Wakala wa barabara nchini (TANROADS) jana ametia saini katika mikataba nane ya ujenzi wa barabara kwa lengo la kuunganisha pwani ya bahari ya Hindi na pwani ya ziwa Tanganyika.
Picture
Meneja Mkuu wa Wakala wa barabara, (TANROADS), Ephraem Mrema (kushoto), mwakilishi Mkuu wa Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Limited, Li Yang na Naibu mwakilishi wa Kampuni hiyo, Liu Xiaobo wakisaini Mkataba wa mradi wa kutengeza barabara yenye urefu wa kilomita 59. 10 kutoka Kyaka, Kagera hadi Bukene. Jumla ya miradi nane yenye Kilomita 525 itakayogharimu Sh Bilioni 593.58 ilisainiwa jijini Dar es Salaam kwa Kampuni tofauti.
Mikataba hiyo ilisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANROADS, Ephraem Mrema na wawakilishi wa makampuni matano ya wakandarasi toka China. Kampuni ya China ya Henan International Cooperation (CHICO) ilisaini mikataba mitatu kati ya minane.

Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo, Mrema alisema barabara hizo zitajengwa kwa kiwango cha lami kwa fedha zinazotokana na mapato ya ndani na jumla ya shilingi bilioni 593.58 zitatumika kukamilisha miradi hiyo ya barabara yenye umbali wa kilomita 525.

“Ujenzi huu utaanza muda wowote kuanzia sasa na kubakiza kilomita 211 tu ambazo hazina lami za barabara kutoka Dar es salaam kupitia Tabora kati ya kilomita 1,253” alisema.
Picture
makabidhiano ya mikataba baada ya kutiwa saini
Mrema alizitaja barabara hizo kuwa ni Tabora hadi Urambo yenye urefu wa kilomita 42, Nyaguge hadi Musoma yenye urefu wa kilomita 85.50 na Kyaka hadi Bugene yenye urefu wa kilomita 59.10 ambazo  zitajengwa na mkandarasi China Henan. 

Barabara ya Manyoni, Itigi hadi Chaya yenye urefu wa kilomita 89.30 na Nzega hadi Tabora yenye urefu wa kilomita 56.10 zitajengwa na kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd pia kutoka china.

Barabara ya Tabora hadi Nyahua yenye kilomita 85 itajengwa na mkandarasi  Chongqing Foreign Trade Economic Cooperation wakati ile ya Nzega hadi Tabora yenye urefu wa kilomita 56.10 itajengwa na China Communications Construction na ile ya Ndono hadi Urambo yenye urefu wa kilomita 51.98 itajengwa na mkandarasi China Civil.

credit: Muhidini Sufiani na Mwananchi

 


Comments




Leave a Reply