![]() Sheikh Yahya Hussein Habari hii imeripotiwa na Christina Gauluhanga na Stella na kuandikwa katika gazeti tando la DarLeo.co.tz MNAJIMU Mkuu wa Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahya Hussein, ametabiri kuwa mwanachama yeyote atakayejitokeza kuwania nafasi ya Urais ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2010 kumpinga Rais Jakaya Kikwete, atakufa ghafla. Akizungumza leo asubuhi nyumbani kwake, Sheikh Yahya amesema utabiri wake unaonesha kuwa Rais Kikwete ndiye mgombea pekee ndani ya CCM na ataibuka na ushindi wa kishindo. Amesema katika wosia ulioachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, unaonesha kuwa baada ya Rais Benjamin Mkapa kustaafu atayefuatia ni rais Kikwete. "Tunakumbuka sana maneno ya baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliyomwambia JK kuwa ‘goja awamu ijayo …mwachie Mpaka' kauli hiyo bado haijafutwa kwani mirathi kwa Mwalimu ni awamu mbili,”"amesema Sheikh Yahya. Pia ameongeza kuwa kuendelea kushika madaraka kwa Rais Kikwete katika uchaguzi ujao kutaleta Serikali ya Mseto Tanzania Bara na Visiwani ambapo Waziri Mkuu atatokea chama cha upinzani. Pia upinzani ndani na nje ya CCM utasambaratishwa na baadhi ya viongozi watajiunga na kambi ya Kikwete. "Hii haina mashaka na inaonesha njia iko wazi kwa JK kwa kuwa kila inapokaribia uchaguzi mkuu kiongozi mmoja hufa ambapo mwaka 2005 alikufa mwenyekiti wa CCM Songea hivyo kifo cha Marehemu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Laurence Gama, ambaye naye ametokea Songea, nayo ni ishara kuwa ushindi ni wa JK tu,"amesema Sheikh Yahya. Mnajimu huyo amesema hali ya uchumi ya Watanzania itakua ambapo pia kutatokea maandamano makubwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge wa pande zote wa vyama vya upinzani na CCM yatakayohusu wizi wa kura. Ameendelea kutabiri kuwa baadhi ya viongozi wa sasa wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere watajiuzulu kwa aibu itakayowafika ya kuihusisha taasisi hiyo na siasa ya kumpinga Kikwete wakati taasisi hiyo ni kusadia watu wote. Katika utabiri wake kwa mwaka 2010, amesema kutatokea ajali nyingi kwenye vyombo vya usafiri ambapo mwaka huo una sifuri mbili ambayo ni namba ya majini ambayo hupenda kusafiri na watu kila siku hata pia binadamu kwenda mwezini. CommentsLeave a Reply |