa mema). Bado hatujasahau vuta nikuvute kati ya Mwakyembe na Lowassa kiasi kwamba Mwakyembe aliwahi kuwapa changamoto kina Lowassa ili kupima iwapo wanakubalika kweli basi yeye na wao waende kuhutubia pale sokoni kariakoo kisha waone wananchi watafanyeje? Kama kweli Lowassa anajiamini tulitegemea ajitutumue hata kujibu au kufanya chochote kuonyesha kuwa anakubalika lakini wapi! Lowassa alikaa kimya hii maana yake nini? na inatafsiri gani? nini hitimisho la mvutano huu wa Mwakyembe na Lowassa? Mvutano kati ya Samwel Sitta na Lowassa ulizua ya kuandikwa, kuna baadhi ya watu wakadai kuwa Lowassa aliposema kuwa …”tatizo ni uwaziri mkuu..” alikuwa akimaanisha mvutano wake na Sitta na hili likapewa uzito na kauli za Andrew Chenge “swahiba wa Lowassa” kuwa Sitta alitumia bunge kujeruhi wenzake kisiasa lakini licha ya yote haya Lowassa hakutia neno yeye kaka kimya, watu wanapotaka kufahamu uwaziri mkuu wake ulikuwa na uhusiano gani na Sitta? yeye “anajibu kisiasa badala ya kujibu ukweli” kuna nini hapa? Anamwogopa nani? CHADEMA katika moja ya mapambano yao dhidi ya ufisadi waliwahi kumhusisha Kikwete na ufisadi tena baadhi ya magazeti yakadai kuwa iweje waziri mkuu Lowassa ahusike na Richmond kisha Kikwete ambaye kimsingi ndiye bosi wa waziri mkuu asihusike? Haya ni maswali ya msingi ambayo Lowassa hakupaswa kukaa kimya alitakiwa atwambie iwapo Kikwete alihusika au la? Na sio kutwambia tu bali aseme kwa nukta na mantiki kiasi tukipima maneno yake tuone yana ukweli na yamejengwa kwa mtiririko wa “logic”. Sasa kuna operation ya kujivua gamba ambayo ilielezwa kuwa mmoja wa walengwa alikuwa ni Edward Lowassa lakini sasa operation hii imekuwa butu kwa maana nyingine imeshindwa na watu wanamlaumu Kikwete kwa kushindwa kuisimamia, wengine wanahoji ingekuwaje kama angeisimamia? Lowassa angeathirika kwa kiwango gani? na je kwa kutoisimamia Lowassa kanufaika kwa kiwango gani? na je Kikwete anamwogopa Lowassa? Au Lowassa bado ni swahiba wa Kikwete? Haya ni maswali ya msingi na hakuna mtu mwingine wa kuyajibu zaidi ya Lowassa hapaswi kukaa kimya. Lowassa anapaswa kuingia kwenye siasa za malumbano na minyukano bila kusita hata ikibidi kumjeruhi “swahiba” wake Kikwete potelea mbali ajali kazini hata ikibidi kulipua msuguano tena baina yake na Sitta na Mwakyembe sawa tu lakini ukweli pekee ndiyo utakaomweka huru Lowassa vinginevyo anajimaliza kisiasa kiasi kwamba hata kwenye historia ya taifa hili hatokumbukwa tena. Lowassa asiishie kusema pembeni kuwa yeye ni msafi anaonewa tu inabidi adhihirishe kauli yake kwa kuwataja wachafu pasipo kusita vinginevyo yeye ndiyo mchafu na anawasingizia wenzake kwa kusema wanamwonea. Lowassa inabidi ajiamini kwani yeye si ndo alikuwa injinia mkuu wa mtandao uliomwingiza Kikwete 2005 kwa maana nyingine maadui Lowassa aliwapata wakati akimtetea Kikwete sasa anaogopa nini? kwa maana nyingine maadui wake pia ni maadui wa Kikwete hivyo asiogope sana! Kwa maana nani ana nguvu za kumshinda kiongozi wa nchi? Na kwa upande mwingine Kikwete na chama chake anachokiongoza CCM wanapaswa kuweka hadharani uchafu wa Lowassa kuliko kuendelea na minong’ono, mzee Chiligati, Nape Nauye na Mukama wamkane waziwazi Lowassa na Kikwete avunje urafiki na Lowassa iwapo kweli anaamini Lowassa ni “mchafu tena anamharibia kwa wananchi”. Tunataka