Habari ni kwa mujibu wa blogu ya Beda Msimbe - Lukwangule

Basi la Kampuni ya Summry lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam limepata ajali baada ya kugongwa na lori na kusababisha kifo cha mtu mmoja, huku wengine watano wakijeruhiwa vibaya katika ajali hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Thobias Andengenye amesema ajali hiyo imetokea Machi 29, majira ya saa 12:00 jioni katika eneo la Maseyu kwenye barabara kuu ya kutokea Morogoro kuelekea Dar es salaam. Amesema ajali hiyo inahusisha basi la Kampuni hiyo aina ya Nissan lenye namba za usajili T 842 ASG lililokuwa likiendeshwa na Nyasio George (38) Mkazi wa Mbalizi Mbeya, ambalo liligongana na lori lenye namba za usajili T 288 AWJ lililokuwa na tela lenye namba za usajili T 666 AVR lililokuwa likiendeshwa na Salumu Sekwa ambaye alikimbia mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo.

Aidha alisema katika ajali hiyo mwanamke mmoja aliyekufa ambaye mpaka sasa jina lake halikufahamika anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 16 hadi 18. Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Ester Robart (14), Tumpe Mwakatobe (31) wakazi wa Tabata Dar es Salaam, Eric Emanuel (mwenye umri wa miezi 11), Dorcas David (21) mkazi wa Iyunga Mbeya na Belnard Leonald mwanafunzi wa Kidato cha nne
katika shule ya Sekondari ya Pandaili iliyopo Mkoa wa Mbeya.

MAZUNGUMZO BAADA YA HABARI
Sidhani kama kipo cha kuzungumza kwani kila mara wanablogu na wasomaji wa blogu wameshatoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kupunguza ajali hizi. Sina la ziada kwa sasa kwani yaliyosemwa hakuna aliyeonesha kuyafanyia kazi na kueleza ufanisi ama ugumu katika utekelezaji wake.
 


Comments




Leave a Reply