Vijana, Kwanini hatushiriki kupiga kura? 15/05/2010
Dakika kadhaa zilizopita nilikuwa nikitazama ukurasa wangu wa facebook. Nilishtuka sana baada ya kusoma maoni ya mmojawapo wa marafiki zangu. Sikuamini alichoandika ilibidi nikirudie mara mbili mbili kujiaminisha ndicho. Kifupi alikuwa anamueleza rafiki yetu mwingine kuwa yeye hajajiandikisha kupiga kura na wala hana mpango wa kwenda kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Nilishtuka sana kwa sababu kuu mbili. Kwanza sikutegemea uamuzi kama ule utoke kwa kijana msomi kama yeye. Lakini pia sikutarajia uamuzi kama ule utolewe na kijana anayelilia mabadiliko katika nchi yake. Nilishindwa kujizuia, nikaamua kumuuliza kujiaminisha kuwa asemacho ndicho, na ndivyo alivyokiri kwa hakika kabisa kuwa hatapiga kura. Sababu kuu zikiwa haoni ni kwanini apoteze muda wake kupiga kura wakati anadhani hakutakuwa na mabadiliko yeyote na hivi kupiga au kutokupiga kwake kura hakutaleta tofauti yeyote. Lakini jingine lililomfanya afikie uamuzi huu ni kuwa hotuba ya mheshimiwa Rais ambayo kwake anasema ilimkatisha tamaa na hakuona umuhimu wa kupiga kura tena. Uamuzi wake huu bila shaka unaakisi kelele za muda mrefu kuhusu ushiriki wa vijana katika uchaguzi wa viongozi wa Taifa letu. Ni mara kadhaa tumesikia watu ama makundi ya watu wakisisitiza kuhusu umuhimu wa vijana kushiriki katika kupiga kura ama hata kugombea uongozi. Wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995, mgombea mmoja wa urais kwa chama cha upinzani alidanganywa na idadi kubwa ya vijana waliokuwa wakijitokeza kwenye mikutano yake ya kampeni. Kundi hilohilo pia lilikuwa likijitokeza katika kulisukuma gari lake na kumshangilia, lakini ambacho mgombea yule hakuelewa ni kuwa vijana wale wala hawakuwa wamejiandikisha kupiga kura wala hawakupiga kura. Na hivi hata idadi ya kura zake haikuwa kama alivyotarajia. Hapo utaona kuwa kumbe vijana wale walitamani mabadiliko lakini walitaka mabadiliko hayo yaletwe na nani na kwa njia gani kama si wao kujiandikisha na kupiga kura? Swali la kujiuliza hivi ni kwanini vijana hawapendi ama hawataki kujihusisha katika kuchagua au kuchaguliwa? Inawezekana kukawa na majibu mengi kwa kila mmoja wetu, lakini je hayo majibu yanatosheleza sababu za kutokutumia haki yako ya kikatiba ya kuchagua au kuchaguliwa? Ifahamike kwamba katika kufanya mabadiliko kuna kadhaa lakini zilizo kuu ni mbili, ama za kutumia demokrasia au kutumia mabavu katika kuuondosha au kuubadilisha uongozi uliopo. Na katika nchi inayojidai inajiendesha kidemokrasia hili la kwanza ndilo linalotumika. Sasa inapotokea kuwa kundi kubwa zaidi katika jamii ambalo ndilo kwa namna moja ama nyingine litaathirika na maamuzi yatakayofanywa na kundi dogo halitaki kutumia fursa yake katika kufanya maamuzi, hali hiyo si ya kufurahisha hata kidogo. Vijana wa Tanzania ambao ndo wazalishaji na wajenga nchi wakuu, wana kila sababu ya kuhitaji mabadiliko. Wana kila sababu ya kuhitaji maendeleo yanayoendana na umri wa nchi yetu, wana kila sababu ya kuhitaji hali bora kwa ajili yao na wazee wao pamoja na wadogo na watoto wao. Lakini kwa vile mabadiliko hayaji kwa kusubiri mwingine akae kukufanyia maamuzi, ni jukumu letu vijana kuhakikisha tunashiriki katika kuleta mabadiliko haya, ama kwa kupigiwa au kwa kupiga kura. Vijana tunapolalamika kuwa kiongozi fulani hafai kwa sababu hafanyi hivi au hivi au tunataka hiki na hiki na yeye hakitimizi wakati hatukupiga kura kumkataa tutakuwa hatujitendei