Kwa heshima zote niliomba ruhusa ya Dk. Mghanga ili niweze kusambaza kumbukumbu yake kuhusu tanzaia ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania hayati, ndugu Edward Moringe Sokoine (pichani) aliyefariki kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Dumila mkoani Morogoro nchini Tanzania, alipokuwa anatoka katika kikao cha Bunge huko Dodoma. Ama kwa hakika kumbukumbu hii imenitoa machozi, hasa si kwa kifo cha Marehemu Sokoine, bali kwa hali halisi ya nchi ilivyo kwa sasa na kufikiri ingekuwaje ikiwa Marehemu Sokoine angekuwa hai na kuongeza nguvu zake katika ushirika wake na marehemu Julius Kambarage Nyerere, Rashid Mfaume Kawawa na viongozi wengine walioshika hatamu ya uongozi nchini Tanzania? Pia nimewakumbuka wengi waliotangulia katika haki, Kwame Nkrumah, Anwar El Sadat, Patrice Lumumba na aliye hai bado Nelson Mandela. Tafadhali shiriki nami kusoma kumbukumbu ya Dk. Mghanga... ![]() Edward Moringe Sokoine (1938 - 1984) Ni miaka ishirini na sita iliyopita. Siku ya Alhamisi, majira ya jioni kama saa kumi na moja. Anga la jiji la Dar es Salaam lilikuwa jeusi likihanikizwa na mawingu madogo madogo yaliyojikusanya kuashiria kamvua kalikokuwa kametawala siku hiyo. Hizi ni nyakati za masika katika sehemu kubwa ya nchi. Ndo kwanza nimerudi toka shule, tayari nimeshajipakia ugali wangu wa njano (Yanga) na maharage ya Iringa. Nipo mtaani nikicheza na wenzangu chandimu. Hatuna viatu, tupo pekupeku lakini hatujali kitu. Maisha yalikuwa mazuri bila kujua adha na masumbufu ambayo wazazi walikuwa wanayapitia ili kutufanya watoto wao tuweze kwenda chooni. Nikiangalia pembeni, akina mama walikuwa wamekaa wakisukana na wengine walikuwa kwenye vibustani vyao wakipalilia matuta ya viazi vitamu. Hakika hatukujua lililokuwa limetokea masaa machache yaliyopita hapa nchini kwetu. Lakini ghafla redio zikaanza kupiga wimbo wa Taifa. Si aghalabu kusikia wimbo wa Taifa mida kama ile tena kipindi kile kisichokuwa na sikukuu wala mgeni yeyote wa kitaifa. Haiyumkiniki kuna jambo kuu limetokea. Katika utoto wangu, ghafla nikaacha kucheza, akina mama waliokuwa wakisogoa nao wakapigwa na ubaridi wa ghafla. Katika mshawasha wangu wa kitoto nikaijongelea redio kutaka kujua kilichojiri jioni hiyo ya Alhamisi nyeusi. Dakika kadhaa zilipita kabla ya wimbo wa taifa kuisha. Sauti iliyojaa huzuni ikasikika. Hata katika utoto wangu, naweza kusema kwa hakika kuwa sauti ile ilikuwa katika huzuni na majonzi na ilionesha ni ya mtu aliyekuwa katika kilio muda si mrefu uliopita. Naam, ilikuwa ni sauti ya hayati baba wa Taifa. Nayakumbuka maneno yake mpaka sasa. Hivi ndivyo alivyosema: "Ndugu wananchi, leo mnamo majira ya saba mchana, ndugu yetu, mwenzetu, Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais, Edward Moringe Sokoine amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea huko Morogoro wakati akilejea Dar es Salaam kutoka Dodoma kwenye mkutano wa Bunge" Naam, hiyo ndiyo sababu ya kupigwa kwa wimbo wa Taifa jioni ile. Utando mweusi ukatanda. Simanzi ikatawala. Vilio