Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Meja Jenerali mstaafu Said Said Kalembo amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tanga Majuto Mbuguyu kufuatia ukengeufu katika ukarabati wa barabara Bombo, Tanga.
Picture
Mej. Jen. Said S. Kalembo (picha ya maktaba)
Meja Jenarali Kalembo amemsimamisha kazi Mkurugenzi huyo kutokana na kukiuka agizo la Bodi ya barabara ya Mkoa iliyomtaka kusimamisha marakoja kazi ya ukarabati huo wa barabara katika eneo la Mkonge - Raskazoni kwa kiwango cha lami.

Kazi hiyo ya ukarabati wa Barabara yenye urefu wa kilometa mbili na nusu, hadi kukamilika ilitarajiwa kugharimu  zaidi ya shilingi milioni 575.

Taarifa za mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo unamuelekeza Mkandarasi huyo kukwangua tabaka la juu na kisha kushindilia kabla ya kuweka lami jambo ambalo hata hivyo limefanyika kinyume kwa kuchimbua mawe yote na kuweka kokoto.

"Tofauti na mkataba unavyosema na hata maagizo ya Bodi ya Barabara, mkandarasi ameendelea kuchimba barabara na kutoa mawe, hii ni dharau kubwa", alisema Kalembo.

Kalembo pia aliwaweka mahabusu kwenye Kituo cha Polisi Chumbageni Tanga, mkandarasi wa kampuni inayojenga barabara hiyo  Ediya Mwalusya, Mavumira Bori, Dereva wa trekta Ayub Yakub pamoja na Mhandisi wa Barabara wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Arafat Kaniki waliokutwa wakisimamia kazi  katika eneo la Barabara hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa aliyekuwa ameongozana na Katibu Tawala mkoa wa Tanga, Paul Chikira na Mkuu wa wilaya ya Tanga Dk. Ibrahimu Msengi aliamua kufanya ziara ya ghafla kwenye eneo hilo baada ya kubaini kuwa agizo lililotolewa na Bodi ya Barabara mapema mwezi Mei mwaka huu limekiukwa.

"Hivi inakuaje agizo litolewe na Bodi ya Barabara ya mkoa ambayo Mwenyekiti wake ni Mimi mwenyewe Mkuu wa mkoa likiukwe, yaani mpaka leo mnaendelea kuchimba hivi mnadhani sisi wote hatujasoma eeeh...?", RAS andika barua DED namsimamisha kazi kuanzia leo.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa, Ofisi yake iliandika barua ya kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji kusimamisha kazi hiyo mara moja.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Majuto Mbuguyu alisema kuwa alitoa taarifa za mdomo kwa mkandarasi huyo na kwamba hata yeye haelewi sababu za mkandarasi kutotii maagizo ya bodi na kuendelea na kazi. "Mimi nilimwambia kwa mdomo tu tena niliongea na yule mkurugenzi na walisimama, lakini, nashangaa kwa nini wameendelea kuchimba Barabara, hata mimi Mheshimiwa sielewi?", alisema Mbuguyu.

Hivi karibuni katika kikao cha Bodi ya Barabara, Kalembo alimsimamisha kazi na kumfukuza kwenye kikao Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Rickson Lema kwa madai ya kushindwa kutoa maelezo ya kitaalamu kuhusiana na ujenzi wa Barabara hiyo.

Mawe yaliyokuwa yakiendelea kutolewa katika Barabara hiyo yameanza kuibwa na watu wasiojulikana.

credit: Mwananchi

 


Comments

kilimasera
01/06/2010 02:21

Nampa 5 mzee kalembo ndicho wakuu wetu wa mikoa na wilaya wanachotakiwa kukifanya yaani umefanya jambo moja kubwa sana ambalo viongozi wetu wengi huwa hawawezi kufanya nakumbuka mzee kalembo ulikuwa mkoa wa Ruvuma ukaleta maendeleo makubwa sana pale then ukaenda mkoa wa morogoro nako ukaleta maendeleo makubwa na sasa Tanga kwakweli nikiambiwa nichague wakuu wa mikoa wachapa kazi wakwanza utakuwa ni wewe kwasababu toka nilipoanza kukujua niligundua kuwa ni mtu usiependa ujinga,kuleana wala kuogopana unachopenda wewe ni kwamba kazi ifanyike big up mzee kalembo nakuombea uendelee hivyohivyo!mungu akulinde!

Reply
shaibu
01/06/2010 03:04

MajorGen. Mstaafu kitu ulichofanya ni kizuri maana nchi hii watu hawana huruma kabisa na pesa za wananchi kwa kutofanya miundo mbinu vizuri ili kila mwaka wafanye ufisadi tu kila la Kheri.

Reply



Leave a Reply