Katika hali ya kukidhi mahitaji ya kila siku kwa kujipatia ujira kwa njia isiyokiuka sheria za maeneo na nchi, katika miji mikubwa nchini Tanzania si jambo la ajabu kuwaona baadhi ya wananchi wakiwa wamebeba mafurushi makubwa ya viroba vya salfeti vilivyojaa chupa za plastiki walizookoteza huku na huko. Chupa hizi aghalabu huwa zinakuwa zimemaliza matumizi yake ya kuhifadhia maji au vinywaji vingine. Watu hawa wamekuwa wakitembea umbali mrefu, wengi wao wakistahimili makali ya jua na joto kali na vumbi na nyakati nyingine wakivumilia mvua na tope. Chupa hizi hupelekwa katika dampo ambalo wahusika hutoa ujira kulingana na makubaliano ya uzito au ujazo wa bidhaa.
Kutokana na matumizi ya chupa hizi kushamiri katika nchi nyingi duniani, baadhi ya wananchi wa nchi fulani wamebuni matumizi ya chupa hizi kuwa nakshi na urembo katika ujenzi wa nyumba zao. Zifuatazo ni picha zinazoonesha matumizi ya chupa hizo katika kutia urembo katika ujenzi.
(bofya bicha ili kuikuza kwa muonekano mzuri zaidi).