Habari hii imetoka katika gazeti la HabariLeo

Kitendo cha Kenya kuongoza kampeni ya kupinga Tanzania isiuze meno ya tembo katika mkutano huko mjini Doha, Qatar kimewachefua wabunge wa Tanzania na wameionya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa makini na nchi hiyo na itambue kwamba Kenya si rafiki wa Tanzania.

Wabunge hao pia wamesema adhabu pekee ya kuipa Kenya ni kwa Bunge kukataa kuridhia itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo linashabikiwa na Kenya ambayo inaamini kuwa itafaidika zaidi kuliko nchi zingine mwanachama wa jumuiya hiyo.

Walitoa msimamo huo kwenye semina baada ya Waziri Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Diodorus Kamala kuwasilisha mada yake iliyolenga kueleza maudhui ya itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki.

Itifaki hiyo itawasilishwa bungeni kesho. Katika mada yake, Dk. Kamala aliwaeleza Wabunge jinsi hatua za utekelezaji zitakavyoanza kutekelezwa mara Bunge litakaporidhia itafaki hiyo kesho. Lakini wabunge wengi waliochangia walisema soko la pamoja, Tanzania bado haijawa tayari na iwapo Bunge litaridhia watakaonufaika zaidi ni Kenya.

Mbunge wa Masasi, Raynald Mrope (CCM) alisema suala la soko la pamoja linaonekana linaharakishwa, wakati Kenya ndio wanaoonekana watafaidika zaidi na akasisitiza kuwa Watanzania hawajawa tayari kwa sababu mbalimbali. “Hawa majirani zetu lazima waelewe kuwa ni lazima wawe jirani mwema, hivi karibuni ametukamata vibaya kule Doha wamekataa tusiuze pembe za ndovu zilizojaa kwetu. Huyu sio ndugu yetu, huyu tukimruhusu aje kufanya kazi kwetu haya mambo yatazidi... walichokifanya ni lazima wapate adhabu na ni kutokubali itifaki hii kama wanavyotaka wao,” alisema Mrope.

Mbunge wa Shinyanga Mjini, Dk. Charles Mlingwa (CCM) alipendekeza Tanzania iwe ya mwisho kuridhia itifaki ya soko la pamoja. Alitoa pendekezo hilo kwa kile alichodai kuwa tabia ya nchi hiyo katika mikutano ya kimataifa imekuwa mstari wa mbele kupinga maombi ya Tanzania. Alisema kitendo cha Kenya kuamua kujenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Taveta, lengo lao hasa ni kutaka kuua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Mbunge wa Njombe Magharibi, Yono Kevela (CCM) aliomba wabunge wakatae kuridhia itifaki hiyo kwa maelezo: “Tuachane na soko hili kwa sababu wananchi wetu bado hawajapewa elimu ya kutosha kwa nini tuhangaike nalo. Hii ni kuwatengenezea ulaji watu wa Kenya, hivyo sisi wawakilishi wa wananchi tusiingie kichwakichwa katika kusaini itifaki hii.”

Mbunge wa Lulindi, Suleiman Kumchaya (CCM) alisema Tanzania haiwezi kuwa mgongo wa nchi nyingine kupandia kwenda kwingine. Alisema nchini Doha nchi za Afrika mashariki zingekuwa na kauli moja na hata kuna kitu Tanzania ilikosea Kenya isingesimama kwenye mkutano huo kulisema.

Naye Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM) alisema yeye alikuwapo Doha alishuhudia kwa macho yake namna jirani yetu Kenya analivyoiua Tanzania kwa sumu na akaonya kuwa Bunge linaweza kuridhia leo; lakini vijana hao wakawalaani hadi wanakwenda kaburini.

Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango (CCM) alitaka Tanzania iende pole pole na liletwe bungeni baada miaka mingine 10.“Iandikeni hii tarehe ya leo maana tutakuja kujutia, angalieni ya Doha namna Kenya walivyotufanyia.” Alitaka Tanzania ifanye sensa kujua Wakenya wanaofanya kazi nchini kwani wamejazana kwenye mahoteli ya kitalii ndipo itifaki hiyo iridhiwe. “Nina ushahidi kule kwenye mbuga za wanyama wamejaa wao, warudi kwao kabla ya sisi kufikiria kuridhia.”

Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikiri kuwa ni kweli Wakenya wamejaa hapa nchini na akahoji “Kwa nini Watanzania hawaendi huko kwao? Alihoji na kuwataka Wabunge wawe wazi ili Kenya wapate ujumbe huo kwamba Tanzania imekasirika.
 


Comments




Leave a Reply