Tukirejee kisa cha mwanaharakati, marehemu, Ken Saro Wiwa.
Ingawaje kila mtu anayefahamu habari hii anaweza akawa na msimamo wake, na ni sahihi kufanya hivyo kadiri ya maelezo mtu aliyonayo kuhusiana na kisa chenyewe. Binafsi ni miongoni mwa wanaoafiki maelezo yaliyotolewa na kundi la wanaharakati watetea haki za binadamu na mazingira walioainisha kuwa marehemu Saro Wiwa alishitakiwa na hatimaye kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa na mahakama ya kijeshi kwa sababu za "kutilia mchanga kitumbua chao". Tunaamini kuwa Saro Wiwa aliuawa siyo tu "kupunguza usumbufu kwa viongozi waliopoteza utu, bali pia ilikuwa onyo kwa yeyote mwenye kuthubutu kutia mchanga kitumbua cha wakubwa".
Ukweli tunaousimamia ni kuwa, Ken aliuawa kwa kuwa tu "alikula nyamu" kutetea kabila dogo la Waogoni wa Niger Delta na kukemea kwa nguvu zote uharibifu wa mazingira uliokuwa ukifanywa na makampuni yaliyokuwa yakichimba nishati ya mafuta na kuisafisha kisha kujipatia faida kubwa il hali wananchi na eneo zima la Ogoni waliachwa na madhara ya uharibifu mkubwa wa mazingira ambao ulitishia ustawi na uhai wa watu walioishi pale, mazao yao, uoto wa asili na raslimali yao ya mifugo.
Maneno ya mwisho aliyoyatamka Ken kabla ya kunyongwa yalikuwa, “Lord take my soul but the struggle continues.” "Muumba ichukue nafsi yangu ila mapambano yanaendelea" - tafsiri ya Kiswahili kadiri ya uelewa.
Unaweza kutizama video za Ken Saro Wiwa enzi za uhai wake kupitia Youtube.com/user/remembersarowiwa
Turudi kwetu nyumbani Tarime.
Wenyeji wa asili wa maeneo ambako Makampuni yanayochimba dhahabu, almasi, tanzanite na vito vingine vya thamani nchini Tanzania wamekuwa wakilalamika mara kadhaa kutokana na baadhi ya vitendo vya makampuni visivyokubalika katika jamii husika.
Madhara makubwa yatokanayo na machimbo ya madini yamewahi kutokea nchini katika maeneo mbalimbali. Mojawapo ni lile lililotokea mwaka 1996 katika machimbo ya Bulyanhulu na kusababisha, aliyekuwa Mwenyekiti wa TLP ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Vunjo, Augustine Lyatonga Mrema kupiga mbiu kubwa sana na kutaka uchunguzi ufanyike kuhusiana na mauaji hayo. Bofya hapa kusoma taarifa hiyo.
Mwaka jana yupo mwandishi wa habari wa kigeni akishirikiana na raia wanaharakati wa Tanzania alichapisha video iliyoonesha mauaji yalivyofanyika kwa wakazi wa eneo ambalo linaendelea na shughuli za uchimbaji madini hadi leo. Lengo kuu la mauaji hayo lilikuwa ni kuwafurusha wananchi waliogoma kuondoka katika maeneo hayo yenye utajiri, maeneo yao ya asili ambayo walizaliwa na kuishi humo kwa miaka nenda rudi. Kwa bahati mbaya, video ile iliondolewa mtandaoni baada ya vitisho vibaya sana, lakini ipo neema kwenye usemi kuwa "ukweli haufichiki kamwe, ila waweza tu kucheleweshwa kujidhihirisha" kuna wanaharakati wa haki za binadamu na wazalendo waliofanikiwa kupata nakala za video hiyo na kuzisitiri katika maktaba za majumbani mwao. Pengine itachukua muda, lakini ukweli huvumilia hadi unapojidhihirisha.
Mathalan, walioamuru kwenye mtandao kwa video ya mauaji yaliyofanyika huko kanda ya ziwa ili kuwahamisha watu katika makazi yao iondolewe mtandaoni, walisahau kuwa zipo picha mnato ambazo zimezunguka mitandaoni zikidhihirisha kuwa makampuni hayo yamechafua mazingira na uoto wa asilibali pia kusababisha madhara makubwa kwa binadamu ambao ndiyo wenye haki ya msingi ya kufaidika na raslimali mali zilizomo kwenye ardhi yao ya asili. Picha hizo zinaonekana hapo chini na ziliwahi kuchapishwa hapa (bofya kurejea chapisho hilo).