haki sisi wenyewe na wala hatuwatendei haki wenzetu. Kupewa nafasi uifanyie kazi halafu huifanyii, lolote baya likitokea basi nawe pia unahusika katika kutokea kwake na hivi huna haki ya kulalamika. Kwa hivi vijana, sisi ambao tunafanya kundi kubwa la jamii ya watanzania tutumie nafasi yetu tuliyonayo katika kupiga kura kuwakataa wagombea wote ambao tutaona hawafai na wale ambao wana uwezo wa uongozi tuchukue nafasi hii kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwa manufaa ya Taifa letu. Taifa linahitaji mawazo mapya, taifa linahitaji sura mpya, taifa linahitaji nguvu mpya. Lakini hivyo vyote vitatoka wapi kama sisi vijana tutakaa kuachia wengine watupigie kura na kutuchagulia watu walewale, wenye sura zilezile, wenye muono uleule, wenye mawazo yaleyale ya kichovu yasioendana na mabadiliko ya ulimwengu kwa sasa. Kijana fahamu kuwa usipopiga kura umeisaliti nafsi yako, umetusaliti vijana wenzako wenye kutaka mabadiliko ya maendeleo ya kwenda mbele (maana kuna mabadiliko ya mendeleo ya kurudi nyuma pia), umewasaliti wadogo zako wanaokutegemea na umewasaliti watoto wako ambao kesho watakuuliza mama au baba ulikuwa na nafasi ya kuleta mabadiliko kwa kupiga au kupigiwa kura lakini hukutimiza wajibu wako. Na hapo sijui utajitetea nini. Tanzania yenye mabadiliko inawezekana, acha kulalamika na kulalamikia viongozi wasiofaa, timiza wajibu wako, waondoe madarakani. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu tubariki vijana. Monsignor "Mtaka cha uvunguni, inua kitanda juu" CommentsKhamis 15/05/2010 6:22am
Tatizo ninalo liona ni kuwa vijana wengi tumeona hata nikipiga kura ni sawa na kupoteza muda wangu. Kwanza watu wenyewe wenye uelewa wa kutaka hayo mabadiliko ni wangapi? Halafu tena kuna hili suala la kuibwa kwa kura, kwa hiyo hata nikisema nipige kura naona kura yangu itapotea tu kwa kuibwa.
Reply
Rosiana 15/05/2010 6:40am
Asante Monsignor kwa kuwakumbusha vijana jukumu lao. Natumaini vijana wa nyumbani wataitikia wito huo kwa kuitumia vema haki yao ya kikatiba.
Reply
15/05/2010 1:51pm
Zile kauli zetu za Kijana usilale bado mapambano, ikiwa tutazitumia leo , moja kwa moja tutakuwa tuaakisi machungu yaliyopitiwa na kizazi kilichotutangualia ambacho kimsingi ni rika la wazazi wetu. Sio ajabu wakasema nyimbo na kauli hizo zilifaa zaidi enzi zaona wala sio sasa. Lakini ukweli ni kuwa, bila kauli za kimapinduzi na nyimbo za kuhamasisha umuhimu wa vijana nchini, rika la viongozi hatilatambua uwepo wetu achilia mbali mchango wetu kwenye ustawi wa jamii ya Tanzania.
Reply
crazy town 16/05/2010 1:04am
"Voters decide nothing; people who count votes decide everything." --Joseph Stalin
Reply
Cassian 16/05/2010 7:51am
Crazy Town, from what you have said, looks like you are not in favor of voting. But you dont give the altenative of bringing changes especially in a bankrupt system like ours. The author has proposed two ways, either voting or using force to overthrow the existing system. My concern is, if not by voting , do you think the majority in Tanzania, who finds it hard to strike for the increase in their own salaries,will dare join arms in overthrowing the rotten system? If not, what then is the way forward?
Reply
crazytown 16/05/2010 6:34pm
Lets change our own destiny.First by overhauling educational system,
Reply
Leave a Reply | Vitabu vya WatanzaniaBofya picha ya kitabu unachokitaka ili ujinunulie nakala
Yaliyomo/CategoriesAll Hifadhi/ArchivesFebruary 2012 |





RSS Feed