Video inayoonekana mwisho kabisa ya hivi karibuni, yenye mawaidha toka kwa Langa, niliiona mara ya kwanza kupitia vijana.fm ambao ni tovuti kaka wa wavuti.

Habari ya Langa inanigusa binafsi na kwa ukaribu wa pekee. Baada ya kusoma safuya Nyota wa Wiki katika gazeti la Serikali la HabariLeo nimefurahishwa sana na hatua aliyoipiga 'very talented' Langa katika mabadiliko ya kweli. Ninapenda vijana wajifunze, wazazi na walezi wapate mwangaza wa maneno ya Langa.

Langa
Langa
cross-posted kutoka  HabariLeo

Je, unamkumbuka Langa Kileo? Bila shaka hili ni jina maarufu, hasa kwa wadau wa masuala ya burudani wa ndani na nje ya nchi. 

Huyu ni mmoja wa matunda ya shindano la muziki la Coca-Cola Pop Stars mwaka 2004 ambalo washindi wake waliounda kundi la Wakilisha. 

Mbali ya Langa, wengine ni Sarah Kaisi `Shaa’ na Witness Mwaijaga `Witness’. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kung’ara kisanii kwa wakali hao, ingawa kwa sasa kundi hilo limesambaratika, kila mmoja akitamba kivyake. 

Lakini kwa bahati mbaya, mmoja wao, Langa kwa miaka ya hivi karibuni hakusikika kabisa, jambo lililomlazimu mwandishi wa makala haya kumtafuta sababu za ukimya wake. 

Haikuwa kazi rahisi, lakini hatimaye Langa alipatikana na bila kutafuna maneno alisema kwamba, alishindwa kufanya kazi baada ya kuwa `teja’ aliyekubuhu. 

Yaani alizama katika matumizi ya dawa za kulevya kiasi cha kupoteza kabisa mwelekeo si wa kisanii pekee, bali hata kimaisha. 

“Siyo siri, kilichokuwa kimenifikisha katika hali hiyo ni dawa za kulevya. Kwa miaka mitano nilitumia sana Cocaine, Heroin, bangi na pombe. Namshukuru Mungu sasa nimerejea katika hali yangu… 

“Siamini kama nimenusurika kwa sababu madawa yalinitesa, nikafanya mengi ya ajabu yaliyoichukiza familia yangu na marafiki ikiwa pamoja na kuwa mwizi na mkabaji mitaani na nyakati za usiku,” anasema Langa ambaye kundi lao la Wakilisha lilitamba na nyimbo kama `Unaniacha Hoi’ na `Kiswanglish’. 

Anaeleza kwamba, kwake hayo ndiyo aliyoyaona maisha yanayomfaa, akidai awali alikuwa amechoshwa kuishi kwa masharti kutoka kwa wazazi wake waliokuwa wanampa mwongozo wa maisha, lakini bila kujua akadhani `anachungwa’. 

Kwamba, umaarufu na ngekewa ya kuzishika pesa katika umri mdogo kupitia muziki vilimtia kiburi zaidi, na hivyo kuamua kujitenga kabisa na familia yake iliyomlea kwa mapenzi mazito. 

“Niliamini naweza kujitegemea kupitia kazi yangu ya muziki, nikajichanganya mtaani,” anasema kijana huyo aliyetoa kibao chake cha kwanza, Matawi ya Juu mara baada ya kusambaratika kwa kundi la Wakilisha kutokana na kila mmoja kuamua kujitegemea kimuziki. Na kweli, Matawi ya Juu ilidhihirisha kuwa Langa ni moto wa kuotea mbali katika fani. Aliweza kusimama kwa miguu yake na kutikisa. 

