Habari hii ni kwa mujibu wa blogu ya Beda Msimbe - Lukwangule

Mwanafunzi wa shule ya Sekondari Uomboni wilayani Moshi vijijini, Festo Kibonda (18), amekufa na wengine ishirin na nne (24) kujeruhiwa katika ajali baada ya basi la Ngorika kuiparamia Hiace(Kipanya) waliyokuwa wakisafiria wanafunzi hao kutoka shuleni.

Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 3.30 asubuhi katika eneo la njia panda ya Himo wilayani humo.

Alisema katika ajali hiyo basi hilo la Ngorika lenye namba za usajili T 154 AHF aina ya Scania lililokuwa likindeshwa na Abbas Maeda likielekea mkoani Tanga ambapo wakati likitokea mizani liliigonga Hiace hiyo yenye namba za usajili T 810 AFK.

“Baada ya ajali wasamamaria wema wakishirikiana na askari wa usalama barabarani waliwakimbiza majeruhi katika hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi lakini, Festo alifariki wakati akipatiwa matibabu”alisema.
Kamanda alisema wakati Ngorika ikitoka eneo la mizani huku dereva wake bila uangalifu aliiparamia Hiace hiyo iliyokuwa imebeba wanafunzi ikitokea shuleni kwao eneo la Marangu Kiraracha Wilayani Moshi vijijini.
“Hii ni ajali mbaya na ilisababishwa na uzembe wa dereva wa Ngorika ambaye hakuwa mwangalifu kwani eneo la mizani ni dogo na halikustahili kwa gari yoyote kutoka kwa kasi… tunamshikilia ili tumfikishe mahakamani hapo badaye” alisema.

Alisema baada ya Ngorika kutoka kwa kasi liliigonga Hiace iyo kwa ubavu na kusababisha mwanafunzi mmoja kufariki huku wengine wakijeruhiwa vibaya ambapo wanafunzi watatu miongoni mwao akiwamo Mwalimu wao hali zao ni mbaya. Aliwataja wanafunzi waliolazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC na hali zao ni mbaya kuwa ni Innocenti Kibonda(18) ambaye ni pacha wa marehemu katika ajali hiyo, Levina Assey (17) na Mwalimu wao Charles Bantalome (26). Alisema majeruhi wengine 21 katika ajali hiyo wamelezwa katika hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi huku ikiripotiwa kuwa hali zao si mbaya na wanaendelea na matibabu.

Hata hivyo dereva wa Hiace aliyejulikana kuwa ni Tumaini Rwaito amelazwa katika hospitali ya Kilema wilayani humo na hali yake inaendelea vizuri.

MAZUNGUMZO BAADA YA HABARI

Kama nilivyoandika jana, narudia kauli hiyo kuwa hakuna jipya la kusema wala kushauri hadi yale yaliyokwisha kusema na kushauriwa yafanyiwe kazi ifahamike kipi kinatekelezeka na kipi hakitekelezeki na tufanye nini.
 


Comments




Leave a Reply