Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) imesema kuanzia wiki ijayo itaanza kupokea awamu ya pili ya maombi ya wanafunzi wanaotaka kujiunga na taasisi za elimu ya juu kupitia mfumo mpya wa udahili wa wanafunzi.

Afisa uhusiano wa TCU, Edward Mkaku alisema kuwa zilikuwepo kasoro nyingi kwenye awamu ya kwanza ya udahili na kusababisha waombaji wengi kukosa nafasi, hivy, baada ya kukamilisha kutoa matokeo ya wanafunzi waliochaguliwa, watafungua tena mitambo ya udahili ili wenye matatizo waombe upya. 

Siwezi kusema utaanza siku gani na kutakuwa na awamu nyingine zaidi kumaliza matatizo yaliyopo - Mkaku. 

  1. Matatizo mengi yaliyotokea yamesababishwa na wanafunzi kutoelewa vyema mfumo, hivyo kufanya maombi yasiyo sahihi. Tatizo la wanafunzi kudahiliwa kwenye kozi ambazo hawakuzichagua limesababishwa na wao wenyewe kutokuwa makini wakati wa kuomba nafasi hizo - Mkaku.
  2. Kwa kuwa kozi ziliwakilishwa na namba za mpangilio (code number), wapo wanafunzi waliochagua namba bila kuangalia inawakilisha kozi gani, matokeo yake wakachagua kozi wasizozitaka.  Yupo mwanafunzi alikuja hapa; yeye amefaulu kwa daraja la kwanza nukta nne kwenye mchepuo wa (historia, kiswali na lugha) HKL, lakini aliomba BS in Engineering, na amedahiliwa kwenye kozi hiyo. Sasa huyu hakuwa makini wakati wa kuchagua kozi - Mkaku. 
  3. Wapo wanafunzi walioomba vyuo kwa kutumia mitandao mingine ya simu za mkononi badala ya VodaCom, hivyo maombi yao hayakufika TCU na hivyo kutochaguliwa - Mkaku.
  4. Kutokana na matatizo hayo, udahili haujaisha. Wanafunzi wasubiri, majina ya wanafunzi waliokosea kwenye maombi ya awali yatatolewa ili waweze kuomba upya. ...na huenda tukafanya uteuzi wa awamu nyingine ili kuhakikisha tunamaliza matatizo yote - Mkaku.

Kwenye ofisi za TCU juzi, wanafunzi wengi walikuwa wakilalamika kutochaguliwa na wengine kuchaguliwa kwenye kozi ambazo hawakuziomba. “Mimi nimetoka Arusha nimekuja hapa kujua hatma yangu, kwa sababu matokeo yangu ya kidato cha sita yalikuwa mazuri tu lakini sikuchaguliwa na rafiki yangu niliyempita, amechaguliwa kwenye kozi kubwa kuliko ufaulu wake,” alisema mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Rahim Bendera. Mmoja alidai amekuta jina lake lakini namba siyo; mwingine alikuta namba yake, ila jina silo.

credit: Hussein Kauli/Mwananchi
 


Comments




Leave a Reply