Mwakyembe, Sitta, Chenge na Rostam waseme ukweli kuliko kumung’unya maneno, tunataka ukweli “kindakindaki” Tumechoshwa na siasa za mipasho na vijembe , hatutaki kusikia upuuzi wa “hao mafisadi” tunataka tuambiwe fulani na fulani ni mafisadi, hatutaki kusikia “mimi ni msafi” bali sina kosa kwasababu moja mbili tatu, hatutaki upuuzi wa “ni lazima CCM ijivue gamba” bali tunataka kusikia “fulani na fulani wamekiuka kanuni za chama sasa tunawatimua na kuwafilisi mali zao” , haya ndiyo matakwa ya watanzania. Mtu pekee ambaye anaweza kutufikisha huko ni Lowassa , Lowassa ni lazima azungumze yeye ni “kichocheo” katika hili, aseme neno moja tu ! na alisimamie pasipo uwoga “UKWELI” huu ndiyo utamweka huru, atwambie bila kificho tena waziwazi basi mlolongo utafata kila mtu atasema ukweli, Kikwete, Chenge, Sitta, Rostam na Mwakyembe wote watasema ukweli mtupu na iwapo kweli Lowassa atajitokeza hadharani na kusema pasipo kumung’unya basi uamuzi wake huo usipokelewe kama amekuja kufukua kaburi bali atazamwe kama amekuja kuweka shada la maua juu ya kaburi….. A Luta Continua! Nani bora anayeandika kwa taaluma yake au mimi nayeandika nachokiamini? Nova Kambota Mwanaharakati, Nipigie; 0717 709618 au +255717 709618 Niandikie kwenda: novakambota@gmail.com kwa habari zaidi za uchambuzi nitembelee: www.novakambota.com Tanzania, East Africa, Jumamosi 11, Juni 2011. I came across this question posted on Yahoo!'s Question and Answers and was very much interested to know what others have in mind. Below is the screen shot of the question, followed by 3 answers given so far. NICK It is not poor. They have gold, gas and agriculture, but like most of Africa have a lot of corruption. They encourage toursim LadyBug Tanzania isn't poor at all. They have a bunch of tourism. They have huge game parks, Masaii Mara being one of the largest in Africa. Also, Mount Kilimanjaro is also popular for many Europeans that like to travel. Dar es Salaam has huge ports for shipping and exporting/importing. And Zanzibar is a gorgeous tropical island that is very popular with other Africans and Westerners. The government is one of the most stable in East Africa. The one huge problem I can think of is that several of its towns, like Arusha, use the hydro-electric plant for their electricity and TZ has been having serious drought for several years, decreasing the levels of the river used for electricity. It's set things back a bit, but most places have gas powered generators.Source(s):I lived in TZ for 3yrs, my family is still there. Watu Safaris Tanzania is among the poor countries in Africa, this has been contributed by many factors regardless of having millions of resources to make Tanzania and same other countries in Africa rich. The reasons to why Tanzania is poor are as listed bellow 1. Improper use of resources - many resources have been used in an appropriate ways leading to lack of development from family to nation level. This can be put into the form of Natural resources, funds people have been miss using funds on unwanted programs/plans hence leaving the targeted developments programs without funds to work with. 2. Corruption and selfishness - most leaders have been thinking on their own benefit rather than to the national benefits that's why many leaders have been involved in high level corruption on National programs and fund hence leading the country into poverty. This has included entering into void contracts, buying used equipments rather than new ones just to save money for themselves, and etc 3. Poor infrastructures - roads and rails have been the back bone on transportation in Tanzania but most roads are not accessible through out the year which makes difficult to travel and transport things around the country. 