Picture
Mandhari ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE)
Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) wamegoma kuingia madarasani kwa siku nzima ya leo, Mei 31 wakishinikiza Serikali kuwapa fedha za malazi na chakula kiasi cha shilingi 300,000.

Wanafunzi hao wameeleza kusikitishwa kwao na hatua ya Serikali kuileta timu ta Brazil kuja kucheza na timu ya taifa (Taifa Stars) kwa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 3 huku wanafunzi wa vyuo vikuu wakiendelea kulia njaa kwa kushindwa kupewa fedha zao hizo kama walivyoahidiwa.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana wanafunzi hao walisema kuwa mgomo wao ni mgomo wa amani na hata maandamano yao waliyoyafanya yalikuwa ni ya amani ila wanashangazwa na hatua ya uongozi wa chuo hicho kuwaita askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kuja kuyayawanya waandamanaji chuoni hapo.

Wageni wa mwaka wa kwanza ilipaswa kupewa fedha ya kujikimu kiasi cha shilingi 350,000 pamoja na shilingi 300,000 ambazo wanafunzi wote walipaswa kupewa.

Wakielezea juu ya tukio hilo kwa sharti la kutotaja majina yao wanafunzi hao walisema kuwa mgomo huo ulianza majira ya saa tatu asubuhi kabla ya FFU kufika chuoni hapo majira ya saa 5 asubuhi.

Walisema kuwa kutokana na mgomo huo kutokuwa na vurugu zozote askari hao hawakuweza kufyatua risasi kama ilivyo siku nyingine japo bado waliendelea kupiga kambi katika eneo hilo la chuo ili kupambana na wanafunzi hao iwapo wangefanya vurugu.

Pia wanafunzi hao walihoji sababu ya uongozi wa chuo hicho pamoja na bodi ya mikopo kuendelea kuchelewesha malipo yao pamoja na yale ya mwaka wa kwanza wakati vyuo vingine vya umma wamepewa malipo hayo. Hivyo waliahidi kuendelea na mgomo huo hadi pale watakapotimiziwa madai yao.

Wanafunzi hao pia walieleza kusikitishwa na uongozi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo kwa kujitenga kwao na mgomo huo na kuwa iwapo watatimiziwa madai yao hawapo tayari kuendelea kuongozwa na viongozi hao ambao wapo kwa maslahi ya viongozi wa chuo.

Mkuu wa chuo hicho Profesa Philimon Mushi akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu kuhusiana na mgomo huo alikiri kucheleweshwa kwa wanafunzi hao madai yao na kuahidi kuwa wataanza kulipwa madai yao kuanzia alhamisi wiki hii. Alisema kuwa checki kwa ajili ya malipo hayo imekwisha tolewa na ipo benki kuu kwa ajili ya kumalizia taratibu za mwisho ili wanafunzi hao waweze kuingiziwa fedha zao. Hivyo aliwataka wanafunzi hao kuingia madarasani na kuendelea na masomo kama kawaida wakati mchakato huo ukiendelea.

Kwa upande wake kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa (ACP) Evarist Mangalla alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kuwa hakuna mwanafunzi aliyekamatwa wala hakuna uharibifu wowote uliofanywa na wanafunzi hao.

Credit: Francis Godwin
 


Comments




Leave a Reply