Nakumbuka ni jana tu hapa niliandika habari ya 'penye miti hakuna wajenzi' kuhusiana na Waingereza kuchukua hatua ya kutufundisha michezo yetu wenyewe ili kutusaidia kuiweka katika hadhi na ngazi ya Kimataifa zaidi. Leo nimesoma habari katika tovuti ya BBC inayohusu jirani zetu wa Kenya kuwa wamechukua michoro ya tingatinga na kiweka katika kiwango cha zaidi ya mchoro tu. ![]() bofya picha kutizama video Hivi sasa wenzetu hao si kuwa wanachora kwa ajili ya kuuza na kujipatia kipato, bali wanaitengenezea michezo ya katuni zinazoonekana katika runinga. Wamepiga hatua na kuwakilisha kazi zao katika mashirika makubwa ya utangazaji na sanaa hii kama vile shirika la Taifa la Utangazaji la nchini Uingereza (BBC) na kampuni kongwe katika sanaa ya katuni ya Disney. Hatua waliyoipiga si ndogo kwani yahitaji utaalamu na umakinifu katika uchoraji na utengenezaji picha kuwa katika uhalisia. Nilichojiuliza ni, ikiwa majirani zetu hawa wameona na wamejaribu na wanaweza, je! sisi tulio asili na chimbuko la michoro ya Tinga Tinga, chatushindani? Ama kweli penye miti wajenzi hamna'ga. Ndiyo yale yale, Mlima Kilimanjaro upo Tanzania, wanaofaidi Wakenya, siye tuendelee kulalamika, 'oh ni wetu, ni wetu', 'waongo, waongo'. Sawa ni wetu, halafu? Yaani ukisha kuwa wenu ndo' basi yatosha? Comments Comments are closed. |