4. Foreign investors - most of these investors are from abroad and most of the investments benefits they get always goes out of Tanzania and only small amount will remain to be circulated in the Tanzanian economy. Also some sectors which seems to bring lots of money in Tanzania is tourism but still majority of investors in this field are foreigners and the big portion of the income from Tourism goes out of Tanzania the same goes for investors in mining, Natural resources, etc. How to tackle these problems 1. It is important that all resources allocated to national programs, projects etc are used accordingly to attain the required results. 2. Leaders and everyone involved in leading other people should make sure that they do not think of themselves rather they should work for the country to bring about social and economic development, stop corruption in all levels of national activities. 3. Use the available resources to improve infrastructure so that transportation can be easy and less expensive. 4. Encourage local investors to invest in their economy since all the money will remain in Tanzania and will be felt in the Tanzania economy from family to National level. Hope this helps, if you have more questions let me know and i will help in anyway. Tafakari hii imeandikwa na Albert Kissima na kuchapishwa katika blogu yake ya "Mwangaza" P.W Botha alikuwa ni raisi wa zamani wa Afrika ya Kusini wakati nchi hii ilipokuwa inatawaliwa. Kuna wakati Raisi huyu alilihutubia baraza lake la mawaziri na nakala ya hotuba yake iliandikwa katika gazeti la Sunday times la Afrika Kusini na David G. Mailu tarehe 18 August 1985. Botha aliongea mengi yaliyoonekana kuwakashifu waafrika. Miongoni mwa mambo aliyoyayongelea ilikuwa ni hili: "By now everyone of us has been seen it practically that Blacks cannot rule themselves. Give them guns and they will kill each other". Naam, hadi sasa, nchi zote za Afrika hazitawaliwi tena na wakoloni wa kutokanchi za ng'ambo; tulishapata uhuru wa kujioongoza kama sio kujitawala. Hali halisi inaonesha tunashindwa kutumia vizuri ule uhuru wa kujiamulia mambo yetu wenyewe; uhuru ambao tuliutafuta wenyewe kwa kumwaga damu ilipobidi. Najaribu kutafakari kuhusu Afrika ya sasa. Hakuna dalili iliyowazi kweli kuwa waafrika hatuwezi kujiongoza (kidemokrasia) kama alivyosema ndugu Botha miaka kadhaa iliyopita pale aliposema: "By now everyone of us has been seen it practically that Blacks can not rule themselves. Give them guns and they will kill each other"? Kwa tafsiri ya leo, uhuru wa kujitawala umekuwa silaha mbaya sana. Tumevuka mipaka ya uhuru tulioutafuta wenyewe kwa hali na mali. Tumejitawala badala ya kujiongoza; tumerudisha matabaka ya kikoloni, watawaliwa na watawala. Uhuru tulipewa (baada ya kuupigania). Hatua ambayo ilikuwa ya umuhimu sana. Kwa hali ya Afrika ya sasa, naweza