Ridhiwani ambaye ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya baraza kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) Taifa akiwa na viongozi akiwemo aliyekuwa mshindi wa kura za maoni jimbo la Iringa mjini Frederick Mwakalebela na washiriki wengine wa kura za maoni kama Jescar Msambatavangu, walifika katika shule ya msingi Ipogolo wakitaka kukutana na vijana wa eneo hilo ili mjumbe huyo aweze kumuunganisha mgombea ubunge wa jimbo hilo Monica Mbega na Mwakalebela japo mkakati huo uligonga ukuta.
Kabla ya msafara wa Ridhiwani kufika shuleni hapo kwa ajili ya kikao chake cha ndani ya vijana wa CCM kwa lengo la kuvunja makundi ndani ya chama hicho, aliyekuwa mmoja kati ya wana CCM 12 walioingia katika kinyang'anyiro cha ubunge jimbo hilo, Msambatavangu, alipita mitaani kujaribu kuwaomba vijana kwenda kumsikiliza mtoto huyo wa Raisi Kikwete japo waligoma kwa madai kuwa hawadanganyiki na ujio wake.
Hata baada ya vijana hao wa vijiweni kugoma kwenda katika shule hiyo kwa ajili ya kutana na mjumbe huyo kwenye chumba cha darasa la pili katika shule hiyo ya msingi Ipogolo, bado msafara huo ulifika katika eneo hilo kwa ajili ya mkutano japo idadi ya vijana waliokuwa wamefika ilikuwa ni kama vijana 10 pekee.
credit: Francis Godwin
Vyombo mbalimbali vya habari vimesharipoti na kulaani mkanganyo unaofanywa katika kampeni za Kisiasa, ambapo chama kilichoko madarakani kinatumia mwanya huo kushindwa kutofautisha shughuli za Kisiasa za Chama na shughuli za Kiserikali. Magazeti yamesharipoti kuhusu Wafungwa kutumiwa katika ujenzi wa majukwaa ya kisiasa na hivi jana imeripotiwa habari ya Wanyamapori kuwindwa ili kuwapatia kitoweo walioongozana katika shughuli za Kisiasa za Chama, na katika wananchi wakauziwa kitoweo (kuzuga?).
Wanaofanya hivi wanafanya kusudi ili kuonesha kuwa wao ni "mwamba" na hakuna wa kuwafanya lolote?
Wanafanya dharau, au ni kwamba hawafahamu kuwa wanalofanya ni kosa?
Kama si dharau ya umuhimu wa elimu, ni kwa nini mikutano ya kisiasa iendeshwe mashuleni? Juzi tu hapa tumeshangazwa na kitendo cha wanafunzi kutokuingia madarasani, ati wanasubiri msafara wa mgombea uraisi upite? Ama, kwa utaratibu upi jama? Mbona hatuna heshima kwa mambo ya msingi kama elimu?
Mimi kinachonifurahisha ni kwamba, wananchi wameshaona huu sasa ushakuwa ujinga. Hizi ndizo chokochoko zinazoamsha hasira na kusababisha watu watwangane makonde... na zaidi ya hapo. Haya!






RSS Feed