MTOTO wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete amemfikisha mahakamani fundi seremala na mkazi wa Mikocheni A, Bw. Omary Said (38) kwa kumtapeli sh. milioni mbili. Mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Bi. Lina Msanga, Mwendesha Mashitaka, Bi. Batiseba Kasanga aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Novemba 5, mwaka huu huko Mikocheni, jijini Dar es Salaam. Bi. Batiseba alidai kuwa mshitakiwa alipewa fedha hizo na Bw. Ridhiwani ambaye ni mwanasheria, kwa lengo la kununulia vifaa mbalimbali kwa ajili ya kukarabati nyumba yake, lakini fundi huyo alizitumia kwa matumizi mengine na hakufanya walivyokubaliana. Mshitakiwa ambaye amekana shitaka hilo amerudishwa rumande kwa kukosa wadhamini. Kesi hiyo ambayo upelelezi wake unaendelea itatajwa tena Desemba 8, mwaka huu.


RSS Feed