kusema kuwa Botha alitumia tafsida pale aliposema "give them (Africans) guns, they will kill each other". Yawezekana alimaanisha kuwa, wape waafrika uhuru, uone namna watakavyojitawala; uone namna watakavyokandamizana, uone namna watakavyoumizana na mwisho kuuana. Hawataitambua demokrasia inayowapasa: Ile ya kisiasa wala ile ya kiuchumi. Ndiyo, tumepewa uhuru. Badala ya kujiongoza tumejitawala. Uhuru umekuwa silaha ya kukwamisha maendeleo. Uhuru umezaa wakoloni wazawa; uhuru umezaa silaha nyingi nyingine ambazo tunazitumia kuangamizana, tunazitumia kuuana kama alivyotangulia kusema ndugu Botha. Ufisadi, rushwa, upindishaji wa sheria ziainishwazo wazi nakatiba na kugombania madaraka ya kutawala (wala si kuongoza), ni miongoni mwa silaha zilizoota mizizi baada ya uhuru (ambao mimi naona ni silaha nambari moja katika karne hii katika bara letu la Afrika) . Silaha hizi kiukweli zinatuua waafrika hususani watanzania. Hali ya maisha inazidi kuwa ngumu kwa walio wengi. Tunanyanyasana, matabaka tayari yapo, tunauana wenyewe kwa wenyewe. Wazawa wachache wanatafuta kutawala (kuliko kuongoza) ili kujinufaisha wao. Wanatafuta maisha mazuri yenye kila watakalo. Wanajitahidi kurefusha maisha yao (wanazuia wao kutokufa) kwa kuua walio wengi. Tumeshuhudia migogoro ya kisiasa katika nchi nyingi za Afrika. Baadhi ni Zimbabwe, Kenya, Madagaska, Ivory Coast, Sudan, Somalia n.k. na sasa Tanzania ambapo hali ya kisiasa si ya kuridhisha. Mifano hai katika Tanzania ni mauaji yaliyotokea Zanzibar katika uchaugzi wa mwaka 2005, maualji ya watu wasio na hatia mkoani Arusha katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, hata na yale ya Nyamongo mkoani Mara. Madhila yote haya yalikuja baada ya nguvu kubwa ya dola kutumika. Mamia ya watu hadi sasa wapo jela pasi na hatia kwa sababu ya matumizi yasiyo stahiki ya madaraka. Tunaodhani kuwa ni viongozi, hawaongozi bali wanatumia madaraka yao kuwachapa wanyonge kwa fimbo ya uhuru wao wa kugeuza sheria na kuzitumia kwa kadiri ya wawezavyo ili kutimiza matakwa yao. Ndio maana haishangazi kuona mahakama zetu za Kiafrika zinavyotoa maamuzi yasiyotegemewa na yasiyo ya kikatiba wala kitaaluma bali ni mashinikizo tu ya watawala fulani. Tanzania yangu ndio hiyo inayoelekea kuadhimisha miaka hamsini ya uhuru wake. Ni yapi tunajivunia baada ya miaka hii hamsini? ujenzi wa barabara ama? shule za kata au? hospitali? Lakini tukumbuke kuwa wakoloni walijenga mashule na mahospitali mazuri sana, mengine hadi leo yanatumika na bado yapo imara. Labda Afrika ya Kusini isingekuwa kama ilivyo hivi sasa kama wakoloni wangeondoka miaka hamsini iliyopita. Kwa mtazamo wangu, uhuru tuliutafuta ili tuweze kutumia uzalendo wetu kwa uhuru na kwa kiwango cha juu kabisa. Uzalendo hapa unabeba maana ya uwajibikaji wa kujituma kwa manufaa ya Taifa, jamii kwa ujumla na kwa mtu mmoja mmoja. Miaka hamsini tangu tupate uhuru.Tupo huru kutumia uzalendo wetu kuijenga nchi? "Give Africans guns, they will kill each other", labda Botha alieleweka vibaya, ilikuwa ni tafsida tu! ![]() photo : google images Yupo Mtanzania mmoja amekerwa sana kwa wivu wa maendeleo, baada ya kusikia habari katika redio moja ya Rwanda zikisema kuwa shirika la ndege la Rwanda, RwandaAir lina safari zake nyingi kwenye miji mikubwa nchi za maziwa makuu na, wanao mpango