wavuti
 
500 bandwidth limit TBC
Jana nilikuwa mmoja wa watu wenye furaha baada ya kuiona TBC hewani, lakini kwa bahati mbaya tabasamu langu halikukawizwa kutiwa nyongo mara mbili.
  • Moja ni baada ya tovuti hiyo kuzidiwa na wingi wa watu walitaka kujionea kilichomo.
  • Pili ni baada ya kupata lalamiko la mwanahabari mmoja kuwa habari zao zimetumiwa bila idhini yao.
Mchangiaji mmoja anasema hawa kama hawana uwezo wa kuwa na 'host' anayewapa 'bandwidth' ya kutosha, wawasiliane naye atawapa ya kutosha tena kwa bure. Nadhani hii ni changamoto kwa TBC, siamini kuwa hawana uwezo wa kununnua 'bandwidth' ya kutosha umma wa Watanzania wachache wanaotumia intaneti, ila nadhani wanahitaji kujipanga upya na kuja mtandaoni rasmi. Ninaafiki maoni ya mchangiaji mmoja kwenye kundi hilo hilo ilkotoka changamoto hiyo, eTTTz, aliposema huenda hawa walikuwa kwenye majaribio na ilikuwa haijazinduliwa rasmi.
Basi itakuwa ni kiherehere changu tu kimenizodoa sasa inabidi nitulie mpole ka maji ya mtungini alfajiri.

Suala la matumizi ya habari ya aina yoyote ile lina sheria zake na taratibu za kufuatwa kabla ya kutumika. Aidha, yapo makubaliano maalumu baina ya mtoa taarifa na yeyote ambaye angependa kuitumia taarifa hiyo, iwe ni taarifa kwa njia ya picha, maandishi ama sauti alimradi ni ya kidigitali, basi huwa inalindwa na sheria za World Intellectual Property Organisation kifupi WIPO na Digital Copyright Millenium Act, kifupi, DCMA.

Zipo haki ambazo mmiliki huzitoa kwa kuridhia makubaliano ya Creative Commons (CC) au maelezo ya Terms and Conditions au Privacy au Disclaimer nk. Yeyote anayetumia kazi hizo hupaswa kuonesha shukrani kwa kueleza alikoitoa habari kwa namna yoyote ikiwa ni pamoja na kumtaja mwenye habari au kuweka linki ya ilikotoka habari (chanzo cha habari).

Inapotokea hali ya wizi au matumizi yasiyo ya haki ya habari, mwenye habari anahaki ya kumwandikia aliyetumia kazi yake isivyo, na kumtaka airekebishe au aombe samahani ama aiondoe habari hiyo (na wakati mwingine afanye mawili kati ya hayo) vinginevyo, ni rahisi sana kumburuza mtu huyo mahakamani. Zipo sheria zinazotuatwa na nchi kadhaa zimeridhia na kukubaliana na sheria hizo. Kadiri matumizi ya intaneti yanavyoongezeka, ndivyo sheria hizi zinavyozidi kuboreshwa na kutumiwa katika nchi mbalimbali.

Aliwahi kuniibia kazi zangu mtu mmoja na baada ya kukosa muafaka naye, ilinibidi kumripoti, na blogu yake ilifutwa kabisa mtandaoni mara moja.

Nakubali kuwa nimewahi na huenda nitaendelea kutumia kazi za watu pasipo ridhaa zao rasmi, si kwa kusudio baya hata kidogo, aidha ni kwa kuwa ni vigumu kuwapata wahusika halisi wa kazi hizo, au itanichukua muda mrefu sana kusubiri kupata haki ya matumizi hayo, hivyo nimekuwa nikizitumia  na kusema nilikozipokea na kisha inapobidi kuziondoa, huwa ninafanya hivyo punde tu ninapotakiwa kufanya hivyo na mmiliki husika.

Tujifunze (mimi mmojawapo) kujali na kuheshimu itakikanavyo kazi za watu wanazozitokea jasho, kutokufanya hivyo tutawavunja moyo wengi na hivyo tukose mengi.
tbc.go.tz
muonekano wa TBC tarehe 27 Oktoba 27
 


Comments




Leave a Reply