Picture
Fatma Kimario
Je, kilichofanyika Igunga siku ya mkutano wa CHADEMA kinaweza kuwa mojawapo ya mambo ya kujifunza na kuzingatia nyakati za kampeni hadi uchaguzi kwa mujibu wa sheria na miongozo mipya? 

Je, kilichofanyika kinaweza kuwa funzo la kutokuchukua sheria mkononi kama walivyofanya wafuasi wa CHADEMA ambao bila shaka walipandwa jazba na hasira kwa walichodhani ni hujuma dhidi ya chama chao?

Ikiwa kilichoelezwa katika habari hizi ndicho hasa kilichotokea, basi ni dhahiri kuwa siku za sasa, kina mtu anapaswa kuyafahamu kinagaubaga majukumu yake na mipaka yake (viongozi na wananchi), kinyume na hivyo, ni kujikuta katika sekeseke kwa kufanya mambo kwa mazoea "kama zamani" au "ndiyo tulivyozoea" kumbe tayari ulishatoka mwongozo mpya unaoelekeza kipi kifanyike, kipi kisifanyike na katika mazingira gani.

Ile dhana ya kutokusoma vitabu na kujielimisha kwa mambo mapya, itakwisha. Utamaduni wa kujisomea na kuelewa kilichoandikwa, na uanze!, ili kuepusha shari.

Ifuatayo ni nukuu ya vyombo rasmi vya habari kuhusiana na tukio hilo.
-------

CHADEMA wamkamata Mkuu wa Wilaya Igunga 
[hii ni sehemu ya habari iliyochapishwa na gazeti Mwananchi]

Vurugu zimezuka juzi katika Kata ya Isakamaliwa, wilayani Igunga zikiwahusisha viongozi wa CHADEMA na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario.

Katika sakata hilo, wanachama wa CHADEMA walimkamata Mkuu huyo wa Wilaya kwa tuhuma za kuendesha mkutano wa ndani na watendaji wa serikali za vijiji, wakati akijua kuwa kulikuwa na mkutano wa kampeni za chama hicho karibu na eneo hilo.

Msafara wa CHADEMA ulifika katika eneo la kampeni saa 8.00 mchana na kabla mkutano haujaanza, Meneja Kampeni wa chama hicho, Sylivester Kasulumbai, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mkuu wa wilaya ya igunga alikuwa akifanya kikao cha ndani katika eneo hilo kinyume na taratibu, hivyo wanakwenda kumshughulikia.

Kasulumbai ambaye ni Mbunge wa Maswa Mashariki akiwa na Mbunge wa Viti Maalum, Susan Kiwanga, baadhi ya wananchi na vijana wao, walifika katika ofisi ya Mtendaji wa Kata kulikokuwa kunafanyika mkutano huo na kuanza kuhoji aliko Mkuu huyo wa Wilaya.

Mmoja wa wananchi alimnyooshea kidole mama ambaye alikuwa amekaa mbele na kusema; “...yule ndiye Mkuu wa Wilaya”. Kundi hilo la vijana na viongozi wa CHADEMA, waliingia katika ukumbi huo na kumtoa nje mama huyo huku wakimtaka aeleze kwa nini anafanya vikao vya ndani katika Kata hiyo wakati anajua kuwa chama hicho kilikuwa na mkutano katika eneo hilo.

Kitendo hicho kilizua purukushani na kutokuelewana kati ya waliokuwa kwenye mkutano wa ndani na viongozi wa CHADEMA, jambo lililovuta umati mkubwa wa watu.

Baadhi ya vijana wa CHADEMA walikuwa wamewashikilia watu waliokuwa wakishiriki mkutano huo huku mama huyo akitolewa nje na kuketishwa kwenye kiti alitakiwa atoe maelezo kuhusu mkutano wake.
Baada ya kukaa kwenye kiti huku akionekana kuchanganyikiwa, alisema yeye ni Mkuu wa Wilaya ya Igunga, jina lake ni Fatma Kimario na kwamba, hakuwa na taarifa za mkutano wa kampeni za CHADEMA.

“Sina ratiba, iko katika ofisi za halmashauri, hivyo sikujua kama kuna mkutano hapa, hata hivyo watu walikuwepo niliwaruhusu waende mkutanoni na mimi nilikuwa naondoka sasa hivi,” alisema na kuongeza:

“Nilichokuwa nafanya ni mkutano wa viongozi wa serikali kwa ajili ya kuangalia hali ya mifugo inayoibwa sana, elimu kwa wote hasa watoto na ujenzi wa nyumba bora na masuala ya amani”.

Picture
Kimario na wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CHADEMA katika sekeseke
Kimario aliwasihi wafuasi wa CHADEMA kusoma karatasi ya ajenda ili wafahamu kilichokuwa kikijadiliwa kwenye kikao hicho.

Karatasi aliyokuwa akiizungumzia Mkuu huyo wa Wilaya ilikuwa na ajenda tano za kikao hicho ambazo ni; Uhamishaji wa mifugo; Kuwa na choo chenye ubora na nyumba bora; Elimu;  Mipaka ya shule na ajenda ya mwisho ilikuwa Uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga.

