Picture
Wakazi wa Migombani mjini Zanzibar wakiingia kwenye kituo hicho na wengine wakitafuta majina yao kwenye ubao wa matangazo kabla ya kuingia kwenye vyumba vya kupigia kura mchana wa leo.
Wakazi wa Zanzibar wamejitokeza kupiga kura ya maoni juu ya mustakabali wa Zanzibar kuhusu hoja ya kuundwa kwa Serikali ya Umojwa wa Kitaifa kwa wagombea watagawana madaraka baada ya uchaguzi.

Vyama vikuu vya kisiasa nchini Zanzibar, yaani chama kinachotawala sasa, CCM na chama kikuu cha upinzani CUF, vinaunga mkono hoja hiyo kwa kuwa inalenga kumaliza ghasia zinazotokana na hisia za kuonewa, wizi wa kura na kutokukubalianana matokeo zinazojitokeza mara kwa mara baada ya chaguzi kuu kufanyika.

Watu walijitokeza na kupiga kura zao bila bughudha na hakuna visa vya uvunjifu wa amani vilivyoripotiwa tofauti na ilivyotarajiwa kuwa wale wanaopinga hoja hiyo wangezua vurugu.

Ikiwa wengi watapiga kura ya NDIYO, basi Zanzibar itaingia katika mfumo mpya wa Serikali ambao utakuwa na Rais na makamu Wawili wa Raisi. Makamu wa kwanza atatoka katika chama kitakachonyakua nafasi ya pili katika uchaguzi il hali yule wa pili atatoka katika chama kilichopata ushindi wa kumtoa Raisi wa nchi. Baraza la Wawakilishi nalo litabadilika katika mfumo huu mpya kwa kuwa na uwiano wa madaraka.

Baraza la wawakilishi la sasa litahusika katika kufanya marekebisho ikiwa kura ya NDIYO itashinda.

Tume ya uchaguzi ambayo ndiyo yenye kuratibu kura hiyo inatarajiwa kutoa matokeo hayo ndani ya siku moja baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika. Unaweza kuperuzi tovuti ya tume hiyo kupitia: http://referendum.zec.go.tz
 


Comments




Leave a Reply