
Ngassa ambaye aliwahi kwenda nchini Uingereza kufanya majaribio katika klabu ya West Ham wakati akiwa Yanga, atarejea nchini na kuichezea Azam katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu utakaoanza Agosti 20 na baadaye taratibu za kukamilisha uhamisho wake zikiendelea kufanyika.
Ngassa aliichezea Seattle Sounders katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Manchester United Julai 20, ambapo aliingia uwanjani katika dakika ya 76 akitokea benchi la wachezaji wa akiba (bofya hapa kutizama sehemu ya mchezo huo).
Nyota huyo aliliambia gazeti NIPASHE hili kwa kifupi kwa njia ya simu juzi kwamba amefarijika kuelezwa kwamba amefanya vyema katika majaribio na anaamini kuwa mazungumzo yaliyobakia ya kukamilisha taratibu za kucheza soka nje ya nchi yatakwenda vizuri na yeye kuanza kusakata soka la kulipwa, "Namshukuru Mungu sasa naweza kuonyesha yale ambayo nilikuwa nayawaza, sitabweteka, huu ndio mwanzo."
Naye kocha, Sigi Schmid wa Seattle Sounders amemtaka mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Azam, Mrisho Ngassa kujifunza kusaidia ukabaji, “Ngasa si mchezaji mkubwa, lakini nina uzoefu ya wachezaji wafupi kufanya vizuri hapa Seattle, hivyo sio jambo litalotusumbua. Ni mchezaji mwenye kasi. Nafikiri kasi yake akiwa kwenye eneo fupi ni kitu cha kipekee,” alisema Schmid. “Kiufundi, ni mzuri. Anaweza kukokota mpira na kupiga mashuti vizuri. Anaweza kusoma mchezo vizuri. Nafikiri anahitaji kujirekebisha kwenye ulinzi zaidi, lakini ni mchezaji mzuri kwenye kushambulia na mwepesi wa kuzoeana na wenzake uwanjani hilo ni jambo zuri,” alisisitiza Schmid.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Azam, Idrissa Nassor, alisema kuwa baada ya kufuzu majaribio hayo, Ngassa, atarejea nchini wakati wowote kuanzia kesho na mazungumzo rasmi kati ya klabu hizo mbili yatafanyika na wao wamejipanga kuweka mbele maslahi ya mchezaji huyo ili kuweza kupata nyota wengi zaidi wanaocheza nje ya nchi.
Alisema kwamba usajili wa Ngassa kujiunga na Seattle Sounders utakamilishwa katika majira ya joto na ataweza kuanza kuichezea timu yake hiyo mpya mwezi Februari mwakani, "Sisi tuko nyuma yake kwa sababu tunafahamu kwamba amepiga hatua moja mbele katika maisha yake na hatua ya majadiliano kati yetu (Azam) na klabu hiyo ya Marekani yatakwenda vizuri," aliongeza katibu mkuu huyo.
Ngassa alipata nafasi ya kwenda katika majaribio hayo baada ya kuteuliwa na uongozi wa timu ya African Lyon ya jijini Dar es Salaam ambayo ndiyo ilikuwa na mahusiano na klabu hiyo ya Marekani.
via MWANANCHI na NIPASHE


RSS Feed