YATOKANAYO na kumbukumbu ya picha hizi...
Picha ya wanafunzi hawa nadhifu imenikumbusha nikiwa STD 1 tulipokuwa tunaimba,
Tujioshe mwili mzima twende safi shuleni x2
Meno tusugue pia nguo tufue x2
Na kagele keupe Mwalimu anapenda x2
Hii ndiyo afya tunayofunzwa shule x2
Ama kwa hakika ya kale dhahabu na maisha ni historia kila leo. Inafurahisha kuwaona wanafunzi bado wanaanza shule wasichana wakiwa wamevalia "vizibao" yaani sketi iliyoungwa na kushikizwa mabegani.
Wakati mmoja nilimwuliza Bibi (nimelelewa na kukua na Bibi ambaye ni Mwalimu Enzi za "Mwalimu", Mstaafu kwa sasa) ya kwamba, ni kwa nini siruhusiwi kuvaa sketi kama wasichana wengine il hali nilikuwa STD III tayari? - kwa maana tuliamini kuwa ukiingia darasa la tatu tayari hufungwi kuvaa vizibao, unakuwa umefuzu na kuvuka ngazi hiyo na sasa kuingia "heshima" kidogo kwa kupanda ngazi ya kuvua kizibao na kubakia na sketi nawe uweze kuruka "rede" vizuri.
Bibi akanifahamisha kwamba, "kwa vile bado u mdogo. Umbo lako likikua ukawa si "nukta" tena, basi na wewe utavaa sketi..." akasiriba msumari wa jina "nukta" ambalo hadi leo kawaita mwanaye wa mwisho (ambaye jina jingine ni "Uhuru" kwa vile alizaliwa siku ile ile ya Tanganyika kupata Uhuru wake, Desemba 9, 1961) na mimi mjukuu wake (kutokana na ufupi wangu, hadi sasa ningali bado "andunje" lakini sivai "vizibao" ingawaje nina magauni mawili "vizibao"... siachi asili!).
Nilipoingia darasa la nne, baada ya ripoti ya matokeo ya mtihani wa mwaka kwa STD III, nikanunuliwa zawadi ya sketi tayari kwa mwaka mpya wa masomo STD IV. Sitasahau kwa furaha niliyokuwa nayo, nikatamani shule zifunguliwe kabla ya wakati nami nikarige na "kagele kangu keupe"...
Asiye kwenda shule ni mjinga kabisa x2
Barua ikija aitembeza kutwa x2
Huyo, huyooo....
Nakushukuruni kwa dhati walimu wangu wote mlionifundisha na kunisaidia kuyamudu maisha. Mungu akulipeni heri!
Naanza kuhesabu namba, Moja, Mbili tatu x2
Nne, Tano, Sita, Saba, Nane, Tisa, Kumi x2
Vidole vya mikono yangu, Jumla yake kumi x2
Huku tano na huku tano, Jumla yake kumi x2
Vidole vya miguu yangu, Jumla yake kumi x2
Vidole vya miguu yangu, Jumla yake kumi x2
Ama kwa hakika Ya kale dhahabu! Unakumbuka? Unakumbuka nini?
Shukrani kwa Juma Mtanda kwa picha hizi zilizonisababisha "nifunguke" na zamani zangu za "Juma na Roza" na "kushuka" kumbukumbu hiyo hapo! Kwa picha na habari za kutoka Mkoani Morogoro, itembelee blogu yake ya jumamtanda.blogspot.com
Subi








RSS Feed