Kama ningekuwa Waziri wa Afya... 14/05/2010
Tarehe 13 Mei 2010 niliandika ujumbe kwenye kundi pepe la "Porojo Club" alias "PiCii Family" na haya ndiyo niliyoyasema (imefanyiwa uhakiki kidogo). Kama ningekuwa Waziri wa Afya, nakuapieni leo mbeye yenu na mbele ya Mwenyezi Mungu, ningetoa kozi ya mafunzo maalumu kwa watu maalumu hata ikibidi Mimi kama Waziri kusimamia utenenezwaji na kisha utumiaji wa DDT katika kaya ili kuua mbu. Katika dunia hii huwezi kufanya kazi na hao mabwana wa upebari na ukomunisti ukitarajia wao wana malengo mazuri ya kukuokoa kwa asilimia mia moja. Hivi hamuoni kuwa kwa kuua malaria watakosa soko kubwa sana la dawa na mahali pa kufanyia majaribio ili wapate fedha na utajiri zaidi? Umewahi kuona nchi yoyote iliyoendelea kwa kusikiliza Wamagharibi au Wamashariki kwa yale wanayotuambia tufanye au tusifanye? Siku zote tunajua kuwa ili kupata maendeleo na kufanya kitu cha maana, lazima watu watofautiane, wakosane na hata ikibidi damu imwagike na wengine wafe ili kufikia maamuzi mtu anayoyaona sahihi. Leo hii tunajisifia tulipata uhuru bila kumwaga damu lakini ni uongo mtupu, walikufa mababu zetu, tusipende kudanganyana kwa kuwa ni watu wachache basi tusiwape thamani ya uhai wao waliopoteza, hawakuwa wajinga, na hao waliokufa ndiyo waliochagiza wale waliodai uhuru wetu. Sasa basi nimetoa mfano huo kusema, ingekuwa mimi ni Waziri, basi lawama zote ningezibeba juu yangu lakini DDT ningeisimamia itumike kwa uangalifu ili kuzuia watu kufa na malaria. Watu wangenilaumu sasa na pengine miaka michache ijayo lakini baada ya kuisha malaria wangenikumbuka na kuniweka kwenye kuta zao kama Waziri aliyetoa uhai wake na kukubali kejeli na kifo kwa ajili ya kuokoa wengi. Ningekuwa mpumbavu na mkaidi kwa sasa lakini potelea mbali wanifananishe na madikteta wengine, mimi ninachojua nitakuwa nimeokoa Taifa langu kama wao (Wamagharibi) walivyookoa mataifa yao ndipo wakazuia matumizi ya DDT. Ikumbukwe kuwa matumizi ya DDT hayakatazwi,ila kiasi na aina ya utumiaji wa DDT. Sisi hatuendi kuitumia kwenye mashamba ya chakula, hata kiasi kidogo kitakachotoka majumbani kwa upepo hadi mashambani hakitoshi kudhuru binadamu. Ikumbukwe kuwa mimi ninayeandika nimezaliwa na kukua katika eneo tulilokuwa tunatumia DDT katika kahawa. Wazee walionitangulia hakuwahi hata mmoja kusumbuliwa kwa magonjwa yoyote ya figo au kibofu cha mkojo. Wao walifariki tu kwa uzee au ajali au kisukari nk, na kamwe si matatizo ya figo na kibofu cha mkojo. Mimi nimechunguza afya yangu na sina tatizo lolote la figo au kibofu. Ikiwa malaria inaua mtu mmoja kila baada ya nusu dakika, je si sawa tutumie DDT ambayo itaua watu wachache kwa matatizo wanayoyaita ya figo na kibofu cha mkojo (pengine kutokuua kabisa)? Ndiyo DDT itaua, lakini Malaria inaua zaidi. Tuna wasomi, na akili zetu zinafanya kazi kama wasomi kweli wenye uchungu na wananchi wenzao? Kweli wasomi hawawezi kutumia kiasi kinachokubalika na Shirika la Afya duniani (WHO) kwa uangalifu hadi tusimamiwe na Wamagharibi katika kufanikisha jambo lolote linaloihusu nchi yetu, hasa hili la malaria? Ukowapi ujasiri wetu? Kwani ni lazima watu wote wakubaliane ili jambo litendeke? mbona inahitaji watu wachache tu wenye ujasiri ili kuweza kubadili mwelekeo mzima? Yailai toba, tupoje? Kama ni kufa mbona watu wanakufa tu? sasa tuogope nini kutengwa? Watutenge lakini hatuna malaria! Hiyo siyo bora? Madhara ya malaria ni makubwa. Kwa uchache, ukiumwa malaria huhudhurii kazini, kwa maana hiyo ufanisi unapungua na kipato kinashuka. Mwanafunzi akikosa masomo shauri ya malaria, anahitaji nguvu mara mbili kuweza kuwafikia wenzie kufidia siku alizokosa vipindi, matokeo yake si kufaulu kwa kiwango cha juu. Mkulima akiugua malaria anakosa kwenda shambani na hivyo mazao yanakosa uangalizi unaotakiwa, matokeo yake ni mazao duni au kidogo. Fundi seremala, ushoni, viatu, makenika, msanii, mchezaji, mwanahabari nk wakiugua, maeneo yao ya kazi yanazorota na hivyo kuzorotesha wengine waliomtegemea. Wachilia mbali watu wanaofariki kwa malaria na hivyo kubidi kuwazika, ni muda na gharama vimekwenda na maji zaidi sana, tumezika nguvu kazi. Tufike mahali tuyaone haya kwa ukubwa na jinsi inavyoathiri Taifa. I am sick and tired of all this. Tunahitaji Kim, Mugabe na Ahmedinejad wetu katika hili. Basi mimi ningekuwa Waziri, walahi ningeutoa rehani uhai wangu na ningefurahi kufa au kuachishwa kazi kwa matumizi ya DDT. Hawatanielewa sasa lakini watakuja nielewa baadaye au vizazi vyao vitajanielewa na watanishukuru kwa hilo, that's how great people go down in history - doing the greater good for the majority, giving their lives for others - that's a definition of a hero on my perspective. Huo ndiyo msimamo wangu kama ningekuwa Waziri wa Afya - kama Ninge - Nami si Waziri wa Afya. Laiti ningekuwa. Laiti ningekuwa. Ninge, ninge, ninge... Subi. PS: Nimesema ninajua wapo watakaonipinga, ni sawa, ni uhuru wao, kadiri ile ile niliyotumia uhuru wangu kuyaandika haya. Huu msimamo wangu, sijaubadili tangu mwaka 2007 na wala sina nia ya kufanya hivyo. | Vitabu vya WatanzaniaBofya picha ya kitabu unachokitaka ili ujinunulie nakala
Yaliyomo/CategoriesAll Hifadhi/ArchivesFebruary 2012 |




RSS Feed