Picture
Mtandao maarufu wa kijamii wa Facebook umemponza msanii mahiri wa muziki wa Injili nchini Tanzania, Flora Mbasha, baada ya mtu asiyefahamika ambaye ni shabiki wake kugandisha picha chafu za ngono kwenye ukurasa wake ambayo iliibuka mijadala na kushangaza wengi wiki iliyopita. 

Mbasha aliyetamba na nyimbo kama 'Adui', 'Usife Moyo', 'Sauti ya Mnyonge' aliibuka kwenye mtandao huo na kutoa ufafanuzi. 

"Bwana Yesu asifiwe wapendwa, naomba niwatake radhi kwa picha ambayo ilikuwa imetupiwa kwenye ukurasa wangu pia niwashukuru wote ambao mmenipigia simu kunieleza kinachoendelea kwenye Facebook yangu, pia nawashukuru wote mlionielekeza jinsi ya kuifuta maana nilijaribu nikashindwa. 

"Lakini pia nimuombe anayetupia picha kama hizi kwenye ukurasa wangu aache upesi la sivyo nitaifunga mtu yeyote asitupie vitu vyake ingawa haikuwa nia yangu kwani hii ni kwa ajili ya Injili, watumishi wa Mungu kukutana kuzungumzia habari za Mungu na marafiki mbalimbali kuelimishana kuhusu Injili na mambo yote yenye maadili na sio jambo lisilompendeza Mungu. 

"Kwa upande wangu nimekwazika sana kwani sikutegemea kama mtu mwenye akili timamu angefanya hivyo, ila nimemsamehe. Nia yangu ni nzuri sana, nataka watu tujadili mambo ya Mungu, tushauriane na hasa kutokana na huduma ya uimbaji niliyo nayo nahitaji sana ushauri wenu na mawazo. 

"Pia niwashirikishe mambo mbalimbali kuhusu maisha yangu binafsi pamoja na huduma, ili kwa pamoja tuonyane na tusaidiane pamoja na kuombeana. Nawapenda sana wote na amani ya Yesu Kristo iwe nanyi." 

Chanzo cha taarifa: blogu ya FloraMbasha ikilinukuu Gazeti la Mwanaspoti la Januari 17, 2012  


Ya kuzingatia...

Kwa wanaotumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook ka Twitter, kila mara mtu anapaswa kupitia 'settings' kuona ikiwa zipo kadiri ambavyo angependa zionekane kwa watu anaohusiana nao kwenye mitandao hiyo na jamii nzima kwa ujumla. 

Mara kadhaa mambo ambayo hayakuidhinishwa na wahusika wenye kurasa yametokea na kuacha makovu. Wamiliki wa tovuti hizi hufanya marekebisho mara kwa mara na bila kutuma ujumbe wowote kwa watumiaji wao kuwafahamisha kuhusu mabadiliko hayo. 

Iwapo mtu hatakuwa mwangalifu kuchunguza mabadiliko hayo, ni rahisi sana kwa mtu mwenye nia mbaya kutumia mwanya huo kufanya atakacho, hasa ikizingatiwa uwezo bwerere uliopo wa kuweza kufungua akaunti ya uongo kisha kuomba urafiki na mtu, mwenye kuombwa urafiki akiwa ni kati ya wale wanaokubali mtu yeyote kwa nia njema hata kama hamfahamu kwa kuona haya kuongekana 'mbaya', ni rahisi sana kukubali wenye nia mbovu ambao wameomba urafiki kwa nia iliyojificha ya kumchafua mtu. 

Kuwa makini! 
 


Comments




Leave a Reply