Jana hapa tumeona orodha ya Marekani ya nchi ambazo raia wake au watu wanaobeba pasipoti za nchi hizo watakavyokumbwa na adha ya usumbufu wa kukaguliwa maradufu ya wengine punde watakapokuwa wakisafiri. Aghalabu mambo kama haya yanapotokea, basi nchi nyinginezo pia huiga yayo hayo hata ikawa kero kila pahala.

Sasa hii kidali po iliyoanza baina ya nchi ya Kenya na Tanzania kumhusu bwana Abdullah Faisal nadhani haitatupeleka pazuri katika macho ya nchi nyingine za dunia. Nasema hivi kwa kuwa bwana huyu ana mlolongo wa vizuizi toka nchi kadha wa kadha kwa madai kwamba yeye anachochea vurugu baina ya matabaka ya binadamu kupitia hotuba zake. Bwana huyu anatuhumiwa ugaidi na kuhusika na vifo vya baadhi ya Wayahudi na Wahindi.

Alifikaje Kenya?
Inasemekana nchi kadhaa zimemzuilia huyu bwana asisafiri kwao iwe ni kwa njia ya anga, maji ama ardhini . Kwa hivyo amekuwa akisafiri kwa kujiiba kwa njia ya barabara akitumia magari. Katoka zake Nigeria  huko kapita hadi Angola, kaenda Msumbiji, Swaziland na Malawi mwishowe kakatiza Tanzania hadi alipokwamia Kenya hapo mwezi jana tarehe ya 24. Yasemekana kuwa safari yake  ilikuwa itamatie  kwao kwa asili Jamaika. Msemaji wa jeshi la Polisi la nchini Kenya amekaririwa akisema kuwa, wao wesha memrejesha bwana huyu nchini Tanzania alikotokea ili apate kurudia njia yake aliyoijia hadi huko alikotokea awali. Askari wa Tanzania nao kwa upande wao wanaruka na kusema kuwa hawana taarifa zozote kumhusu , wanasisitiza, hayupo nchini.

Hii ndiyo nayoiita kidali po, na ninadhani si nzuri hata kidogo kwetu sisi wananchi na hasa wafanyabiashara wanaoleta ama kupeleka bidhaa nchi za ng'ambo. Hivi ilivyo tu tayari ni vigumu kupata vibali vya ruhusa ya kusafiria nchi za mbali. Mtu unanyimwa viza bila  hata ya kuwa na hatia yoyote, seuze tutakapounganishwa katika orodha ya nchi zinazosaidia au kushirikiana na magaidi?

Tafadhali, tusijefikishwa huko kubaya wafanyabiashara wetu wakashindwa kusafiri nchi za ng'ambo. Tutaendelea kubaki kuwa Taifa la wapokea vya nje tu, na inafahamika vyema kuwa nchi yoyote inayopokea zaidi ya kutoa kibiashara, uchumi wake huzorota marafudu.

Chondechonde jama, mtoeni huyu bwana arudi zake kwao huko alikotoka asijetusababishia mabalaa zaidi ya tuliyonayo.

Habari zaidi zisome katika: BBC na FOX News
 


Comments

06/01/2010 15:07

Kwa kweli wamtoe, hatutaki matatizo ya kujitakia siye!!

Reply



Leave a Reply