Mzee Pwagu amefariki leo Ijumaa, Mei 28, 2010 katika hospitali ya Amana jijini Dar Es Salaam kutokana na kusumbuliwa na kwikwi na hali ya uzee.
Mzee Pwagu alikuwa anakamilisha pacha wake Mzee Pwaguzi katika kipindi cha redio kilichokuwa maafuru sana miaka ya sitini hadi themanini kilichojulikana kwa jina la Pwagu na Pwaguzi.
Kipindi hicho kilikuwa kikirushwa hewani kila siku ya Jumamosi saa kumi na moja na dakika arobaini na tano jioni hadi saa kumi na mbili kamili (11:45 - 12:00) kupitia Redio Tanzania Dar Es Salaam (RTD). Kwa mara ya kwanza kipindi hicho kilianza kusikika mwaka 1966 na kilipendwa kusikilizwa na watu wa rika zote kutokana na kuelimisha na kutoa burudani inayogusa maisha ya kila siku ya Mtanzania, hadi mwaka 1980 kilipokoma.
Marehemu alikuwa akiishi Kigogo Mbuyuni jijini Dar Es Salaam na anatarajiwa kuzikwa kesho.
Apumzike pema Rajab Kibwana Hatia/Mzee Pwagu.
Historia fupi ya Mzee Pwagu
Pwagu alizaliwa mwaka 1923 mjini Tabora na kuanza elimu yake katika shule ya msingi Tabora Town mwaka 1942.
Kabla hajamaliza elimu hiyo ya msingi, Pwagu alihamishiwa jijini Dar es Salaam alikojiunga na shule moja ya seminari iliyokuwa ikifahamika kwa jina UMCA, Minaki. Hata hivyo msanii huyo ambaye anasema uwezo wake katika maigizo aliuanzia akiwa hapo, hakuwahi kumaliza masomo yake hayo baada ya kutakiwa aende Mombasa kujiunga na kozi nyingine.
“Desemba 1942 alikuja Mzungu mmoja aliyeitwa Donald Brown Skout pale shuleni kwetu na kuuliza iwapo yupo anayetaka kumsaidia King George. “Mimi na wenzangu tukawa sehemu ya waliokubali kazi hiyo ya kumsaidia Mfalme huyo aliyekuwa akipigwa na watu mbalimbali akiwemo Adolf Hittler,” anasimulia.
Walipopelekwa Mombasa, Kenya kwenda kujifunza, mafunzo ambayo yaliwachukuwa mwaka mmoja tu na baadaye wakapangiwa kazi. “Mimi nilianza kuingia kwenye meli ya kivita iitwayo H.A. Losaland ambayo ilikuwa ikizunguka takriban bahari yote ya Hindi hadi mwaka 1946,”anazidi kuweka wazi Pwagu.
Mwaka huo wa 1946 alirejea Dar es Salaam na kufanya kazi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kama fundi mchundo, kazi ambayo kwa mujibu wa msanii huyo alitakiwa aiache na wazazi wake kwa maelezo kuwa ilikuwa ni hatarishi kwake.
Mwaka 1948 alipelekwa kwenye meli iliyokuwa ikiitwa ACT na kuwa baharia hadi mwaka 1949.
Mmoja kati ya watoto wake ndiye mama mzazi wa msanii chipukizi Abdul Ahmad Salum maarufu kwa jina la Mr Benny wa Kaole.
Makala kumhusu Mzee Pwagu(Novemba 13, 2009)
NI matumaini yangu kwamba Watanzania wengi watakuwa wanalikumbuka vema jina la Mzee Pwagu. Na watakaoenda mbali zaidi hawatolisahau pia jina pacha na hilo la Pwaguzi.
Walio wengi huthubutu kudhani hivyo kutokana na ukweli kwamba, licha ya kuwa ni miongoni mwa wasanii mahiri wa michezo redioni, lakini pia alikuwa hodari katika kipindi maarufu kilichofahamika kwa jina la Wakati wa Pwagu na Pwaguzi.
Kipindi hicho kilichokuwa kikirushwa hewani kila Jumamosi kuanzia saa 11:45 hadi 12;00 jioni na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) tangu mwaka 1966, kiliweza kukusanya rika zote za wasikilizaji.
Kwa mujibu wa Pwagu, kipindi hicho kiliendelea mpaka mwishoni mwa miaka ya 1980 kilipopotea kabisa, enzi ambazo kulikuwa hakuna utitiri wa vituo vya redio.
Akizungumza nyumbani kwake Kigogo Mbuyuni jijini Dar es Salaam wiki hii, Pwagu ambaye jina lake halisi ni Rajab Kibwana Hatia, anasema lengo kubwa la igizo hilo ilikuwa ni kuonesha umuhimu wa uaminifu katika jamii.