unaokamilika hivi punde wa kuanza kuruka kwenda Urabuni. Kwetu Tanzania, shirihirika letu la ndege, ATCL, linakufa. Akauliza, "Why can't we learn form others? Hii nchi inatia hasira mazee!" Mtanzania mwenzie akamjibu jibu ambalo linafaa kuwa nukuu ya leo ya Mtanzania kwa kuwa linazungumza ukweli ulio wazi, na asiyeuona ukweli huu, hatufai: "What's wrong is that... we educated cream of this country are not doing anything rather than criticising the government behind our desktops, hoping that one day the so called 'walalahoi' who are now referred to as 'people's power' will one day wake and remove this government for us, and let us enjoy their sweats! This is bull shit... If something is wrong we are the eyes of illiterate Tanzanians, we have to show them something is wrong and give them options for solutions, sio tunachapa keyboard tu then inakuja topic nyingine tunachapa keyboard... siku inaisha tunaingia kwenye mikoko yetu tena ya 2nd hand kwenda kunywa laga za jioni, then home... make love to our wives/girlfriends/fiancees/vimada, and then tomorrow we do the same old shit! THATS MY BROTHER... IS THE PROBLEM!" Mauaji yaliyotokea huko Tarime hivi karibuni si jambo geni kutokea katika maeneo ya machimbo ya vito vya thamani ndani au nje ya Tanzania. Tukirejee kisa cha mwanaharakati, marehemu, Ken Saro Wiwa. Ingawaje kila mtu anayefahamu habari hii anaweza akawa na msimamo wake, na ni sahihi kufanya hivyo kadiri ya maelezo mtu aliyonayo kuhusiana na kisa chenyewe. Binafsi ni miongoni mwa wanaoafiki maelezo yaliyotolewa na kundi la wanaharakati watetea haki za binadamu na mazingira walioainisha kuwa marehemu Saro Wiwa alishitakiwa na hatimaye kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa na mahakama ya kijeshi kwa sababu za "kutilia mchanga kitumbua chao". Tunaamini kuwa Saro Wiwa aliuawa siyo tu "kupunguza usumbufu kwa viongozi waliopoteza utu, bali pia ilikuwa onyo kwa yeyote mwenye kuthubutu kutia mchanga kitumbua cha wakubwa". Ukweli tunaousimamia ni kuwa, Ken aliuawa kwa kuwa tu "alikula nyamu" kutetea kabila dogo la Waogoni wa Niger Delta na kukemea kwa nguvu zote uharibifu wa mazingira uliokuwa ukifanywa na makampuni yaliyokuwa yakichimba nishati ya mafuta na kuisafisha kisha kujipatia faida kubwa il hali wananchi na eneo zima la Ogoni waliachwa na madhara ya uharibifu mkubwa wa mazingira ambao ulitishia ustawi na uhai wa watu walioishi pale, mazao yao, uoto wa asili na raslimali yao ya mifugo. Maneno ya mwisho aliyoyatamka Ken kabla ya kunyongwa yalikuwa, “Lord take my soul but the struggle continues.” "Muumba ichukue nafsi yangu ila mapambano yanaendelea" - tafsiri ya Kiswahili kadiri ya uelewa. Unaweza kutizama video za Ken Saro Wiwa enzi za uhai wake kupitia Youtube.com/user/remembersarowiwa Turudi kwetu nyumbani Tarime. Wenyeji wa asili wa maeneo ambako Makampuni yanayochimba dhahabu, almasi, tanzanite na vito vingine vya thamani nchini Tanzania wamekuwa wakilalamika mara kadhaa kutokana na baadhi ya vitendo vya makampuni visivyokubalika katika jamii husika. Madhara makubwa yatokanayo na machimbo ya madini yamewahi kutokea nchini katika maeneo mbalimbali. Mojawapo ni lile lililotokea mwaka 1996 katika machimbo ya Bulyanhulu na kusababisha, aliyekuwa Mwenyekiti wa TLP ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Vunjo, Augustine