Ni kijana tu wa miaka 20 na anao uwezo mkubwa kweli wa kulisakata kabumbu. 

Lakini tatizo lake ni vituko visivyomwisha kila awapo kiwanjani.

Kituko kimoja kile cha wakati timu yake ya Manchester City ilipokutana katika ushidani wa kombe la FA ambapo dhidi ya timu ya Manchester United ambapo City ililinyakua kombe hilo. Kituko alichokifanya Balotelli ni kukushangilia upande wa washabiki wa timu yake ya Manchester City, bali yeye akatimua mbio kusherehekea kwa kebehi mbele ya timu pinzani  ya ManUnited. Jambo hili lilimkera kapteni Rio Ferdinand na kusababisha apandwe na jazba almanusura watandikane kisawasawa kiwanjani, kama siyo wachezaji na viongozi wa timu waliepusha rabsha. Mwenyewe Balotteli kumwona mwenziye amepandisha mzuka akamalizia kwa kumkonyeza! La haula! Akaharibu zaidi! (tizama video hapo chini). Sikubali kuwa ati Rio alikasirika kwa vile walifungwa, kwani mara ya kwanza Rio kupoteza kombe au kufungwa bwana?

Kocha mashuhuri Jose Mourinho "the special one" aliwahi kufanya kazi katika timu ya Inter Milan ya Italia, timu ambayo Balotelli alikuwa akiichezea wakati huo. Wachilia mbali tambo na majigambo 'the special one', alipoulizwa uzoefu wake wa kumfundisha Balotelli alisema, "kijana ana kipaji ila tatizo lake wakati mwingine hajui jinsi ya kutumia ubongo wake"... "The guy has incredible qualities, but sometimes does not know how to use his brain", nadhani ukifuatilia nyendo za Balotelli utakubaliana na Mourinho kuwa jamaa nati hazijakaza kichwani. Mara kadhaa yupo mbili kasorobo na anayoyafanya sijui ni kujitafutia umaarufu ama sifa ya kuandikwa na kuzungumzwa (kama hivi ninavyofanya mimi saa)? Ama diyo ile niliyosema, pengine anahitaji tambiko/sala! Inawezekana, ukiisoma historia yake unaweza kudhani hivyo (bofya hapa kuisoma). Historia ya ya mtu maisha inaweza kumjenga au kumbomoa mtu kwa jinsi ya ndani (roho) na nje (mwili).

Kabla ya kituko cha juzi, aliwahi kukamatwa na Polisi wa Uingereza, akaulizwa vipi kwenye gari mbona unabeba fedha zote hizi? (fedha taslimu £25,000 zilikuwa kwenye kiti cha abiria ndani ya gari lale la kifahari - Maserati ambalo lilikuwa limepigwa faini mara 27 anasimulia mfanyakazi mmoja wa klabu ya Manchester City  - The other week the Maserati misfired so he just abandoned it. Staff have had to bail it out 27 times.) Alichowajibu, "Because I can" - habari kamili isome kwenye the Daily Mail. Sijui kila mtu tajiri angeamua kuwa anatembea na fedha taslimu nyingi kiasi hicho uhalifu ungekuwa wa kiwango gani. Inahitaji akili kidogo tu! 

Kituko cha juzi sasa! Kakitoa wakati akiwa amekaribia golini akiwa ana nafasi kubwa kabisa ya kufunga goli, kwa kuwa alitaka kulifunga kwa staili anayoijua yeye, akaamua kugeuka kisha akaubetua mpira kwa kisigino, matokeo yake, mpira ukatoka nje ya goli. Aliwashangaza si tu wachezaji wenzie, kocha wake Mancini na watazamaji bali na hata wasiokuwa wanajua kilichofanyika sasa wanashangaa! Ilibidi kocha amtoe kwa hasira na badala ya kuliona kosa lake, ah, yeye akaabwatuka kwa malalamishi angali anatoka kiwanjani!

Watu hufanya vituko kiwanjani, vituko vizuri vya kuwakumbuka vizuri, si vya ajabu ajabu hivi. Sasa basi afanye vituko vyenyewe afanikiwe, wapi, na kwenye vituko anachemsha. We tizama goli alilojaribu kulifanyia mbwembwe (ama alikuwa akiiga staili ya Awana Diab wa nchi za Falme za Kiarabu, UAE, ilipopambana na Lebanon akafunga penati kwa kisigino, bao ambalo limemtia matatani, video ipo hapo chini).

Kama ni historia, anaiandika ila sidhani kama anaiandika vizuri. Anahitaji maombi/matibabu (pengine)!
 


Comments

25/07/2011 21:53

Huyu ni mbongo so ana tabia zilezile za kibongo japo anaishi ulaya.
Dawa yake asajiliwe na timu za bongo ili aje aoneshane ubabe wake na waloshiba ugali na bamia

Reply



Leave a Reply