Watu wawili wamethibitika kufa na wengine zaidi 60 kulazwa katika hospitali mbalimbali mjini Tarime mkoani Mara, baada ya kuugua ugonjwa wa kipindupindu. Habari ambazo hazijathibitishwa na wataalamu wa afya zinadai kwamba idadi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa huo mjini Tarime katika kipindi cha wiki moja iliyopita ni zaidi ya watano. Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Dk. Samson Charles, amewataja wakazi wa mjini Tarime waliokufa juzi baada ya kuugua ugonjwa huo kuwa ni Mzee Msabi (zaidi ya miaka 50) na Magesa Rozana aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Nkende. Amesema baadhi ya wagonjwa wameshatibiwa na kuruhusiwa na kwamba waliokuwa wanaendelea kulazwa katika wodi maalumu hospitaini hapo kufikia jana ni 23 wakiwemo wanawake 18 na watoto wawili. Mkuu wa shule ya Sekondari ya Nkende, Mwalimu Michael Ng’wanang’walu, amesema hadi jana wataalamu wa afya walikuwa hawajafika shuleni hapo kuweka dawa ya kutibu maji ya visima kama walivyofanya katika maeneo mengine. Kwa upande wake, Mkuu wa shule ya sekondari ya Tarime, Mwalimu Mutta Jeremiah, amesema shule hiyo ilifungwa Agosti 21, mwaka huu, baada ya wanafunzi tisa kuugua ugonjwa huo na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya kabla ya kuruhusiwa siku tatu baadaye. Naye Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tarime, Mkufunzi Lucas Samuel, amesema wakufunzi na wafanyakazi wengine wameanza kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo baada ya wanachuo wawili kuugua na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya. Changamoto kubwa inayokabili wataalamu wa afya na wakazi wa mji wa Tarime kwa sasa ni namna ya kudhibiti vitendo vya kufua nguo za wagonjwa wa kipindupindu katika mito ya Bomani na Msati, hali inayoweza kueneza zaidi ugonjwa huo. Wakati huo huo, baadhi ya ndugu na jamaa wa wagonjwa wa kipindupindu wamelalamikia vitendo vya kunyimwa na kuuziwa dripu za maji kwa ajili ya wagonjwa wao waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, ambapo Dk. Charles ameahidi kufutilia tuhuma hizo ili wahusika wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria. Hata hivyo, Dk. Charles amesema ofisi yake imenunua maji ya kutosha tofauti na mwanzoni ambapo kulikuwa na upungufu wa dripu za maji hospitalini hapo na hivyo kushindwa kumudu mahitaji ya dripu 24 za maji kwa kila mgonjwa wa kipundupindu. credit: Christopher Gamaina/Radio Free Africa CommentsLeave a Reply | Vitabu vya WatanzaniaBofya picha ya kitabu unachokitaka ili ujinunulie nakala
Yaliyomo/CategoriesAll Hifadhi/ArchivesFebruary 2012 |




RSS Feed