Mwenyewe anasema: “Jina hilo la Matawi ya Juu lilidhihirisha hivyo pale video ya kibao hicho ilipotajwa kuwania Tuzo za MTV Base kwa upande wa hapa Bongo miaka michache iliyopita, kisha kutwaa Tuzo ya Kisima nchini Kenya. “Moto huo uliwafanya baadhi ya wasanii wakongwe katika gemu ya Bongo Fleva kunitafuta na kunipa majukumu ya kushiriki katika kazi zao, ikiwemo Chagua Moja ya Farid Kubanda `Fid Q’. 

“Baada ya kuona wakongwe wamekubali vitu vyangu na kuanza kunishirikisha…nikapata pia safari za nje ya nchi. Huko Nairobi (Kenya) niliweza kufanya kazi na vichwa vikali vinavyounda Kundi la Necessary Noise, Naaziz na Wyre (Kevin Wyre)….” 


Anasema mafanikio hayo yalimtuma kufyatua albamu yake ya kwanza aliyoipa jina la Langa, akiamini itampaisha zaidi kimaisha na kimuziki. Hata hivyo, mambo yalikwenda kinyume. Anasema alipoipeleka sokoni, wauzaji wakubwa waliigomea, hivyo kumpa wakati mgumu wa kuwaza na hatimaye kujikuta akiongeza kasi ya matumizi ya dawa za kulevya. 

Siyo siri, kugoma kwa albamu yangu sokoni kulichangia kasi ya kutumia dawa za kulevya…niliona ni njia pekee ya kuondoa mawazo kwa sababu kazi iligoma, na home (nyumbani) nilishaharibu. 

Sikufanya tena kazi kwa umakini na kila kazi niliyoitia haikufanya vizuri….” Anasema kwamba, baada ya mambo kumwendea mrama, ndipo alipoanza kuiba vitu nyumbani kwao kwa lengo la kuviuza na inapotokea amekosa, alidiriki hata kupiga debe katika vituo vya mabasi ili mradi apate fedha za kununua `unga’. 

Haikuishia hapo, kwani anasema alijiingiza katika kundi la wahuni waliojihusisha na wizi na ujambazi. “Kwa ujumla nilipoteza mwelekeo. Maisha yangu yakawa ya kutembea na kisu kama kitendea kazi changu katika wizi,” anasema huku akitikisa kichwa kama ishara ya kujutia matendo aliyoyafanya kwa msukumo wa madawa ya kulevya. Anakumbuka akiwa mtumwa wa `unga’, aliingia katika mikasa kadhaa ikiwa pamoja na kupigana na polisi baada ya kunaswa na dawa hizo haramu. 

Katika wizi, chochote alichokikuta mbele yake kilikuwa halali. Anasema alikwapua vitu magengeni, madukani na hata magari yaliyoegesha vibaya alinyofoa vioo na mashine zinazosaidia kupandisha na kushusha vioo ndani ya gari. 

“Ni matukio ya aibu. Yanasikitisha…,” anasema Langa anayedokeza kwamba, akiwa mtumiaji wa `unga’, alikuwa anakutana na wasanii na watu wengine mashuhuri. Hata hivyo anakataa kuwataja, akidai ni siri yake. `Ufufuo’ wa Langa kutoka katika lindi la mateso ya dawa za kulevya ulipatikana kuanzia Machi mwaka huu, baada ya familia yake kumpeleka kijana wao kwa tiba maalumu ya kuachana na matumizi ya `madudu’ hayo. Na kweli, elimu imemwingia na kujikuta akirejea ufahamu wake wa kawaida. 

Ametangaza kuachana na `unga’, pombe, sigara na badala yake amejikita zaidi katika mazoezi ya kurudisha mwili wake katika hali ya kawaida. Aidha, amekata shauri la kuirudia fani yake na tayari ana vitu vipya, Bombokiata na Mteja Aliyepata Nafuu. 