Lyatonga Mrema kupiga mbiu kubwa sana na kutaka uchunguzi ufanyike kuhusiana na mauaji hayo. Bofya hapa kusoma taarifa hiyo. Mwaka jana yupo mwandishi wa habari wa kigeni akishirikiana na raia wanaharakati wa Tanzania alichapisha video iliyoonesha mauaji yalivyofanyika kwa wakazi wa eneo ambalo linaendelea na shughuli za uchimbaji madini hadi leo. Lengo kuu la mauaji hayo lilikuwa ni kuwafurusha wananchi waliogoma kuondoka katika maeneo hayo yenye utajiri, maeneo yao ya asili ambayo walizaliwa na kuishi humo kwa miaka nenda rudi. Kwa bahati mbaya, video ile iliondolewa mtandaoni baada ya vitisho vibaya sana, lakini ipo neema kwenye usemi kuwa "ukweli haufichiki kamwe, ila waweza tu kucheleweshwa kujidhihirisha" kuna wanaharakati wa haki za binadamu na wazalendo waliofanikiwa kupata nakala za video hiyo na kuzisitiri katika maktaba za majumbani mwao. Pengine itachukua muda, lakini ukweli huvumilia hadi unapojidhihirisha. Mathalan, walioamuru kwenye mtandao kwa video ya mauaji yaliyofanyika huko kanda ya ziwa ili kuwahamisha watu katika makazi yao iondolewe mtandaoni, walisahau kuwa zipo picha mnato ambazo zimezunguka mitandaoni zikidhihirisha kuwa makampuni hayo yamechafua mazingira na uoto wa asilibali pia kusababisha madhara makubwa kwa binadamu ambao ndiyo wenye haki ya msingi ya kufaidika na raslimali mali zilizomo kwenye ardhi yao ya asili. Picha hizo zinaonekana hapo chini na ziliwahi kuchapishwa hapa (bofya kurejea chapisho hilo). Wakadiriki kuulazimisha umma uamini kuwa madhara hayo hayakutokana na sumu zinazomwagwa na mitambo yao, wakataka wananchi waamini kuwa ni hali iliyojitokeza. Na mtu ujiulize, iweje watu hawa waishi katika maeneo haya kwa karne na miongo kadhaa bila kupatwa na madhara, lakini miaka michache tu baada ya kampuni kuanza shughuli zake, madhara yaanze kuonekana? Watasema ah, wananchi wenyewe walifuata maeneo ambayo hawakupaswa kufuata. Beh! Kwani kampuni ilishindwa vipi kutoa elimu na kuhakikisha uchafu wanaoutoa hauingii karibu na makazi ya watu? Tuliache hilo. Tuje kwa watawala wetu. Inakuwaje vigumu kwa watawala kufahamu kuwa harakati za wananchi za mara kwa mara kupinga na kutaka kuharibu mali za makampuni/wawekezaji, zinatokana na ukweli kwamba wananchi hawaoni faida inayoletwa na uwepo wa makampuni haya, kwa hivyo, wanataka majibu yanayoeleweka? Kwamba, watawala hawafahamu kuwa wananchi kwa kukosa mbinu za kuwafuata viongozi hao maofisini mwao huko Dar Es Salaam, na kutokana na viongozi kuwaona wananchi kwa nadra, hasa pale inapotokea kutokuelewana au nyakati za uchaguzi tu, na kwa kuwa wananchi hawapati majibu ya kuridhisha kutoka kwenye makampuni husika kwa maelezo kwamba Serikali ndiyo msemaji mkuu, basi, viongozi hawaoni kwamba wananchi wataamua kuwashughulikia wawekezaji hao ili kutuma ujumbe kwa viongozi? Nadhani viongozi wetu wanayo dhana vichwani mwao kuwa uharamia unaofanywa na baadhi ya Wasomali kuteka meli zilizosheheni mali na watu kisha kudai kiasi kikubwa cha fedha kwa mwenye meli kama fidia kwa matumizi ya maeneo yao ya maji; kwamba hilo halifanani na wananchi wa maeneo ya machimbo kutaka kuwaharibia wawekezaji ili kutuma ujumbe kwa Serikali na Viongozi kuwa tunahitaji huduma zinazoendana na shughuli inayofanyika katika eneo letu. Mtu yeyote makini anapaswa