Wauguzi wapata watetezi bungeni - Majira 28/01/2010
Tumaini Makene analiripotia gazeti la Majira kuwa: MUSWADA wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2009, umedaiwa kushindwa kugusa maslahi wala kuonesha thamani ya wauguzi hasa kwa kuangalia kazi ngumu na mzigo mkubwa walionao na mazingira magumu na hatarishi wanayofanyia kazi. Hayo yalidhihirika jana katika Kikao cha Pili cha Mkutano wa 18 wa Bunge, ambapo wengi waliochangia walikuwa wakitilia mkazo suala la maslahi ya wafanyakazi waliko katika sekta hiyo nchini. Kutokana na michango ya wabunge hao, serikali imeshauriwa kuhakikisha kuwa mswada huo unawathamini wakunga na wauguzi nchini, walioko katika sekta ya umma na binafsi, kwa kuongeza mishahara yao, kuwapatia posho za mazingira magumu ya kazi na posho za kufanya kazi hatarishi. Akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni juu ya muswada huo, Msemaji Mkuu wa kambi hiyo katika masuala ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Ali Tarab Ali alisema kuwa, muswada huo hauoneshi kifungu chochote ambacho kinatoa motisha kwa Wauguzi na Wakunga katika utendaji kazi wao. "Hali halisi ya tasnia ya afya inaendeshwa na fani ya uuguzi na ukunga, lakini jambo ambalo mpaka sasa Serikali bado haijaligundua au imeligundua lakini inashindwa kulitekeleza ni mazingira ya kazi na maslahi duni kwa wanataaluma wa fani hii. Jambo hili limekuwa ndicho kikwazo kikubwa cha adui namba mbili wa nchi hii (maradhi) anaondoka. "Mh. Naibu Spika muswada huu hauoneshi kifungu chochote ambacho kinatoa motisha kwa Wauguzi na Wakunga badala yake umesheheni vifungu vya kuwadhibiti Wauguzi na Wakunga katika utendaji kazi wao. Kambi ya upinzani inaona pamoja na nia nzuri ya Serikali tunayoambiwa, lakini jambo hili litazidisha uhaba na upungufu wa wataalamu katika fani hii, jambo ambalo ni hatari katika mustakabali wa nchi yetu, kumbuka kuwa hata kama tutakuwa na madaktari wengi kiasi gani bila Wauguzi bado hatujafanya kitu," alisema Bw. Tarab. Akichangia muswada huo ambao uliwasilishwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Bi. Aisha Kigoda, Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Bw. Ibrahim Muhammad Mnyaa alisema kuwa muswada huo badala ya kuonesha kuwajali watu wanaofanya kazi ngumu za Uuguzi na Ukunga na kuthamini kazi zao, umejaa vitisho vya adhabu na kuwaonya katika jambo moja na jingine. "Mswada haungalii thamani ya Wauguzi, hakuna priviledges zozote, unaongelea adhabu tu, hakuna risk allowance, hakuna hardships allowances, watu hawa hawalipwi mafao kulingana kwa mujibu wa taaluma, hii siyo sawa, maana kama wachache tulionao hatuwaridhishi halafu wakati huo huo tunaambiwa kuwa kuna maombi mengi yanawahitaji kutoka nje sijui tunafanya nini," alisema Bw. Mnyaa. Hali hiyo pia iliwagusa Wabunge wengine waliochangia mswada huo wakitanguliwa na Profesa Idrisa Mtulia (Rufiji, CCM), George Lubeleje (Mpwapwa, CCM), Job Ndugai (Kongwa, CCM), Jenista Mhagama (Peramiho, CCM), Anna Lupembe (Viti Maalumu, CCM) na Pindi Chana (Viti Maalumu, CCM). Mapema akiwasilisha muswada huo, Bi. Kigoda alisema kuwa muswada huo umekusudia kutungwa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ambayo itainua na kudhibiti huduma za uuguzi na ukunga. "Kutokana na mtazamo huo, muswada huu unakusudia kuifanya taaluma kutambulika kuwa taaluma muhimu katika jamii ambayo inahitajika kupatiwa nguvu ya kisheria ili kusaidia utekelezaji wa majukumu yake," alisema Bi. Kigoda. CommentsWenger 31/01/2010 11:18pm
Hii nimeipenda na imetulia..Lakini inabidi na wao wainuke na kupiga kelele mpaka wasikilizwe.Wanalaumiwa bila watu kujali maslahi yao..Wito?? eeeeh ndo waonewe?
Reply
Leave a Reply | Vitabu vya WatanzaniaBofya picha ya kitabu unachokitaka ili ujinunulie nakala
Yaliyomo/CategoriesAll Hifadhi/ArchivesFebruary 2012 |




RSS Feed