Anasisitiza kwamba, kutokana na mateso aliyoyapata, anakusudia katika siku za baadaye afungue kituo chake cha tiba ya dawa za kulevya ili aweze kuwaokoa vijana wengine wanaoangamia kutokana na matumizi ya dawa hizo haramu zinazopigwa vita karibu kote duniani. “Nimenusurika, namshukuru Mungu. 

Nami najipanga kutaka kuwasaidia wengine waachane na mateso ya dawa za kulevya. Pia nichukue fursa hii kuwaomba msamaha wote niliowakosea kwa namna moja ama nyingine wakati nikiwa `teja’,” anasema Langa, kijana mwenye umri wa miaka 25.

Je, historia ya maisha ya Langa ikoje? Anasema Desemba mwaka 1985 jijini Dar es Salaam akiwa tunda la wanandoa Vanessa Kimei na mumewe Mengisen Kileo. Alisoma Shule ya Msingi Olympio na Sekondari ya Loyola, zote za jijini Dar es Salaam. 

Hata hivyo, akiwa kidato cha pili alihamishiwa Kampala, Uganda katika Shule ya Vienna na baadaye Shule ya Hillside International Academy, huko huko Uganda. Baadaye alirejea nchini na kujiunga na masomo ya Stashahada ya Masoko katika Chuo cha Biashara Dar es Salaam (CBE), Kampasi ya Dodoma. 

Huyo ndiye Langa Kileo msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye baada ya kulewa umaarufu na kujikita katika matumizi ya dawa za kulevya, ameibuka na kujutia `ujanja pori’, sasa akitaka kujiingiza katika kampeni ya kuwaokoa vijana wengine waliozama katika `unga’. Anakusudia pia kurudi darasani kujiendeleza na masomo ya elimu ya juu. Je, atafanikiwa? Kwa hakika, hili ni jambo la kusubiri na kuona.
 


Comments

Sabato
03/08/2011 01:33

Ushauri wangu ni kwamba asirudi tena katika fani ya Bongo Fleva, labda aingie kwenye Gospel Songs. Huku atakutana na walokole ambao watamsaidia zaidi kukimbia mbali na unga kuliko akirudi kwenye muziki wa kidunia, ambapo kuna vishawishi vibaya na uwezekano mkubwa sana wa kurudi kwenye madawa ya kulewa. Bado kijana huyu ana safari ndefu ya kuachana kabisa na 'unga'.

Reply
Pepe
03/08/2011 04:53

Pole sana, Langa kwa mapito hayo, natumaini umepata fundisho, fanya kile ambacho unaona kitakusaidia kimaisha na wathamini sana wazazi wako.

Reply
Anna
16/08/2011 06:55

Nakupongeza Langa kwa hatua uliyofikia kwa sababu ni watu wachache huwa wanarudi nyuma na kukumbuka wapi alikosea, Mungu ni Mwema kwa maana alichokufunulia ni siri yako uer so lucky, nilisikiliza ulipokuwa unaongea clouds fm nililia chozi Langa coz u are among ma best musician in Tanzania ninaowapenda na ntaendelea kukukubali Langa. Mungu akupie Nguvu tunasubiri kwa hamu kubwa albamu yako mpya na naamini utokuwa kwenye makundi kama zamani. uer the herro Langa keep it up we love u!

Reply
mdau USA
16/08/2011 19:15

inasikitisha sana,pole Langa, cha msingi usirudi nyuma,ikiwezekana kaa mbali na watu waliokufanya ukayajua madawa, hadi hapo utakapokua tayari kuwasaidia na wao kuacha,ukiwa nao close kwa sasa itakua rahisi wewe kurudi nyuma,
una kipaji , lakini kama ulivyosimulia kuwa mauzo mabaya yalikuchanganya ukazidisha madawa, jitahidi either kukubali kuwa kwenye fani kuna kukosa na kupata so utakachopata utakubali, au fanya kazi nyingine ndio iwe ajira yako, kama ulivyoelezea umesoma marketing CBE,
all the best
mdau USA

Reply



Leave a Reply