Juzi nilisoma habari iliyochapishwa kwenye blogu kuhusu Mbunge kuwapa Walimu fedha, kwa jina la "posho".

Ingawaje sikupata muda wa kuandika yatokanayo na taarifa hiyo, bado hainizuii kuandika leo niliyowaza.

Mazingira na sababu za ziada hasa za kutoa fedha hizo kwa Walimu sina undani wake, hivyo ninatoa mtizamo huu kulingana na kile kilichoripotiwa katika habari hiyo.

Nakiri kuwa kuwapa Walimu "posho" ya aina yoyote si kero kwangu, sina "wivu" walimu kupewa "posho" bali, napenda kuona "posho" hizo zinatolewa kwa kufuata utaratibu uliokubalika Kitaifa na usiyoleta manung'uniko kwa waajiriwa wengine, wala kuwapa shinikizo wawakilishi na waajiri wa maeneo mengine kutakiwa kufanya hivyo katika maeneo yao ya uwakilishi/kazi.

Mosi, nilipoisoma tu nilisema moyoni, "how cheap"! Kwamba ni udhalilishwaji. Nilisikitika sana kuona Walimu wanapewa shilingi elfu hamsini "kama posho" yao il hali huu si utaratibu wa Serikali. Nikajiuliza, ili kutoa posho, si lazima iwepo sheria au kanuni za Kiserikali zinazoruhusu kufanya hivyo, la sivyo, hii ni sawa na rushwa? Pengine sifahamu sheria hizo, nitafurahi kuelimishwa katika hilo.

Pili, nilihesabu hii sawa na rushwa ingawaje wengine huiita kwa jina lisilo na makali, "takrima", kuwashukuru wananchi kwa uchaguzi uliokwisha tangu Oktoba 2010. Naifananisha na rushwa kwa kuwa imetoka kwa Mtu binafsi kwenda kwa wafanyakazi wa serikali, na mtu huyo pia anaweza kutumia cheo cha Ubunge, nayo pia naiona ni rushwa hata ikiwa tayari miezi kadhaa ya uchaguzi imepita na ipo mingi mbeleni kwa uchauguzi ujao. Kumbukumbu hii ya kutoa fedha inatosha kabisa kurejelewa wakati wa uchaguzi ujao kuomba "kuzikumbuka fadhila" hizi kwa wakati huo.

Tatu, nimeona kama ufalme unaopingana ndani yake wenyewe. Nasema hivi kwa kuangazia kurunzi la siasa za vyama. Kwamba aliyefanya hivi ni Mbunge anayetokana na chama ambacho ndicho kimeshika hatamu ya uongozi wa Serikali ya nchi nzima. Kwamba, ikiwa yanafanyika haya kwa jina la kuisifu Serikali kupitia Chama fulani, je, ikiwa utaratibu huu si wa Kiserikali, hilo si kinyume na sheria/taratibu? Ikiwa ni ndani ya utaratibu wa Chama na Serikali, je, majimbo mengine na maeneo ya uwakilishi Wabunge wao wameshafanya hivi au wameweka kibodoni fedha za watu? Na, ikiwa wamepewa posho walimu, je, makundi mengine ya wafanyakazi hayastahili kupewa posho nao? Au kipimo cha kupewa posho hasa ni kipi? Kuwa na mshahara mdogo au kufanya kazi fulani? Na kama hivo viwili ni sehemu ya vigezo vya kiwango na aina gani ya posho itolewe, basi kutoa posho haitasaidia, badala yake, vigezo hivyo viwili inabidi kurejelewa ili kuona ni kwa vipi kundi hilo litajiweza bila kupewa posho. 

Nne, tujiulize, ikiwa jambo hili lingefanywa na chama chochote chenye upinzani wa kisiasa Tanzania, lingetafsiriwaje? Sikatai kuwa vipo vyama pinzani ambavyo vimefanya mambo fulani kwenye majimbo yake, mathalan wapo waliotoa magari kwa ajili ya "ambulance" au "madawati" au "pikipiki" n.k., ambavyo vyote hivyo vimetolewa kwa manufaa ya Wananchi wote na siyo kwa watu wachache au kikundi fulani katika jimbo/eneo la uwakilishi.

Mwishowe, najiuliza, je, huu ni mpango endelevu au ni tukio la kustukiza mara moja moja? 

Nihitimishe, kwamba, kama ambavyo ilipigiwa kelele ya kupinga kitendo cha baadhi ya Wabunge kuchangia nauli, kutoa vyombo vya usafiri na kuwawezesha wananchi wao kwenda Samunge "kwa Babu kupata kikombe", hata ikiwa msaada ulifanyika kwa wananchi wote bila kujali itikadi za vyama, tukahoji utaratibu huu unatuma ujumbe gani kwa watu wa maeneo mengine ambapo wabunge/wawakilishi wao hawana uwezo wa kifedha kuwasaidia wananchi wao wafike Samunge; Vivyo hivyo tuhoji, Je, kuwapa kundi fulani la watu "posho" badala ya kundi matokeo yake kwa jamii nzima ni yapi?

Rubuni isitutege na kututenga.

Silioni kosa katika utoaji fedha na shukrani/takrima, bali natilia shaka kwenye utaratibu unaotumika.

Binafsi nimehesabu hili sawa na udhalilishaji kwa Walimu (ama kundi lolote la waajiriwa/wafanyakazi), utumiaji usio sahihi wa cheo na kitendo cha rushwa aidha kwa kutokujua au kwa kupuuziwa madhara yake na kubeba sifa za matokeo ya kilichofanyika.
 


Comments

mera rupaiya
17/06/2011 02:47

Nimekubaliana na hoja yako! Kwa mtazamo wangu, ni jinai inayofanyika hdharani, kila mtu anajua kinachofanyika, mfumo umesimama namna hiyo kwa sasa na kwa kuwa kila mwenye mamlaka ananufaika mfumo basi kazi inabaki kwetu wapiga kelele tu. Baadaye nawe utaambiwa 'utafuta maarufu'. Kuwao kwa sheria ya kuwaripa wabunge pesa nyingi, isiyofanana na mchango wao ktk maendeleo ya nchi wala kuzingatia hali halisi ya uchumi wa nchi ndiyo chanzo chake. Lazima ujue huo ni uwekezaji, anawekeza kwa kuwa anajua walimu hutumika kwenye zoezi la kupiga kura na umaarufu wao vijijini si haba. Na zaidi sana anajua atazirudishaje. Ni nani ataubadili mfumo huu unaotuletea wabunge wezi na matapeli? nawasilisha

Reply



Leave a Reply