Mwanzoni mwa mwezi huu nilikuwa nasikiliza kipindi (sikukumbuki jina) katika Redio Sauti ya Injili, Moshi, Tanzania siku ya Jumapili kikiendeshwa na Hellen Madege-Yongo ambapo aliwahoji baadhi ya watu kuhusiana na mila na desturi ya kukeketa wanawake "female genital mutilation" (FGM).
Sikiliza audio hii:
Ajabu ni kwamba, wanathubutu kuwatahiri hata watoto wadogo!
Yupo mwanaume aliyesema kuwa sababu ya kuendelea kufanya hivyo ni ili kumzuia mkewe asipate hamu ya kujamiiana na mwanaume mwingine hasa pale mumewe anapokuwa amesafiri mbali na nyumbani kwa shughuli za kikazi na kipato. Alipoulizwa lengo la kuoa, akajibu kuwa, mkewe aliposwa na kuletwa nyumbani ili kukaa na mama mkwe. Alipoulizwa ikiwa huko aendako kikazi hatoki nje kwa wanawake wengine, alikiri kuwa anaweza kutoka lakini yeye ni mwanaume na "ngono ni kitu kizuri" hivyo "unapokunywa na kula nyama za kuchoma huwezi kukaa miezi sita bila kuruka na mwanamke". Alipoulizwa iweje si sawa kwa mkewe, alijibu kuwa mke yupo kwa heshima ya mama mkwe!
Hata hivyo wanaume wengine waliohojiwa walishangazwa kusikia kuwa zipo koo na familia zinazokeketa na hiyo ilikuwa ni enzi za utawala wa Mangi lakini hazifai kwa kuwa si sahihi.
Baadhi ya wanawake walipinga vikali desturi hiyo.
Wanaharakati wa kike na wakiume wanaopambana kukomesha ukeketaji kwa wanawake kutokana na madhara yake, walikemea tendo hilo na kutaka elimu na uhamasishaji zaidi viendelee ili kuepusha madhara ya ukeketaji.
Mbunge asikitishwa na ukeketaji Rombo via HabariLeo
Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Kilimanjaro, Betty Machangu (CCM), ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya ukeketaji vinavyoendelea kufanywa na baadhi ya mangariba wilayani Rombo kwa malipo ya Sh 10,000, kitenge na mkia wa kondoo hali aliyosema linahitaji kuvaliwa njuga.
Akizungumza na viongozi wa Umoja wa Wanawake (UWT) wilaya ya Rombo, alisema katika kijiji cha Endomet bado wapo wazazi wanaokeketa watoto wao wa kike na baada ya kuona serikali imechachamaa hutumia mbinu ya kuwadanganya watoto hao kuwa wanakwenda kuwatembelea aidha shangazi au mjomba na wakirudi wanakuwa tayari wamekeketwa.
Naye Mwenyekiti UWT wilayani Rombo, Ambrosia Mashingia alisema mtandao unaopinga ukatili wa kijinsia (NAFGEM) ulitoa semina katika kijiji hicho ambayo iliwasaidia watoto hao na sasa wamekuwa na elimu ya kutosha juu ya madhara ya ukeketaji.


RSS Feed