Anasema: “Lengo letu kubwa lilikuwa ni kuionesha jamii kuwa hii ngozi nyeusi ina matatizo katika suala zima la kuaminiana, watu wawili, watatu au zaidi wanaweza kukubaliana jambo katika biashara, lakini ikatokea baadhi yao wakawa si waaminifu”.
Mbali na hilo, anasema kuwa, michezo hiyo pia ilikuwa inalenga kuelimisha jamii juu ya uwepo wa baadhi ya watu wenye mawazo mazuri katika kujitafutia maisha, lakini kwa ukosefu wa elimu ya kutosha pamoja na miundombinu dhaifu, hufanya wakashindwa kufikia malengo.
Mathalani katika michezo ambayo Pwagu anaielezea na inathibitisha hayo ni kuwa walianzisha mradi wa zahanati ya kung’oa meno huku wakiwa hawana mafunzo yoyote ya kazi hiyo ingawa nje ya ofisi yao kulikuwa na bango kubwa likionesha wataalamu wa kung’oa meno wapo hapo.
“Mteja alipofika na mgonjwa wake alipokewa mapokezi na mwenzangu Pwaguzi, baada ya kulipia pesa ya matibabu huja chumbani niliko mimi na kuanza kumng’oa kwa kutumia koleo za mafundi baiskeli,” anasema kwa lafudhi yake ya kisanii.
Ukiachana na mchezo huo, vilevile kwa kushirikiana na mwenzake Ali Said Keto (Pwaguzi) ambaye kwa sasa ni marehemu, walianzisha miradi ya ushonaji, ujenzi wa madaraja (makandarasi), wauzaji nyama, japo walikuwa hawana ofisi mahususi, wakipanga chini hali iliyosababisha wakamatwe kwa kuhatarisha afya za walaji, mafundi rangi na kadhalika.
“Lakini hakuna hata mmoja katika miradi hiyo tuliofanikiwa kuingiza pesa na tukamaliza kwa usalama bila kushtukiwa na wateja.
"Kana kwamba haitoshi mwenzangu aliyekuwa akipokea fedha ninapokutana naye baadaye kuulizia kile kiasi ambacho mteja alitoa, anasema zilishapotea katika purukushani za kukimbia, jambo ambalo lilizidi kuonesha watu weusi tusivyo waaminifu,” anabainisha.
Mwandishi alipotaka kujua kama michezo hiyo ilikuwa ni ubunifu wao ama kulikuwa na mtu nyuma ya pazia aliyekuwa akiwatungia vituko hivyo, msanii huyo mwenye umri wa miaka 86 anasema; “Ki ukweli ni kwamba hakuna mtu aliyekuwa akitutungia michezo, bali ni sisi wenyewe.”
Msanii huyo aliyekuwa akifanya kazi Mamlaka ya Bandari kitengo cha foko kama dereva, aliweza kushirikiana kwa karibu na mwenzake Pwaguzi ambaye alikuwa Ofisa Kamisaa wa Michezo Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuandaa michezo kulingana na jamii ya wakati huo.
Mbali na wasanii hao nyota, wengine walikuwemo kwenye kundi hilo lililokuwa likijulikana kwa jina la Raha Leo Radio Tanzania ni pamoja na kiongozi wake Hamis Tajiri (Janja au Meneja Mikupuo) ambaye ni marehemu.
Wengine ambao kwa mujibu wa Pwagu ni Tunu Mrisho (Mama Haambiliki), Mwanaheri Ng’andu, Justin Kilumbi, Ali Manjunju (Ngosha), Batholomeo Milulu (Masawe) na Ibrahim Raha (Mzee Jongo wakati ambapo Fundi Said Kipara, baadhi wapo hai na wengine wamefariki dunia.
Pwagu aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa kundi la Sanaa la Kaole lenye makao yake Dar es Salaam, amesema anasononeshwa sana na hatua ya baadhi ya wasanii kukiuka maadili ya utamaduni wetu wakati wakifanya shughuli zao.
“Haiwezekani msanii wa kiume awe jukwaani akionekana kama vile mtoto wa kike, kwa vyovyote vile hii haikubaliki katika jamii inayothamini utu na maadili,” alieleza.
Bila kutaja majina ya wasanii wenye mwenendo huo, Pwagu alitumia muda mrefu kulaani kitendo hicho ambacho alidai kwa sasa kinaonekana kama jambo la kawaida na ni cha kistaarabu kwa wasanii huku akisisitiza kuwa kinapingana hata na mafundisho ya dini.
