wavuti
 
Katika Mkutano uliofanyika tarehe 27 Octoba 2009 ukishirikisha Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Wakala wa Usajili na sheria za Biashara (BRELA), and Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) zikiwa ni taasisi zinazosimamia shughuli za kampuni chini ya sheria mbalimbali, mambo yafuatayo yalijitokeza.

I. Yaliyojitokeza
1. Kukiuka Kanuni za Kimataifa za Kihasibu (IFRS)
Baada ya NICOL kuwasilisha taarifa ya hesabu za fedha zilizokaguliwa kwa mwaka ulioishia tarehe 31 Desemba 2008, katika kupitia taarifa hizo, CMSA ilibaini kuwa utayarishaji wa taarifa hizo haukuzingatia kanuni za kimataifa za uandishi wa vitabu vya hesabu za fedha (uhasibu) yaani International Financial Reporting Standards (IFRS) na pia ilibainika kuwa hesabu hizo zinapotosha hali halisi ya kifedha ya Kampuni ya NICOL (financial position) na faida ambayo NICOL iliripoti. Mkutano huo ulithibitisha kuwa:

(a) CMSA na NBAA kwa pamoja walitoa maagizo kwa Wakaguzi wa hesabu wa Kampuni ya NICOL wamtake mteja wao, NICOL kuwa:-
(i) aondoe taarifa za hesabu za mwaka unaoishia tarehe 31 Desemba 2008 kwa kuuarifu Umma (press release)
(ii) atayarishe upya taarifa hizo kwa kufuatana na kanuni za kimataifa za kihasibu na kuziwasilisha kwa ukaguzi kulingana na Kanuni za kimataifa za Ukaguzi wa hesabu yaani International Standards on Auditing (ISAs)..
Sababu kubwa ya kuitaka NICOL iondoe taarifa za hesabu zake ni kuwa taarifa hizi za hesabu za fedha zilikuwa hazitoi ukweli kuhusu hali halisi ya kifedha ya kampuni na hivyo kupotosha Umma.
(b) Wakaguzi wa Hesabu wa NICOL walikiri kufanya makosa kwa kutoa hati safi (unqualified audit opinion) kuhusiana na taarifa hizo za hesabu za kampuni ya NICOL na Kumtaka mteja wao atayarishe upya hesabu hizo kufuatana na kanuni za kimataifa za Kihasibu na kuziwasilisha kwao kwa ukaguzi kabla ya kuzitoa kwa Umma.
(c) Endapo taarifa za hesabu za Kampuni ya NICOL zingetayarishwa kuendana na kanuni za kimataifa za uandishi wa vitabu vya hesabu za fedha hali ya kifedha ya NICOL na faida iliyoripotiwa ingekuwa tofauti kabisa na ripoti yao potofu inavyosema.

2. Kuitisha Mkutano Mkuu wa Wanahisa Kinyume na Matakwa ya Sheria ya Makampuni.
Katika kulinda maslahi ya Wanahisa wa NICOL, CMSA na DSE waliiagiza Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya NICOL wasifanye mkutano wa Mwaka wa Wanahisa (AGM) bila kuwa na Taarifa za Hesabu sahihi na zinayokubalika kwa mwaka unaoishia tarehe 31 Desemba 2008 kama Sheria ya Kampuni ya mwaka 2002 inavyoelekeza. Kwa mujibu wa sheria ya Makampuni, uwasilishaji wa taarifa za fedha zilizokaguliwa ni moja ya kipengele cha lazima katika ajenda za Mkutano wa Mwaka wa Wanahisa.

3. Kukaidi Kutekeleza Maagizo na Kutoa Taarifa Potofu kwa Wanahisa
(a) Wakurugenzi wa kampuni ya NICOL pamoja na kutakiwa na Mamlaka tatu za usimamizi, NBAA, CMSA and DSE walikaidi agizo la kutayarisha upya taarifa za fedha za Kampuni kwa Mwaka Ulioishia tarehe 31 Desemba 2008.

(b) Pamoja na kukumbushwa mara kadhaa na kushauriwa na Wakaguzi wa Kampuni, Wakurugenzi wa NICOL walikaidi agizo la kuondoa taarifa hizo za hesabu. Kibaya zaidi Wakurugenzi wa NICOL waliweka kwenye ripoti ya Mwaka Maoni ya Wakaguzi (audit opinion) huku wakijua kwamba tayari wakaguzi hao walishaondoa maoni yao.

