Ufisadi nina imani ni hulka au tabia ya mtu ambayo hakuzaliwa nayo, ila amejifunza akiwa anadhamiria au mfumo wa jamii iliyomlea umemlazimisha kujifunza ufisadi bila yeye mwenyewe kujua. Tabia hii wakati mwingine inamfanya yule anayetuhumiwa kutojiona yeye mwenyewe kuwa ni fisadi, bali anawaona wale wanaopambana nao ndio mafisadi.
Hulka hii kwa namna moja au nyingine imelelewa na viongozi wetu, watendaji wa serikali, mifumo ya elimu, familia zetu ambao ni mafisadi bila kujijua au kwa kujijua. Ninasema bila kujijua kwani, shuleni wakati nasoma tulikuwa na miradi ya elimu ya kujitegemea mfano, bustani za mbogamboga, kilimo cha mahindi, n.k, waalimu waliokuwa walezi wa ufisadi waliweZa subiri mazao yakikomaa wanachuma mboga bila kulipa hela na kwenda kula na watoto wao, mwanafunzi aliyetoa jasho kwa kulima na kumwagilia mboga akibeba mbolea ya samadi toka nyumbani aambulii kitu, bali anayefaidi ni mwalimu wake aliyekuwa mnyapala. Kwa mantiki hiyo mwalimu huyu amefanikiwa kumfundisha mwanafunzi huyu kuwa hana haki na kile alichokifanyia kazi, kwa hiyo kesho atakuwa fisadi, Mungu asipoingilia kati.
Katika familia, mama na watoto wanashiriki sana katika shughuli za kilimo na ufagaji, hadi mazao yanakomaa, siku ya siku baada ya kuvuna na kuweka stoo, baba anakuja chini ya kivuli cha mfumo dume(ufisadi) anachukua mazao yale na kuyapeleka sokoni na kuanza kuyatumia kwa anasa, ikiwezekana na vimada au hata kuoa mke wa pili, huku watoto waliozalisha anachokitumia wakibaki wanapiga miayo na mlo wa siku moja. Kwa upande wa wafugaji watoto wanashiriki kuchunga mifugo, wakina mama wakikata nyasi lakini mwisho wa siku baba anapeleka mifugo mnadani, na kwenda kutumbua maraha akiiacha familia ikiishi kwa mlo mmoja usohakika. Nakumbuka sana wakati wa msimu wa mavuno magonvi yaliongezeka sana katika familia, mama kapigwa, mara kapewa talaka n.k.
Viongozi wa kiroho wanaposhindwa kusimamia kweli na kuwakumbatia watu wanaouasi uadilifu wazi wazi ni dalili kuwa hawa viongozi nao si waadilifu. Ni jambo la kawaida kusikia vurugu mbalimbali katikati ya waumini wa dini na madhehebu mbalimbali, ukichunguza kwa umakini sana sahemu kubwa ya mitafaruku hii inasababishwa na u-mimi au kujali maslahi binafsi zaidi kuliko kujali hali ya kondoo. Inapofika mahali pa kugunduana ndipo huunda makundi na hatimaye mitafaruku kutokea, kulinda maslahi au kupokonyana maslahi hayo. Hivi hawa viongozi wa kidini watajivua je lawama za kuwaandalia Watanzania waumini wasiowaadilifu? Nilitegemea siku moja tusikie waumini wa dini fulani chini ya uongozi wao wamemwita mwenzao anayetuhumiwa wakae naye wazungunze kuonesha namna gani anamfedhehesha Mwenyenzi Mungu na jamii ile wanayoshiriki pamoja kumwabudu Mungu. Kama taasisi hizi za kidini hazina zinachowezeza kufanya kuwaokoa watanzania toka kuwa na viongozi wasio waadilifu, basi wingi wa taasisi hizi zitakuwa zimejaa unafiki na ufisadi.
