Wapinzani kuungana na Ukomavu wa Kisiasa 20/07/2010
Wiki hii limetokea jambo katika anga za siasa ambapo waliokuwa wanachama wa CCJ ambao awali walijitenga na CCM wameamua kujiunga CHADEMA. Hili si jambo geni kwa kuwa tumewaona baadhi ya viongozi wa vyama kadhaa pinzani wakijiunga na hata kuzungumzia tetesi za wao kutaka kuunganisha vyama kabisa. Kwa mtizamo wangu, nadhani hii ni mojawapo ya ukomavu, kukua na kupevuka katika uhuru na demokrasia. Nasema hivi kwani, tangu kuanzishwa kwa demokrasia ya vyama vingi, watu wengi walijiengua toka CCM na kutaka kutumia uhuru uliopatikana kwa kuanzisha vyama. Angalabu, vyama vingi vilianzishwa kwa kuwa baadhi ya watu waliona sera za vyama fulani haziendani na matakwa au sera zao. Vilianzishwa vyama zaidi ya ishirini. Baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, na baada ya kuanguka kwa vyama hivyo katika ngazi za udiwani, ubunge hata uraisi, baadhi ya vyama hivyo vilikufa kifo cha kawaida. Vipo vilivyobaki na vipo vipya vilivyoanzishwa, ama kwa kuungana au kwa kufuta na vya zamani na kuunda vipya kabisa. Hiyo nayo ni hatua katika demokrasia ya kisiasa na matumizi ya uhuru wa kuchagua. Hivi sasa, vyama vya upinzani nchini Tanzania si utitiri mkubwa wa kumchosha mwananchi. Angalao vyama vinavyotoa changamoto vinahesabika kwa vidole vya mkono mmoja. Bado kwa mtizamo wangu, naona hii ni hatua muhimu katika ukomavu wa demokrasia na siasa. Kitendo cha viongozi wa CCJ kujiunga CHADEMA kinamsaidia mwananchi wa kawaida kupunguza utitiri wa idadi ya vyama anavyotakiwa kufahamu na kumwacha na jukumu la kukumbuka wagombea tu. Ikiwa siasa zetu zinaakisi zile za mataifa ya nje, tutakubaliana kuwa katika nchi hizo, mabadiliko yamekuwa yakifanyika ndani ya mpambano wa vyama viwili au vitatu vikuu. Mifano hii ni hai kwa nchi kama vile Uingereza, Marekani, Kenya nk. Nchi hizi zilianzia tulikoanzia sisi kwa kuwa na mlolongo wa vyama, vikapungua na hatimaye kusonga hadi kufika zilipo sasa. Jirani zetu Kenya wameweza kung'oa KANU baada ya kuungana hata ikiwa muunganiko huo ni wa mashaka na wenye mgogoro, bado lengo lao kuu la kuiondoa madarakani KANU lilifanikiwa. Sasa ni kwa namna gani wataitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi katika kujitelea maendeleo, hilo ni suala la wananchi kuuliza na kushinikiza kupata majibu na mwongozo unaofaa. Hivi ndiyo kusema, ninawapongeza kwa dhati kabisa viongozi wa CCJ kwa kitendo chao cha kuhamia CHADEMA na zaidi ya hayo, kuwahimiza wanachama wengine kufanya hivyo. Ni kweli kuwa yawezekana ukawepo msukumo wa ubinafsi au uroho wa madaraka katika kuhama vyama, lakini dhana hii si alama ya chama au watu fulani tu, hii ni hali dhahiri kwa kila chama, kwamba wapo wanachama wenye uroho kila mahali. Hawa ni watu tunaokutana nao na wanaotoka katika jamii tunamoishi. Ikiwa tunawafahamu kwa uthibitisho usiopingika kuwa nia zao ni chafu, basi wananchi ndiyo tulio na uwezo wa kuwakataa kwa njia halali ya kutokuwapa kura zetu za ndiyo. Kuwepo katika chama fulani tu haitoshi kuwa sababu ya kutokuonekana mroho au mbinafsi wa madaraka; hali kadhalika, kuwepo katika chama fulani tu haitoshi kumaanisha kuwa watu wake tayari ni wabinafsi na waroho wa vyeo na madaraka. Aliyesema, Umoja ni nguvu na Utengano ni udhaifu, hakuwa amekosea ijapokuwa wakati mwingine ni vyema na sahihi kabisa kutengana, hii ni kweli inapotokea mtoto anajitenga na familia ili kuanzisha mji au familia yake. Vivyo hiyo katika siasa, uwepo wa vyama zaidi ya kimoja ni muhimu ili kuleta changamoto kila linapoonekana jambo linakwenda kombo. Wakati mwingine inabidi awepo mtu nje ili kuweza kuona jambo kwa mapana na marefu yake, wenyewe wasemaji wa lugha ya Kiingereza wanasema, 'check and balance', yaani lazima wawepo wahakiki na hawa watafanikiwa vyema ikiwa watakuwa nje au kutokufungamana na upande wowote kama yafanyavyo mashirika ya kitaaluma. Natamani kuifikia siku ile ambapo nitaona na kusikia kuwa vyama vikuu vya kisiasa nchini Tanzania ni viwili ama vitatu na pia nafasi ya mgombea huru imethaminishwa. CommentsLeave a Reply | Vitabu vya WatanzaniaBofya picha ya kitabu unachokitaka ili ujinunulie nakala
Yaliyomo/CategoriesAll Hifadhi/ArchivesFebruary 2012 |




RSS Feed