Hata hivyo mbunge Kiwanga alimtaka mkuu huyo wa wilaya aeleze tangu lini kikao cha viongozi wa serikali kikahudhuriwa na wazee maarufu na mabalozi wa nyumba kumi, swali ambalo lilionekana kumchanganya mkuu huyo wa wilaya kwa kutoa majibu tata.

Wakati hayo yakiendelea, mkutano wa kampeni ulikuwa nao ukiendelea, hivyo viongozi hao wa CHADEMA walimtaka DC huyo afike kwenye mkutano huo ili aweze kuonana na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willibrod Slaa.

Kimario alikubali, lakini akataka dereva wake atangulize gari na kwamba yeye angefuata. “Nitakwenda kwani napaswa kuwepo pale kama msimamizi wa usalama, sijahudhuria mkutano wowote hivyo nitakwenda,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo kwenye mkutano wa kampeni, Dk Slaa alisema wakuu wa wilaya na mikoa kufanya mikutano wakati wa kampeni ni kinyume cha sheria, hivyo Kimario alienda kuanzisha vurugu.

“Hapaswi kufanya mkutano wowote hapa hasa akijua kuwa sisi tuna mkutano wa kampeni na yeye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Wilaya,” alisema Dk Slaa na kuongeza, “DC anafanya nini huku wakati hiki ni kipindi cha uchaguzi au ndiyo wanapanga mikakati ya uchakachuaji halafu wanadai sisi ndiyo tunaofanya vurugu?”


VIDEO: Hatua walizotangaza CHADEMA kuwa watachukua kwa tukio hilo


DC Amedhalilishwa 
[habari iliyochapishwa na HabariLeo, inayohusiana nayo kwa Kiingereza ni Police question five for harassing Igunga DC]

Serikali imesikitishwa na udhalilishaji uliofanywa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Fatma Kimario juzi. 

Imesema kwa kuwa nchi inafuata utawala wa sheria, inaviachia vyombo vya Dola vifanye uchunguzi wake. 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Mkuchika, alipozungumza na gazeti hili akiwa Newala mkoani Mtwara., “Serikali imesikitishwa na udhalilishaji uliofanywa kwa DC wa Igunga. Nchi ina taratibu, kanuni na sheria kwa hiyo unaviachia vyombo vya Dola kufanya kazi yake. “Lakini tumesikitishwa na tukio lile kwa sababu DC alikuwa tayari kusema nao, alikuwa eneo lake la utawala akifanya kazi. Kwa nini wamkamate na kumtoa nje kwa udhalilishaji ule,” alisema Mkuchika. 

Alisema haikuwa vyema kwa wahusika kufanya udhalilishaji huo hasa baada ya Mkuu huyo wa Wilaya kuwa tayari kuzungumza nao; hivyo wangeweza kuzungumza naye ofisini katika mazingira ya ustaarabu. 

DC Kimario alifanyiwa vurugu na vijana wa CHADEMA juzi akiwa katika shughuli zake za kikazi. 

Vijana hao walidai DC alikuwa akifanya kampeni za kisiasa katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Igunga utakaofanyika Oktoba 2, mwaka huu. 

Katika taarifa yake jana, Polisi ilisema DC huyo amefanyiwa shambulio la kudhalilisha kinyume cha maadili, ikiwemo kuvuliwa vazi lake la hijab ambalo humsitiri mwanamke wa Kiislamu hasa kichwani. 

Akizungumza jana wilayani Igunga, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini wa Polisi, Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu, alisema mbali na kuvuliwa hijab, pia DC alidai alivuliwa viatu na kukatiwa mkufu, "Pia simu yake ya mkononi aina ya Samsung ilipotea na alitukanwa matusi ya nguoni ya kumdhalilisha …(hatuwezi kuyaandika hapa)," alisema Mngulu akielezea madai hayo ya DC Kimario. 

Alisema wakati Mkuu huyo wa Wilaya akifanyiwa vitendo hivyo na vijana hao wa CHADEMA, Ofisa Tawala wa Wilaya ya Igunga, Sunera Manoti, alikwenda Polisi kutoa taarifa. 

Hata hivyo, baada ya Polisi kupata taarifa hiyo, kwa mujibu wa Mngulu, walikwenda eneo la tukio na kukuta hali ni shwari na kuanza upelelezi baada ya majalada ya tuhuma; la kwanza la DC akilalamika kufanyiwa shambulio la aibu na la pili la CHADEMA wakilalamikia kuingiliwa katika mkutano wa kampeni. 

Kwa mujibu wa taarifa za CHADEMA, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Kiwanga, Mbunge wa Maswa Mashariki, Kasulumba Sylvester pamoja na shabiki wao ambaye jina lake halikupatikana waliitwa Polisi na kuhojiwa saa moja na kuachiwa kwa dhamana. 

