Somo limehaririwa kidogo nami, lakini msingi wake ni maandiko ya Lucy Nkya katika gazeti la Tanzania Daima.
Mahali popote palipo na mkusanyiko wa watu iwe majumbani, kazini, shuleni, vyuoni na sehemu nyingine upo uwezekano mkubwa wa kutokea migongano isiyokuwa ya lazima, kama mtu hatajitathmini na kuamua kujiepusha na hali hiyo.
Hivyo basi kutokana na hali hiyo ni vizuri kila mmoja akajua na kujifunza mbinu mbalimbali za kuishi na kila mtu, kwani anaweza akafanya jambo ambalo anaona kwake ni zuri na wakati huo huo likawa chukizo kwa watu wengine. Hii hutokana zaidi na maeneo ya mtu aliyokulia, mazingira ya familia iliyomzunguka, shule aliyosoma na malezi kutoka kwa wazazi au walezi wake.
Mtu hupendwa na watu kutokana na kufuata tabia na kanuni za watu wanaomzunguka, pia mtu huchukiwa kutokana na kwenda kinyume cha kanuni za kuishi na watu vizuri wanaomzunguka.
Tabia za kujifunza:
- Penda watu kwa moyo wote, unapoonesha upendo kwa mtu, uwe hivyo hadi ndani ya moyo wako na si kumuonesha mtu tabasamu la machoni wakati ndani ya moyo umejaa unafiki. Tabasamu la kuchangamka na kuonesha uso wenye furaha kwa watu. Epuka tabasamu la uongo, kwani mwishowe huleta athari.
- Heshimu kila mtu, awe mkubwa au mdogo, na kumuona ni wa maana na anahitajika. Mthamini kwa kumuonesha kuwa ni wa maana kuanzia maneno yake, matendo yake na mawazo yake yote, hata kama wakati mwingine atatoka nje ya mstari.
- Epuka tabia ya kulaumu, kuchamba watu au kusengenya.
- Jizoeze kutoa shukrani kwa jambo lililotendeka. Pokea shukrani mzazi wako, mkubwa wako wa kazi au mwalimu wako anapokupa pongezi kwa jambo fulani ambalo umelifanya. Kufanya hivyo kutamfurahisha aliyekupongeza. Shukuru hata kama jambo hilo ni dogo uonavyo wewe.
- Jitahidi kukumbuka majina ya watu. Mara nyingi kila mtu hupenda kupendwa, hivyo basi inapotokea mwalimu, mfanyakazi mwenzako au mkubwa wako wa kazi anakuwa makini na kukumbuka majina ya watu wanaomzunguka inaleta heshima na faraja. Hivyo ni vizuri ukajifunza kukumbuka majina ya watu unaoweza kukutana nao.
- Jifunze kusikiliza shida na matatizo ya watu. Unapokuwa baba au mama wa familia, kiongozi katika ofisi, shule, mtaa, taifa na maeneo mbalimbali yanayotuzunguka penda kusikiliza shida za kila mtu bila kubagua jinsia, kabila, rangi au elimu.Unapojenga tabia ya kuwa msikilizaji wa shida na matatizo ya watu utakubalika katika jamii na hata kwa taifa. Hali hiyo itakuongezea heshima.
- Jifunze kuvumilia na kusamehe pale unapokosewa na watu wengine na toa msaada unaohitajika kwao kila wanapohitaji. Baadhi ya watu mbalimbali neno uvumilivu huwa ni gumu kwao pamoja na neno kusamehe, hivyo ni vizuri kujijengea tabia ya kuwa mvumilivu na mtu wa kusamehe unapoumizwa na rafiki, mwenza, jirani, mwalimu, mfanyakazi mwenzio, mkubwa wako wa kazi n.k.