kujifunza kwa mifano, si lazima iwe tukio halisi linaloendana na hali anayoikabili. Sielewi kama ni dharau au pengine ni viongozi wetu kuwa na shughuli nyingi, hata wanashindwa kupanga muda wa kutosha wa kujadili na wananchi wao matatizo yanayowakabili na kusikiliza mapendekezo yao? Ipo hii tabia mbovu kweli ya baadhi ya viongozi ya kwenda kwa wananchi na kuwaambia yale wao (viongozi) wanayoyaona ni sawa na yanafaa kwa jamii ile, halafu wakaondoka wakidhani wamemaliza kuhubiri, wakasahau kuwa wananchi ndiyo wasemaji wa mwisho ikiwa wameelewa kweli ama la. Kiongozi unapoondoka ukidhani umeeleweka, basi subiri muda upite uuone mwenendo na kusikia mrejesho ndipo utaelewa ikiwa kweli ulichohubiri kilieleweka au unahitaji kubadili mbinu ya ueleweshaji. Nikiri kuwa baadhi yetu tunakerwa na matumizi mabaya ya siasa, hasa pale inapoingilia na kuvuruga ukamilifu wa mambo. Ninajiuliza, ikiwa njia zinazostahili kufuatwa ili kupata ufumbuzi wa matatizo yetu zimeshatumika, na wahusika wanaona bado hawajapata suluhu waliyoitaka, je, ni kosa kwa siasa kuingilia kati? Siasa ni njia mojawapo ya kutoa taarifa ya yanayoendelea. Hatuwezi kuikataa. Tuifuate kwa uangalifu. Lakini, inawezekana kuwa tunaielewa visivyo siasa kiasi kwamba mtu anapofanya jambo lolote, kwa kuwa tu ametokea kuwa mwanasiasa, basi talanta nyingine alizokuwanazo hazipaswi kuonekana kwa kuwa tu, amekuwa mwanasiasa? Je, hili si kosa? Tukubali kuwa mtu aweza kuwa zaidi ya jambo moja. Mtu aweza akawa mwanasiasa, vile vile mwanataaluma, mfanyabiasahara, kiongozi wa imani, mwanamichezo, na kadhalika, alimradi utendaji wake wa kazi katika kutimiza jukumu fulani hauingiliani na talanta zisizohitajika. Pengine nasi kwa kuwa na mtizamo wa mrengo mmoja, tumewafungia vibandiko fulani watu fulani fulani kuwa kwa kuwa wapo hivi, basi hawapaswi kuwa hivi. Hivi, kisa cha Ken Saro Wiwa na yaliyokwisha kutokea Tanzania na kwingineko, hayatoshelezi mafunzo? Kwa nini hawataki kujibu hoja? 26/05/2011
Na Nova Kambota, Tangu kuibuka kwa maandamano ya CHADEMA ya mkoa kwa mkoa kuna mambo kadhaa yaliyojitokeza na yanaendelea kujitokeza ambayo yanadhihirisha kile ambacho wachambuzi hukiita “ ombwe la uongozi” , kwa kujua au kutojua tumeshuhudia mara kadhaa serikali ikiacha kila mwenye kuweza aisaidie serikali kujibu hoja na kibaya zaidi ni kuwa wasaidizi hawa wanaonekana kupwaya mno kwenye kujibu hoja za msingi badala yake wamegeuka kuwa waropokaji. Miongoni mwa watu wanaofanya kazi isiyowahusu ni pamoja na watendaji mbalimbali wa chama tawala CCM ambao wamekuwa na tabia hii inayorudisha nyuma maendeleo, viongozi hawa wa CCM wamelewa madaraka kiasi kwamba wanajiona wao ndiyo serikali na serikali ndiyo wao, wamefikia hatua ya kupindisha ukweli na kuendesha vituko na siasa za majitaka kwenye mambo ya msingi yanayogusa wananchi . Chukulia mfano wa hoja zinazotolewa na CHADEMA kwenye maandamano yao ambazo kwa hakika ni sauti za wananchi tena masikini kabisa ambao wanaiuliza serikali yao juu ya mustakabali wa maisha yao na watoto wao, cha kuhuzunisha ni kuwa licha ya mikutano hii ya CHADEMA kuwa ya halali kabisa kikatiba pia kuendeshwa kwa utulivu mkubwa bado serikali inachukulia kuwa ni uchochezi hivyo badala ya kuja na majibu ya msingi ya hoja zinazoibuliwa kwenye mikutano hiyo serikali imewaachia wanapropaganda