Madai ya CHADEMA Awali, kabla ya Polisi kuzungumzia hilo, CHADEMA iliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuelezea makosa 15 ya DC huyo, likiwemo la kuitisha mkutano waliodai kuwa ni wa hadhara na kinyume cha sheria. 
Picture
Mtendaji wa Kata na wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CHADEMA katika sekeseke
Akifafanua madai hayo, Mkurugenzi wa CHADEMA wa Oganaizesheni na Mafunzo, Benson Singo, alidai kuwa mtu ye yote akitaka kufanya mkutano, lazima atoe taarifa kwa Polisi na kwa kuwa polisi walikuwa wakifahamu kuwepo kwa mkutano wa Chadema, wasingemruhusu DC kufanya wa kwake. 

Hata hivyo, Mngulu alisema DC Kimario alikuwa katika kikao cha ndani na sio mkutano wa hadhara kama Chadema walivyodai, ambacho kisingehitilafiana na mkutano huo wa CHADEMAa, lakini hata muda wa tukio la kushambuliwa Mkuu huyo wa Wilaya na mkutano wa CHADEMA vilikuwa tofauti. 

Kwa mujibu wa ratiba ya mikutano ya hadhara ya kampeni iliyooneshwa na Mngulu, CHADEMA ilipaswa kufanya mkutano wao wa hadhara katika eneo hilo la Kijiji cha Isakamaliwa saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana na tukio hilo, lilitokea kati ya saa 8:30 na saa 9. 

Mngulu alisema hata polisi walikwenda eneo la mkutano huo kulinda amani saa 4 mpaka saa 6, lakini waliondoka kwa kuwa CHADEMA hawakwenda katika mkutano huo kwa mujibu wa ratiba. 

CHADEMA pia walilalamika kuwa katika kikao hicho, DC huyo alikusanya na kujadili barua za maombi ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura na waelekezaji wa vituo kinyume cha sheria. 

Hata hivyo, DC Kimario alipozungumza na waandishi na kuhojiwa kuhusu kukutwa na baadhi ya barua za maombi ya wasimamizi wa vituo vya kupiga kura, alisema alipewa na wasimamizi wa uchaguzi vijijini ili awasaidie kuzipeleka kwa msimamizi wa uchaguzi. 

DC katika maelezo hayo, alisema anajua Chadema watasema kuwa alikuwa na hizo barua, lakini kwa maelezo yake ni kwamba yeye alitoa msaada tu wa kuzifikisha kwa msimamizi wa uchaguzi. 

Waandishi wagawanyika Katika tukio lingine, waandishi wa habari waliokutana Kituo cha Polisi muda mfupi baada ya kumalizika kikao cha Chadema na waandishi, waligawanyika, baadhi wakimtuhumu DC kuwa ndiye mwenye makosa; wengine wakiituhumu Chadema ndiyo chenye makosa. 

Waliomtuhumu DC Kimario kuwa ndiye mwenye makosa, walidai ameitisha mkutano huo kinyume cha sheria na walipopewa sheria hiyo na kutakiwa kuisoma, walibadilika huku wakisahihishana kuwa, hakukiuka sheria, bali maadili ya uchaguzi. 

Waliokuwa wakituhumu kuwa CHADEMA ina makosa; walitaka kujua Polisi imechukua hatua gani; kama inawashikilia watuhumiwa ni wangapi, akina nani na lini watapelekwa mahakamani. 

Akijibu hoja hizo, Mngulu alisema suala la kukiuka maadili ya uchaguzi ni la Msimamizi wa Uchaguzi, Protas Magayane, lakini suala la shambulio ni la Polisi. 

Alisema mpaka sasa wameshawahoji watu watatu, lakini akakataa kuwataja majina kwa maelezo kuwa uchunguzi bado unaendelea. Hata hivyo katika mkutano na waandishi wa habari na CHADEMA, Mkurugenzi wa Chadema wa Oganaizesheni na Mafunzo, Singo alisema waliohojiwa ni pamoja na wabunge hao wa Chadema. 

Gazeti la HabariLeo liliwasiliana na Msimamizi wa Uchaguzi, Magayane kwa simu ambaye alijibu kuwa yupo Dar es Salaam akishughulikia picha za wagombea. 

Kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Igunga tayari zimekumbwa na matukio ya vurugu huku yakihusishwa na CHADEMA ikiwemo mtu mmoja kumwagiwa tindikali na wengine kukatwa mapanga.


(picha zote kwa hisani ya DewjiBlog)
 


Comments

17/09/2011 14:05

hamna lolote hapa, hizi ni michezo ya kisiasa tu ili watu wawazidi wenzao kete na kuchukua jimbo. Hizi ndizo longo longo watanzania wanapenda kwa kweli

Reply
Bina
17/09/2011 15:04

Hapa ndo kutafutana kwenyewe.Cha msingi hili la uchaguzi lisimeze yanayoendelea huko Pemba.Hatua za makusudi za kulifanyia upembuzi lile jangwa lifuatiliwe

Reply



Leave a Reply