Tabia za kuepuka:
- Tabia za ubishi na mabishano hazifai katika jamii. Kumbuka kwenye mkusanyiko wa watu mahali pote huwa kuna watu wanaojiona kuwa wao wanajua kila kitu hivyo jaribu kujua tabia ya kila mtu ili uweze kuishi nao na kuepuka mabishano yasiyo ya lazima. Fahamu kuwa huwezi kumbadilisha mtu kwa njia ya mabishano, kinachotakiwa ni kueleweshana kwa ustaarabu kwani mnapobishana wote mnakuwa wajinga.
- Tabia ya upole inajenga mahusiano bora katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu. Pamoja na upole jitahidi kuwa mtu rahisi wa kufikiwa katika ushauri na mahitaji mbalimbali ya kiofisi na kimasomo.
- Epuka kumsifu mtu isivyostahili kwani ni kumvika kilemba cha ukoka. Watu wengine hupenda kutoa sifa kwa mtu tofauti na mpewa sifa alivyo, hivyo basi anayestahili sifa mpe sifa yake na anayestahili heshima mpe heshima yake lakini usithubutu kutoa sifa ya uongo kwani itakuondolea heshima na kumvika kilemba cha ukoka mhusika huyo kiasi kwamba ataweza kudharau wengine.
- Unapozungumza na mtu, jaribu kuchunguza na kuzungumza naye kulingana na mambo anayoyapenda. Kwa mfano, ukigundua kuwa unayezungumza naye hapendi mizaha, masuala ya muziki, siasa, michezo n.k., basi jaribu kuzungumza naye yale anayoyapenda ili muwe na uwiano katika mazungumzo yenu ili kuepusha kutofautiana katika mazungumzo.
- Epuka mijadala juu ya hoja zinazoleta ugomvi au mifarakano. Katika jamii inayotuzunguka mara zote mijadala ya siasa ambayo hutofautiana, mijadala ya timu za mipira na dini mbalimbali huchangia ugomvi na mara nyingine mifarakano.
- Epuka kusengenya au kusema mtu katika udhaifu wake. Mara nyingi tabia mbaya ya masengenyo ipo kwa makundi ya kina mama, naomba mniwie radhi kina mama kwa kuwa huwa na tabia ya kuoneana wivu na kutopenda maendeleo ya wenzao; Pia wapo wanaume ambao wamejiingiza katika makundi ya wanawake na kushiriki kusengenya ili tu waonekane wema machoni pa wanawake hao. Unapomwona mwenzako ana udhaifu mathalani katika kujieleza, kuvaa, usafi katika maeneo mbalimbali ni vizuri ukamwita kwa upendo na kumrekebisha. Si ustarabu kusimulia udhaifu wa mwenzako kwa kuwaeleza watu na baada ya kumsengenya ndipo unamwita na kumweleza upungufu wake. Fanya hivyo kabla ili kujijengea heshima katika jamii inayokuzunguka hata yule unayemsaidia.
- Epuka tabia ya kujisifu kutokana na mafanikio uliyoyapata. Hii ina maana kuwa hata kama unajua umefanya mambo ambayo yanahitaji usifiwe, ni vema ukasubiri watu wakusifu kuliko kujisifu, kwani hali ya kujisifu kwako inaweza kusababisha watu wakaona kama unajisikia kumbe sivyo na wakaamua kukujengea chuki.
- Kamwe usimfanyie mtu jambo lolote ambalo wewe hutaki utendewe. Angalia katika Biblia, kitabu cha Mathayo 7:12, kinasema kuwa: “Basi, yoyote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo.” Mara nyingi katika maeneo ya mkusanyiko wa watu huwa kuna tabia mbalimbali zinazojitokeza za baadhi yao kuwatendea wengine ambayo wasingependa wao kutendewa. Kwa mfano, wanaopenda kutuma wenzao wakati wao hawapendi kutumwa, au wanaopenda kukosoa wenzao wakati wao hawapendi kukosolewa, wengine hupenda kutania wenzao lakini wakali na ni marufuku kwao kutaniwa.


RSS Feed