vikasikika, furaha ikatoweka. Giza la mawingu meusi likaongezea upotevu wa furaha. Nikausikia ukelele mkuu kutoka kwa mama mmoja aliyekuwa ameshika jembe akipalilia bustani yake "Mama wee mkombozi wetu amekufa, nani atatutetea sisi wanyonge?" Hakika ndivyo aliomboleza mama yule. Huzuni kuu ikaniingia ghafla. Nikajiwazia "Sokoine kafa? Hapana, amekufa?" Nafsi ilikataa kuamini, akili ya utoto ikaniambia haiwezekani. Ghafla machozi yakaanza kunitiririka. Naam nililia. Nilimlilia mzalendo wa kweli. Wazazi walilia, wananchi walilia, hata Nyerere alilia tena hadharani, hakulia kiunafiki alilia kweli. Watanzania wapenda haki tulilia, tulimlilia mpenda haki mwenzetu. Sokione mzalendo wa kweli. Mwana wa Kitanzania asilia, mtetezi wa kweli wa wanyonge, mchapakazi, mpigania mema ya nchi. Naam, yawezekana kwa wengine ameshafutika lakini kwa wapenda haki, Sokoine atabaki kuwa kioo chetu daima. Huyu ndiye mtu aliyekuwa na sifa nilizozitaja wakati ule kwenye ile ndoto yangu ya "Namuona mtu huyu". Yawezekana alikuwa na kasoro zake kama mwanadamu na hata kiutendaji lakini daima nia yake njema kwa watu wake iliyafunika makosa yake hayo. Alipendwa na wanyonge na kuchukiwa na wezi, wabadhiifu wa mali ya umma na wahujumu uchumi (leo tunawaita mafisadi). Huyu ndiye aina ya mtu tuliyemuhitaji Tanzania ya leo. Nimemkumbuka Sokoine, Mtanzania, Mzalendo, Mwana mpenda nchi aliyenifanya nihisi msiba wake kuwa unanihusu kwa ukaribu mno. Naam, wajamaa kama kina Subi lazima watamkumbuka mtu huyu na kumuomboleza daima. Mungu alipenda kumchukua ingawa tuliona amemchukua mapema mno. Pumzika kwa amani Baba Sokoine, Mtanzania na Mzalendo wa kweli. Amina! Dk. F. Mghanga, MD CommentsMonsignor 12/04/2010 12:29pm
Pumzika kwa amani Sokoine. Tunakukumbuka kwa yote uliyotutendea wana wa Tanzania. Leo watu wa kariba yako hawaonekani, na hata wakitaka kuonekana wanakandamizwa ili wasijitokeze. Tuna wapigaporojo na wasanii tu. Tutakukumbuka daima.
Reply
makafu,s.s. 12/04/2010 2:51pm
Sokoine alikuwa mtu wa watu wanyonge,nashangaa viongozi kutokumuenzi hii ni kwa sababu kile alichopigania ni mwiba kwao nafsi zinawasuta.Fisadi tangu lini akamuenzi Sokoine?????????????
Reply
Lulu 12/04/2010 4:56pm
Nimeshangaa kuona magazeti yote kwenye internet hayakughusia hii siku ila Blogs. Tunashukuru wana blog kwa kuwa na kumbukumbu ya kaka yetu.
Reply
Asanteni sana nyote kwa maoni yenu, na zaidi sana Lulu kwa kuona umuhimu wa blogu na tovuti katika kumuenzi kiongozi huyu ambaye mafisadi, wezi na wabadhirifu wa mali ya umma hawataki kusikia lolote kumhusu. Ukweli hautapingika kuwa mbegu aliyoipanda marehemu Edward Moringe Sokoine haitakufa kamwe! Itaoza na kumea na kuchipua tena na tena.
Reply
hans 14/04/2010 1:52am
marehemu Moringe ni mfano bora kabisa wa kuigwa na viongozi wetu wanaotuongoza. mr Moringe alikuwa ni kiongozi hodari sana. upumzike kwa amani!
Reply
Leave a Reply | Vitabu vya WatanzaniaBofya picha ya kitabu unachokitaka ili ujinunulie nakala
Yaliyomo/CategoriesAll Hifadhi/ArchivesFebruary 2012 |





RSS Feed