Kundi la majambazi yapatayo kumi na yasiyojulikana ambayo yaliivamia nyumba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Taifa ya Jamii (NSSF), Ramadhan Dau, na kupora kasha la fedha zenye thamani ya mamilioni lilifanikisha azma yao kwa kutoboa ukuta wa uzio wa nyumba hiyo.

Tukio hilo lililothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Elias Kalinga, lilitokea kwenye nyumba hiyo iliyopo Kinondoni eneo la Ada Estate.

Habari ambazo gazeti la MTANZANIA Jumapili imezipata kutoka eneo la tukio, zinasema lilitokea usiku wa manane ambapo majambazi hao waliingia baada ya kutoboa ukuta wa uzio na kisha kuwateka walinzi. Baada ya kufanikiwa kufanya hivyo, waliwalazimisha walinzi kutoa funguo za geti, wakalifungua na kuingiza gari lao ndani. Inadaiwa baada ya hapo walifungua milango ya nyumba na kuanza kupekua vyumbani hadi katika chumba cha Dau walikolikuta kasha hilo, waliloondoka nalo pamoja na nyaraka kadhaa zilizokuwamo.

Wakati tukio hilo linatokea, Dau na familia yake hawakuwamo nyumbani humo.

Majirani wanasema ndani ya nyumba kulikuwamo na kijana mmoja, ambaye alifungwa kamba na kuzibwa mdomo kwa plasta huku akilazimishwa kuonyesha zilipo fedha na nyaraka walizokuwa wakihitaji majambazi hao.
Taarifa ya Kamanda Kalinga kuhusiana na tukio hilo inasema Polisi inawashikilia walinzi wawili kwa ajili ya upelelezi kamili. “Katika hali ya kawaida haiwezekani wawe na silaha halafu watu watoboe ukuta waingie ndani bila ya kudhibitiwa,” alisema Kamanda Kalinga. Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Deus Mtatilo (52) mkazi wa Kinondoni na Yusuph Bakari (56) mkazi wa Ubungo. Walinzi hao ni waajiriwa na NSSF. “Dau na familia yake hawakuwapo, walinzi walikutwa wamefungwa kamba…katika matukio ya uhalifu kama huu zinaweza kufanyika hadaa vilevile,” alisema.

Picha kwa hisani ya blogu ya Sufiani Mafoto
 


Comments

Issah - KIA
20/04/2010 03:13

HE!! Kasha la Mamilioni? iweje ziwe nyumbani? ikiwa hawajakatwa imejulikanaje kuwa kilichoibiwa ni kasha la mamilion!!? Habari haijakamilika hii

Reply



Leave a Reply