(c) Wakurugenzi wa NICOL waliendelea kuitisha mkutano tarehe 24 Octoba 2009 na wakagawa kwa Wanahisa pamoja na nakala nyinginezo, Ripoti ya Mwaka ambayo ina mahesabu ambayo Mamlaka za usimamizi ziliagiza ziondolewe kwa sababu zilikuwa zikitoa taarifa potofu kwa Wanahisa.

(d) Wakurugenzi wa NICOL wamekaidi kurekebisha taarifa zao kama Mamlaka za Usimamizi zilivyoelekeza. Wakurugenzi wa NICOL walitakiwa kutekeleza kwanza maagizo waliyopewa kabla ya kuitisha Mkutano Mkuu wa Wanahisa ili wasiwape wanahisa taarifa potofu.

4. Wakaguzi Kuondoa Maoni yao Kuhusiana na Mahesabu na Hatima yake.
Kutokana na kukosekana ushirikiano kutoka kwa Wakurugenzi wa NICOL, Wakaguzi wa Hesabu kupitia barua yao nambari MACO/NICO/10/09 ya tarehe 8 Octoba 2009 waliondoa maoni yao (audit opinion) juu ya taarifa hizo za hesabu za Fedha za NICOL kwa mwaka ulioishia tarehe 31 Desemba 2008 na kumtaka mteja wao arudishe kwao nakala zote zilizosainiwa za mahesabu hayo. Kuondolewa kwa Maoni kuhusiana na hesabu maana yake ni kuwa NICOL haina taarifa za hesabu za fedha zilizokaguliwa kwa mwaka ulioishia tarehe 31 Desemba 2008.

5. Kampuni ya NICOL Kufanya Maamuzi ya Uwekezaji Bila Kufanya Uchunguzi Yakinifu
Baada ya zoezi la ukaguzi lililofanywa na CMSA (onsite inspection), ilithibitika pia kuwa, Wakurugenzi wa Kampuni ya NICOL wamefanya maamuzi mbalimbali ya Uwekezaji bila ya kufanya uchunguzi yakinifu (Due Diligence) na hivyo kuwa na uwekezaji wenye ubora hafifu kama ilivyowekeza kwenye makampuni ya Interchem Pharmaceutical and Beverage Limited (IPBL) na Twiga Feeds Ltd na hivyo kuhatarisha maslahi ya wanahisa. Wakurugenzi wa NICOL waliagizwa waajiri Mtaalamu wa Mambo ya Uwekezaji (Fund Manager) ili awashauri katika kufanya maamuzi ya uwekezaji. Mpaka sasa hawajatekeleza agizo hilo pamoja na kukumbushwa mara kadhaa.

II. Maoni na Mapendekezo ya Mamlaka Zinazosimamia Kampuni kwa Mkutano wa Wanahisa Uliopangwa Kufanyika Tarehe 31 Octoba 2009.
Kufutia maelezo hayo hapo juu, ni wazi kuwa Wakurugenzi wa kampuni ya NICOL wamekuwa wakaidi na wameshindwa kutimiza wajibu wao. Wanahisa wana haki katika Mkutano Mkuu kuteua Wakurugenzi na inapoonekana muhimu kuwaondoa. Mamlaka zinazosimamia shughuli za kampuni tuna maoni na mapendekezo yafuatayo kwa Mkutano wa Wanahisa uliopangwa kufanyika tarehe 31 Octoba 2009.

Wakurugenzi wa kampuni kwa kipindi kinachoishia tarehe 24 Octoba 2009 hawana sifa ya kuendelea kuwa wakurugenzi na hivyo wajiuzulu au waondolewe. pia hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002.
Bodi mpya iahidi kwamba itatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mamlaka za Usimamizi.

III. Kushindwa kwa Wanahisa Kutekeleza Mapendekezo ya Mamlaka za Usimamizi
Wanahisa wanatakiwa watambue kwamba wakishindwa kutekeleza kwa ukamilifu mapendekezo ya Mamlaka za Usimamizi itapelekea Mamlaka hizo Kuchukua hatua kali dhidi ya Kampuni kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo.
 


Comments




Leave a Reply