Wakadiriki kuulazimisha umma uamini kuwa madhara hayo hayakutokana na sumu zinazomwagwa na mitambo yao, wakataka wananchi waamini kuwa ni hali iliyojitokeza. Na mtu ujiulize, iweje watu hawa waishi katika maeneo haya kwa karne na miongo kadhaa bila kupatwa na madhara, lakini miaka michache tu baada ya kampuni kuanza shughuli zake, madhara yaanze kuonekana? Watasema ah, wananchi wenyewe walifuata maeneo ambayo hawakupaswa kufuata. Beh! Kwani kampuni ilishindwa vipi kutoa elimu na kuhakikisha uchafu wanaoutoa hauingii karibu na makazi ya watu?
Tuliache hilo.
Tuje kwa watawala wetu.
Inakuwaje vigumu kwa watawala kufahamu kuwa harakati za wananchi za mara kwa mara kupinga na kutaka kuharibu mali za makampuni/wawekezaji, zinatokana na ukweli kwamba wananchi hawaoni faida inayoletwa na uwepo wa makampuni haya, kwa hivyo, wanataka majibu yanayoeleweka?
Kwamba, watawala hawafahamu kuwa wananchi kwa kukosa mbinu za kuwafuata viongozi hao maofisini mwao huko Dar Es Salaam, na kutokana na viongozi kuwaona wananchi kwa nadra, hasa pale inapotokea kutokuelewana au nyakati za uchaguzi tu, na kwa kuwa wananchi hawapati majibu ya kuridhisha kutoka kwenye makampuni husika kwa maelezo kwamba Serikali ndiyo msemaji mkuu, basi, viongozi hawaoni kwamba wananchi wataamua kuwashughulikia wawekezaji hao ili kutuma ujumbe kwa viongozi?
Nadhani viongozi wetu wanayo dhana vichwani mwao kuwa uharamia unaofanywa na baadhi ya Wasomali kuteka meli zilizosheheni mali na watu kisha kudai kiasi kikubwa cha fedha kwa mwenye meli kama fidia kwa matumizi ya maeneo yao ya maji; kwamba hilo halifanani na wananchi wa maeneo ya machimbo kutaka kuwaharibia wawekezaji ili kutuma ujumbe kwa Serikali na Viongozi kuwa tunahitaji huduma zinazoendana na shughuli inayofanyika katika eneo letu. Mtu yeyote makini anapaswa kujifunza kwa mifano, si lazima iwe tukio halisi linaloendana na hali anayoikabili.
Sielewi kama ni dharau au pengine ni viongozi wetu kuwa na shughuli nyingi, hata wanashindwa kupanga muda wa kutosha wa kujadili na wananchi wao matatizo yanayowakabili na kusikiliza mapendekezo yao?
Ipo hii tabia mbovu kweli ya baadhi ya viongozi ya kwenda kwa wananchi na kuwaambia yale wao (viongozi) wanayoyaona ni sawa na yanafaa kwa jamii ile, halafu wakaondoka wakidhani wamemaliza kuhubiri, wakasahau kuwa wananchi ndiyo wasemaji wa mwisho ikiwa wameelewa kweli ama la.
Kiongozi unapoondoka ukidhani umeeleweka, basi subiri muda upite uuone mwenendo na kusikia mrejesho ndipo utaelewa ikiwa kweli ulichohubiri kilieleweka au unahitaji kubadili mbinu ya ueleweshaji.
Nikiri kuwa baadhi yetu tunakerwa na matumizi mabaya ya siasa, hasa pale inapoingilia na kuvuruga ukamilifu wa mambo.
Ninajiuliza, ikiwa njia zinazostahili kufuatwa ili kupata ufumbuzi wa matatizo yetu zimeshatumika, na wahusika wanaona bado hawajapata suluhu waliyoitaka, je, ni kosa kwa siasa kuingilia kati? Siasa ni njia mojawapo ya kutoa taarifa ya yanayoendelea. Hatuwezi kuikataa. Tuifuate kwa uangalifu.
Lakini, inawezekana kuwa tunaielewa visivyo siasa kiasi kwamba mtu anapofanya jambo lolote, kwa kuwa tu ametokea kuwa mwanasiasa, basi talanta nyingine alizokuwanazo hazipaswi kuonekana kwa kuwa tu, amekuwa mwanasiasa? Je, hili si kosa? Tukubali kuwa mtu aweza kuwa zaidi ya jambo moja. Mtu aweza akawa mwanasiasa, vile vile mwanataaluma, mfanyabiasahara, kiongozi wa imani, mwanamichezo, na kadhalika, alimradi utendaji wake wa kazi katika kutimiza jukumu fulani hauingiliani na talanta zisizohitajika. Pengine nasi kwa kuwa na mtizamo wa mrengo mmoja, tumewafungia vibandiko fulani watu fulani fulani kuwa kwa kuwa wapo hivi, basi hawapaswi kuwa hivi.
Hivi, kisa cha Ken Saro Wiwa na yaliyokwisha kutokea Tanzania na kwingineko, hayatoshelezi mafunzo?


RSS Feed