Gazeti tando la HabariLeo linaripoti: Kwa mujibu wa maoni ya utafiti huo uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya utafiti ya Afro Barometer yenye makao makuu nchini Ghana na kuongozwa na Amanda Lea Robinson wa Chuo Kikuu cha Stanford, Marekani, nchi ya Tanzania imeweka rekodi ya aina yake barani Afrika kwa kuibuka nchi pekee yenye Wananchi wenye mapenzi makubwa kwa taifa lao kuliko jambo au mfumo wowote wa kitamaduni, kiuchumi au kijamii unaowagawa katika makundi mbalimbali na matabaka. Katika mahojiano hayo yaliyohusisha wananchi kati ya 1,200 na 2,400 katika kila nchi kati ya nchi 16 zilizochaguliwa kufanya utafiti kuhusu ujenzi wa Taifa katika nchi za Afrika, wananchi waliulizwa maswali ili kubaini iwapo wanajisikia fahari zaidi kutambulishwa kwa jina la taifa lao kwa mfano Mtanzania, au kwa jina la kitu kingine haswa kabila. Robinson ambaye ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Idara ya Sayansi ya Siasa ya Stanford University anasema katika utafiti huo uliotolewa Septemba mwaka huu kwamba wakati wastani wa wanaopenda mataifa yao katika nchi hizo ni asilimia 42 ya wahojiwa, kwa Tanzania wanaolipenda taifa lao ni asilimia 88 ya wahojiwa wote. Nchi ya pili kwa kuwa na wananchi wanaopenda Taifa lao kuliko kabila ilikuwa Afrika Kusini ambayo asilimia 63 ya wananchi wake wanalipenda taifa lao kuliko kabila, ya tatu Namibia ambayo wiki hii ilikuwa katika mchakato wa uchaguzi wa Rais. Nchi ya nne ni Senegal asilimia 51 na ya tano Madagascar, asilimia 50. Nigeria imekuwa ya mwisho kwa kuwa na asilimia 17 tu ya wananchi wake wanaolipenda taifa lao kuliko kabila. Rekodi hiyo ambayo ni moja ya kigezo cha nchi iliyo na ulinzi imara, imepatikana baada ya wananchi wa nchi za Afrika, wakiwemo Watanzania, kufanyiwa mahojiano maalumu kuhusu jambo la fahari wanalodhani ni muhimu kujitambulisha nalo kati ya mambo kadha wa kadha yanayotumika kumtambulisha mwanadamu. Vigezo vingine vinavyoifanya nchi kuwa na ulinzi imara na madhubuti licha ya uzalendo wa wananchi wake kulipenda taifa lao ni teknolojia ya vita, ushirikiano mzuri na nchi marafiki zikiwemo nchi jirani, wingi wa wanajeshi, bajeti inayotumika kwa ajili ya ulinzi na usalama na idadi ya watu. Soma habari nzima kupitia: http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=4594 CommentsLeave a Reply | Vitabu vya WatanzaniaBofya picha ya kitabu unachokitaka ili ujinunulie nakala
Yaliyomo/CategoriesAll Hifadhi/ArchivesFebruary 2012 |




RSS Feed