Banyana Banyana 6 Twiga Stars 0 24/07/2010
Magoli matatu kwa kila kipindi cha mchezo yaliiwezesha timu ya Tafia ya soka ya wanawake ya Afrika Kusini, Banyana Banyana 'kuwadushua' wenzao wa Tanzania, Twiga Stars mabao sita kwa nunge. Mechi hiyo ilichezwa siku ya Jumamosi katika uwanja wa Makhulong, Afrika Kusini mbele ya washabiki wanaozidi elfu tano. Goli la kwanza la Banyana Banyana lilifungwa dakika ya 16 ya mchezo kufuatia shuti refu la Yola Jafta na hivyo kuitikisa ngome ya ulinzi ya Twiga Stars, siri ambayo ilisababisha wapinzani wao washambulie zaidi ambapo dakika kumi na tatu baadaye, mchezaji Smeda aliandika bao la pili. Wakati Twiga wakitafakari imekuwaje bao hilo kuingia, dakika baadaye, yaani dakika ya 39 ya mchezo, Smeda alitundika kimyani bao la tatu kwa kichwa, bao ambalo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kinakwisha. Baada ya mapumziko, kipindi cha pili kilianza kwa kocha wa Banyana Banyana, Augustine Makalakalane kuwabadili wachezaji watatu ambapo golikipa, mshambuliaji na kiungo walipumzishwa ili kuwapa nafasi chipukizi wengine. Mabadiliko hayo yalizaa matunda dakika ya sitini na tisa ya mchezo ambapo mchezaji mpya Popela alifunga bao la nne. Kocha wa Banyana Banyana alifanya mabadiliko mengine ya kuwatoa wachezaji watatu na kuwaingiza wengine wapya ambapo mmoja kati yao, Nkhumise, hakufanya ajizi kwani alimthibitishia kocha kuwa 'anaweza' kwa kuandika bao la tano. Tanzania nayo ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa wachezaji watatu na kuwaingiza wengine wapya lakini mabadiliko hayo hayakusaidia kupata hata goli la machozi na badala yake mchezaji wa Banyana Banyana, Sikiti, alifunga kitabu cha magoli pale alipoandika bao la sita. Meneja wa timu hiyo Fran-Hilton Smith alisema wamefarijika sana kuifunga Tanzania kwani ni timu yenye rekodi nzuri na ambayo ilifuzu kuingia katika kinyang'anyiro cha African Woman’s Championship. CommentsLeave a Reply | Vitabu vya WatanzaniaBofya picha ya kitabu unachokitaka ili ujinunulie nakala
Yaliyomo/CategoriesAll Hifadhi/ArchivesFebruary 2012 |




RSS Feed