Hatua hiyo inafuatia Serikali kushindwa kutoa tamko la makubaliano yao ya kikao cha tatu kilichofanyika Mei 8 mwaka huu, ambapo kwa mujibu wa sheria, Waziri wa Kazi-Ajira na Maendeleo ya Vijana, anapaswa kutoa taarifa ya kikao hicho ndani ya siku 21.
Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholas Mgaya amesema kutokana na Serikali kushindwa kutoa taarifa yoyote ndani ya siku hizo, baraza linaloratibu mgomo litatoa tamko lake. Wafanyakazi wamekuwa kimya kutokana na kusubiri tamko la Serikali kuhusiana na kikao chao hicho, ambapo mpaka sasa Waziri ameshindwa kutoa taarifa yoyote kutokana na hali hiyo watakaa kikao hicho kwa ajili ya kujadili hatua zitakazofuatwa na wafanyakazi hao. "Tunatarajia kufanya kikao cha mwisho siku ya Ijumaa, ambacho kitatoa mwelekeo wa wafanyakazi kufanya mgomo au la, kwa sababu tulikuwa tunasubiri tamko la makubaliano kutoka Serikalini, lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika badala yake waziri amekaa kimya,"alisema Mgaya.
Aliongeza kutokana na hali hiyo baraza hilo limesikitishwa na hatua hiyo, kwa sasa wanaendelea na mikutano ya ndani kwa ajili ya kupanga utaratibu watakaotumia wakati wa kutoa tamko hilo. "Wafanyakazi ndio wanaokuza uchumi wananchi, lakini wanarudishwa nyuma na baadhi ya viongozi kwa kuwadharau na kutosikiliza matatizo yao, jambo ambalo linawafanya waingie kwenye mgogoro mkubwa namna hii na serikali," anaongeza.
Kwa mujibu wa Mgaya, mbali na tamko hilo pia, siku hiyo hiyo shirikisho hilo litatoa taarifa za kutaka kumshitaki Waziri huyo kutokana na kutangaza mishahara yenye mapungufu katika baadhi ya vipengele.
credit: Patricia Kimelemeta/Mwananchi


RSS Feed