wa CCM kuyumbisha nchi wanavyotaka. Hivi CHADEMA na wananchi wanapohoji juu ya ubabaishaji kwenye shule za kata kuna kosa hapo? au pale mwananchi mmoja wa Mbeya alipotaka kufahamu hiyo meli waliyoahidiwa ziwa Nyasa itakuja lini kuna kosa hapo? au yule mwananchi wa Rukwa aliyetaka kufahamu lini serikali itahakikisha huduma za afya zinakuwa za uhakika? Au kuna tatizo lolote wavuja jasho wa nchi hii wanaposema kwa sauti kubwa kuwa hawataki kulipa madeni ya kubambikiwa kama Dowans? Hivi hapa kuna tatizo lolote? Kwanini serikali isitoe majibu ya kina kwa maswali haya badala yake wanaachiwa waropokaji? Au serikali inadhani wananchi masikini wa taifa hili wanashiba kejeli za viongozi wa CCM? Wakati wananchi wanataka kuona wezi wote wa mali za umma wanafikishwa mahakamani bila huruma tena pia wanataka kufahamu ufisadi unaonuka kwenye ofisi za serikali utakoma lini? cha ajabu anaibuka Nape Nauye katibu wa itikadi na uenezi wa CCM anamtuhumu Dr Slaa kuwa na yeye ni fisadi tu, hii ndiyo nini sasa?, hapa ndiyo watu wanahoji Nape katumwa na nani kuwadhihaki masikini wa taifa hili? Kwanini asikae kimya akamwacha Dr Shukuru Kawambwa akatujibu ni lini shule za kata zitaboreshwa? Itamgharimu nini Nape kukaa kimya ili Kikwete atwambie Dowans tunawalipa kwa misingi ipi? Wananchi wanahoji kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha, bei ya vitu imepanda na viongozi wa CHADEMA wanaitaka serikali kuhakikisha bei ya vitu inashuka ili kumsaidia mvuja jasho , haya ni mambo ya msingi sio mzaha kabisa, sasa Nape anaita waandishi wa habari kisha anasema Dr Slaa ni fisadi na Mbowe ni fisadi wakae kimya mara moja! , haya kama sio matusi ni nini? huu ni mzaha kwa wananchi na inabidi kukemewa haraka vinginevyo tabia hii itaendelea kukua mwisho wa siku tutamwona katibu mkuu wa CCM akisoma hotuba ya mwisho wa mwezi kwa niaba ya rais wa nchi, ndiyo inaonekana kama kichekesho ila hakika tunaelekea huko. Ni lazima kama taifa ifike sehemu tufahamu kuwa kuna mambo ya siasa na maisha ya watu hivyo tusiweke mzaha kwenye kila jambo ni lazima wananchi wanapoihoji serikali basi ni watendaji wa serikali wanaopaswa kujibu, viongozi wa chama wakae kimya waache kuropoka hovyo wakumbuke kuwa hii nchi ni yetu sote hivyo wasijifanye kujimilikisha. Sidhani kama serikali imefaidika kitu na majibu ya kejeli yanayotolewa na viongozi wa CCM kwa wananchi badala yake wananchi wanazidi kujenga chuki dhidi ya serikali yao. Wananchi wanaendelea kuuliza na wataendelea kuhoji kwanini viongozi wa serikali hawajibu hoja? Hakika hili litaendelea kuwaandama kokote walipo na kamwe haliwezi kupoozwa kwa kuwaruhusu viongozi wa CCM kuropoka hovyo bila mpangilio pasipo kujua kuwa wanazidi kukoleza chuki. Naam! imefika wakati sasa serikali iache kufanya vitu kwa mazoea, iache kutoa majibu ya zamani kwa maswali mapya halikadhalika iache kutoa majibu mepesi kwa hoja nzito, propaganda zozote za kuwatumia kina Nape na viongozi wengine wa CCM kuzima hoja za msingi za wananchi hazina manufaa yoyote badala yake zinazidi kuibomoa na kuidhoofisha serikakali…..Tafakari! 0717 709618 / 0766-730256 novakambota@gmail.com http://novatzdream.blogspot.com | Vitabu vya WatanzaniaBofya picha ya kitabu unachokitaka ili ujinunulie nakala
Yaliyomo/CategoriesAll Hifadhi/ArchivesFebruary 2012 |









RSS Feed