“Kwanza kimavazi wanaacha kabisa maadili ya Kitanzania, wanapenda sana kuiga mavazi ya kimagharibi na haya sio mavazi mazuri,” anasema.
Akitoa nasaha zake kwa wasanii chipukizi, Pwagu amewataka warudi nyuma kuangalia wapi walikotoka na walifanya nini kipindi hicho, na hivi sasa wako wapi.
Akienda mbele zaidi, Pwagu anakusudia kulifikisha kwenye Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA ), suala la ukiukwaji maadili kunakofanywa na baadhi ya wasanii, ambao amedai wapo mpaka wanaume wanaosuka nywele pamoja na kuvaa shanga na vidani.
“Hawa wakuu wa BASATA wawe wanatembelea kila kikundi kuondoa kitendo hicho kwa kuwa haivumiliki watu wachache waachwe wakiuchafua utamaduni wetu na wao wakitazama tu,” anasema huku uso wake ukiwa umebadilika.
Anamuomba Ofisa anayeshughulikia vikundi vya sanaa BASATA kuongeza juhudi katika kushughulikia suala hilo.
Ingawa msanii huyo hivi sasa ni mgonjwa kama, ambapo mwandishi wa makala haya alimkuta amelala chumbani kwake, amesema bado anaendelea kushiriki kwenye michezo anapohitajika kutengeneza filamu.
“Hivi karibuni nimecheza mchezo unaoitwa Bint Kimanzi na kundi la Dhahabu Halisi la Keko kama baba yake Anthony,” anaeleza.
Katika hatua nyingine, msanii huyo aliutolea uvivu uongozi wa iliyokuwa RTD ambayo sasa ni TBC Taifa, kwa kile alichodai kuwatupa wasanii hao wakongwe licha ya kuwa mchango wao mkubwa ulikiwezesha kituo hicho cha redio kuwa juu.
Anasema awali walipewa ofa ya kutangaziwa vifo vinapotokea kwa watu wa karibu yao, lakini hivi sasa kitu cha namna hiyo kimeondolewa kabisa kwao.
“Sisi tuliambiwa kuwa, tutapewa ofa ya kutangaziwa bure matangazo ya vifo, na kweli utaratibu huo ulikuwepo huko nyuma. Cha ajabu hivi sasa haupo,” anasema. Pwagu ambaye sasa ni mshauri mkuu wa Kaole, alizaliwa mwaka 1923 mjini Tabora na kuanza elimu yake katika shule ya msingi Tabora Town mwaka 1942.
Kabla hajamaliza elimu hiyo ya msingi, Pwagu alihamishiwa jijini Dar es Salaam alikojiunga na shule moja ya seminari iliyokuwa ikifahamika kwa jina UMCA, Minaki.
Hata hivyo msanii huyo ambaye anasema uwezo wake katika maigizo aliuanzia akiwa hapo, hakuwahi kumaliza masomo yake hayo baada ya kutakiwa aende Mombasa kujiunga na kozi nyingine.
“Desemba 1942 alikuja Mzungu mmoja aliyeitwa Donald Brown Skout pale shuleni kwetu na kuuliza iwapo yupo anayetaka kumsaidia King George.
“Mimi na wenzangu tukawa sehemu ya waliokubali kazi hiyo ya kumsaidia Mfalme huyo aliyekuwa akipigwa na watu mbalimbali akiwemo Adolf Hittler,” anasimulia.
Anasema ndipo walipopelekwa Mombasa, Kenya kwenda kujifunza, mafunzo ambayo yaliwachukuwa mwaka mmoja tu na baadaye wakapangiwa kazi.
“Mimi nilianza kuingia kwenye meli ya kivita iitwayo H.A. Losaland ambayo ilikuwa ikizunguka takriban bahari yote ya Hindi hadi mwaka 1946,”anazidi kuweka wazi Pwagu.
Mwaka huo wa 1946 anasema alirejea Dar es Salaam na kufanya kazi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kama fundi mchundo, kazi ambayo kwa mujibu wa msanii huyo alitakiwa aiache na wazazi wake kwa maelezo kuwa ilikuwa ni hatarishi kwake.
Msanii huyo ambaye hata hivyo aliingia tena majini mwaka 1948, ambapo alipelekwa kwenye meli iliyokuwa ikiitwa ACT na kuwa baharia hadi mwaka 1949.
Ana mke na watoto wawili. Mmoja kati ya watoto wake ndiye mama mzazi wa msanii chipukizi Abdul Ahmad Salum maarufu kwa jina la Mr Benny wa Kaole.
Credits: Makala - Rashid Mtagalukai/HabariLeo | Audio - KBH/EastAfricanTube | Picha - Vincent Kigosi/Ray



RSS Feed