Nimeshangazwa, si mara moja, mbili au tatu, ni zaidi.
Kinachonishangaza na kunitia simanzi ni jinsi ninavyowasoma watu kwenye blogu, e-groups, e-forums na tovuti, ambazo yapo matangazo ya nafasi za masomo au kazi zinazowahusu Watanzania, lakini mara nyingi nafasi hizo zinachangamkiwa zaidi na jirani zetu Wakenya.
Mathalani ni kazi ya kutafsiri ambayo nimeinukuu na kuimeibandika hapo chini.
Ukiitizama, wengi waliojitutumua ni Wanaigeria au Wakenya. Pengine tutajitetea kuwa Naigeria ina wakazi wengi na raia wengi waliotawanyika kote ulimwenguni, je, kwa Kenya tutajiteteaje? Idadi yao ya raia kweli ni tishio kwa Tanzania hata waweze wao kuchangamkia fursa hizo zaidi yetu sisi?
Hata ikiwa matumizi ya TEHAMA kwa Wakenya ni kubwa zaidi ya ile ya Watanzania kwa sababu kadha wa kadha ikiwamo matatizo ya umeme na jamii kubwa kutokutumia tarakilishi; Ninakataa dhana hiyo kwani ipo idadi ya Watanzania wengi ambao huperuzi blogu na tovuti mbalimbali za habari na pia wapo sana kwenye mitandao jamii kama faceboook na twitter. Cha ajabu, nikitizama walio wengi katika kundi langu la marafiki (ninao wafahamu na nisiowafahamu) mengi ya wanayozungumzia ni mambo yasiyo kuwa na kichwa wala mkia, aghalabu, mambo yasiyoweza kumsaidia katika kujijazia elimu na maarifa bora.
Wanaotoa maoni mengi huegemea zaidi upande wa siasa, tena siasa za lawama na siyo siasa za nini cha kufanya ili kusaidia kuondokana na hali duni. Inakuwa kama vile kila siku mtu anataka kurusha lawama kwa watu au kundi fulani, kisha anajisikia vizuri kuwa naye siku hiyo ametoa machungu yaliyo moyoni. Sasa kusema tu bila kutenda kwa mfano kuna faida gani? Kama ni kuzungumza na kusema mbona yayo hayo yanasemwa na kurejelewa siku nenda rudi, kwani wanaopaswa kusikia hawajasikia? Hilo halitoshi kuwa funzo kuwa mbinu ya kupiga domo mfululizo tu si hoja tena? Kila mtu tu aseme, nani asikilize?
Sisi tukiendelea kupiga kelele, wenzetu Wakenya, pamoja na kupiga domo huku na huko kwa mambo yasiyo na kichwa wala mkia, bado wanaongoza kwa kuchangamka kutafuta ziliko nafasi za kazi mitandaoni.
Hivi sisi tutabaki tunawapigia kelele Wakenya kwa kufanya hivi na vile hadi lini badala ya kuchangamka?
Kwa kweli ninakereka ninapoona wengine wanajitahidi kusambaza nafasi za elimu na kazi, lakini bado ni kama vile walengwa wamevuta shuka na kugeukia upande wa pili. Tutasaidiana vipi ndugu, jamaa na marfiki zetu ikiwa wengine wanabakia tegemezi na kuomba omba tu?
Watanzania wenzangu, tuwahimize watumiaji intaneti wanapofika kwenye intaneti kuwa jambo la maana na muhimu kufanya ni kuperuzi tovuti zenye nafasi za kazi, shule na zile zenye taarifa chanya zinazoihusu jamii.
Watu wasiishie kuweka "status update" kwenye facebook na twitter na kutumiana tu jumbe za "nakupenda", "unakaa wapi?", "unasoma au unafanya kazi?", "naweza kukuona?", "naomba namba yako ya simu", "wewe mzuri..." maoni (comments) yasiyo na tija!
Habari ya kazi ya kutafsiri niliyoitolea mfano ni hii ifuatayo [inapatikana: freelancer.com]:-
I have a translation project from english to Swahili, Igbo, and Afikaans.
I want to be ready with some freelancers or companies to help me with these translation.
Please send me your fees per 1000 words. Also, let me know your daily output.
Budget: $250-$750 USD
Created: 06/26/2011 at 18:16 EDT
Bid Count: 13
Average Bid: $373 USD
Ends: 07/01/2011 at 18:16 EDT






RSS Feed