CAJAtz inatambua thamani ya sanaa na Utamaduni wa Taifa hili na inaamini kwamba sehemu kama hizo ndiyo muafaka hasa katika kutangaza shughuli za sanaa na Utamaduni wetu.
Tunaamini pia kwamba katika maonesho hayo ya biashara makampuni na asasi mbalimbali huwatumia wasanii katika kufikisha ujumbe wao kwa watu mbalimbali hasa kwa kuamini katika nguvu ya sanaa. Tunashangaa leo hii kuona BET inawakataza wasanii kutumia fani zao kutoa ujumbe kwa watu licha ya kuwa makampuni na asasi hizo zimetumia pesa kuwakodi wasanii hao.
CAJAtz inaamini kwamba sanaa ni biashara hivyo kwanza ilipaswa kuachwa ili ijitangaze kupitia maonesho hayo. Pia BET inapaswa kufahamu kwamba kwa miaka yote ambayo wameilezeza kuwa na mafanikio makubwa katika maonesho hayo, sanaa hizo na ngoma vilikuwa vinatumika sana katika kusherehesha, kutoa ujumbe na kuelimisha wananchi juu ya mambo mbalimbali ya washiriki.
Kwa kitendo cha kupiga marufuku maonesho ya sanaa, BET imekosa Uzalendo wa utamaduni wetu na pia imebana ajira ya wasanii wengi walikuwa wameajiriwa na makampuni kwa ajili ya kufanya shughuli za maonesho kwenye mabanda yao.
Kwa msingi huo, sisi wadau wa masuala ya sanaa na Utamaduni hapa nchini, CAJAtz, tunalaani vikali zuio hilo ambalo halina tija na limeegemea zaidi ulimbukeni na kasumba ya watu wa kuthamini sanaa za nje na kuwatukuza wageni wachache kwa visingizio visivyo na maana.
Iweje sanaa za Kitanzania iwe kelele na hizo za magharibi iwe burudani?
Tunaiomba Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kulishughulikia suala hili haraka iwezekanavyo. Pia tunomba BET kutafakari upya zuio hilo.
Hassan Bumbuli
Katibu Mkuu CAJAtz



RSS Feed