Mwishoni mwa mwaka jana nilipokuwa ziarani Kanda ya Ziwa nilikutana na mzee mmoja maarufau wa chama, katika mazungunzo yetu nilimwuliza swali hili, “ ikiwa Rais wa kwanza wa Tanzania alikuwa mwalimu alishindwa je kuwafundisha wafuasi wake uaadilifu na hatimae wahitimu? Mbona wale wale waliokuwa vijana wa mwalimu na walioaminiwa na Mwalimu ndo wamekuwa mstari wa mbele kupingina na sera za mwalimu za uadilifu? Wanafunzi wake wa kisiasa walihitimu kweli? Yule baba alikaa kimya kwa muda kisha akaniambia “kuna tofauti kubwa kati ya wanafunzi wa darasani na wale wa kisiasa”. Kwa kuwa sikuridhika na majibu yake niliendelea kutafakari, Ufisadi umeanza enzi hizi za awamu ya pili, tatu na nne tu, awamu ya kwanza haikuwa na ufisadi? Nadhani nitakuwa sahihi nikisema ufisadi ulikuwepo, na ndiyo maana hayati Rashid M. Kawawa, Edward M. Sokoine, Mwl. Julius K. Nyerere na wengine wachache walionekana kuwa kioo, wakimaanisha kile walichokisema na wakisema kile walichokimaanisha. Hata kama leo tunasema walishindwa kuwaleta watanzania maisha bora, lakini yale waliyoyafanya yalikuwa na dhamira safi na yakiuadilifu. Kwa mantiki hiyo wakajichanganua miongoni mwa wengine wengi. Kwa mantiki hiyo ufisadi ulikuwepo ila kwa kujifichaficha na kwa unafiki mwingi.
Ushahidi ni jinsi mashirika mengi ya umma yalivyofilisika kutokana na kukosekana kwa uadilifu kwa wale walithaminiwa na Watanzania kuyasimamia, hatma yake ikawa ni kufilisika kwa mashirika hayo. Waliokuwa watoto enzi hizo waliyaona hayo yote wakawa kimya kwani enzi hizo ilikuwa mwiko kuhoji, tofauti na hali ya sasa.
Tatizo ninaloliona sasa ni mtu yeyote mwanye mali nyingi kudhaniwa kuwa fisadi bila hata kujiuliza kwanini? Mali hizi za halali au za kifisadi? Tumebaki kuhitana mafisadi mafisadi lakini bado hatuna suluhisho la tabia hii mbaya kwa Mwenyenzi Mungu na hata mwanadamu yeyote mwenye akili timamu na angalau chembe ndogo ya uadilifu. Hatari kubwa imekuja pale viongozi wa kiroho (mashehe na wachungaji) wameingizwa katika mkumbo huu wa tuhuma. Upande mmoja nilikubaliana na tuhuma juu ya upande huu wa viongozi wa dini, kwani binafsi niliamani ndio waliobaki pekee kusafisha mioyo miovu ya waumini wao, ili wawe waadilifu na wawatumikie watanzania kwa uadilifu, ila dalili inaonekana kama wameshindwa.
Nisiendelee kuwa miongoni mwa watoa tuhuma, lakini tuangalie nini cha kufanya sasa. Pakuazia ni malezi ya watoto wetu kiroho na kiakili. Ni lazima tuangalie utaratibu mzima wa malezi ya watoto wetu ili wasiwe mafisadi, Kwa waalimu wao kiroho na kiakili kuishi uadilifu ili wanapowaelekeza watoto kuwa waadilifu wauone mfano kutoka walezi hawa. Ni lazima wauishi uadilifu, wauseme wazi wazi mbele ya watoto hawa n.k. Leo tukiwa na watoto waadilifu, kesho tutakuwa na vijana waadilifu, na keshokutwa tutakuwa na watu wa umri wa kati ambao ni waadilfu. Swali kubwa ni hili, tutatoa wapi waalimu wa kiroho na kiakili wenye kufundisha uadilifu kwa vitendo? Kama serikali ikishindwa tuanze nyumbani kwetu na kudhamiria wanetu wawe waadilifu, hata kama akikutana na mwalimu asiye mwadilifu, ajitahidi kumtambua na akwepe ushawishi wake wa kutokuwa fisadi.
Nina amini kuwa wewe nawe unasuluhisho mbadala tushirikishane, ili kuona kama tunaweza kupambana na sumu hii ya kukosa uadilifu badala ya kupambana na watu walio matokeo ya tabia hizi. Tutafute mizizi ya ufisadi tuing’oe na tuiteketeze kasha tufute kumbukumbu ya historia yeke.
Nawasilisha
Godleader Shoo
(anwani pepe imehifadhiwa)


RSS Feed