Nilimsikiliza Sued Mwinyi akisimulia mechi hii kupitia redio TBC, nikatamani ningekuwepo kiwanjani. Ukitaka kusikia sehemu ya simulizi, bofya vipande vya audio vilivyopachikwa hapo chini.
Ilikuwa ni mechi kati ya timu ya soka ya wanawake Taifa, Twiga Stars dhidi ya wa Namibia katika kuwania kufuzu kushiriki fainali za soka kwa Mataifa ya Afrika. Mechi hiyo ya marudiano ilifanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hadi kipindi cha kwanza kinaisha, kila timu ilitoka kiwanjani ikiwa na mabao mawili, kisha Taifa Stars wakapata bao la tatu dakika ya mwanzo tu ya kipindi cha pili. Mabao mawili zaidi yalipatikana dakika ya 86 na 90+.
Bao la Namibia la dakika ya 29 lilitokana na mlinzi wa Twiga, Etoe Mlenzi, kujifunga mwenyewe. Bao lao la pili lilifungwa dakika ya 73 na Juliana Skrywer.
Wafungaji kwa Taifa Stars walikuwa Mwanahamisi Omari dakika ya 21 na 88 na Asha Rashid dakika ya 46, 88 na 90.
Kwa hivyo hadi mwisho wa mchezo, Twiga Stars ilifungasha kibindoni mabao 5 na Namibia 2.
Katika mechi ya awali Twiga Stars waliwafunga Namibia 2:0 huko kwao.
Tunasubiri kujua tutacheza na nani kati ya Misri na Ethiopia wanaocheza baadaye leo.
Pongezi za dhati timu inayofanya vyema ikilinganishwa na maandalizi hafifu inayopewa dhidi ya timu nyingine.
Twiga - Fatuma Omary, Fatuma Bushiri, Pulkaria Charaji/Mwajuma Abdallah (52), Fatuma Khatib ‘Foe’, Sophia Mwasikili (nahodha), Mwapewa Mtumwa, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, Etoe Mlenzi, Fatuma Mustafa, Asha Rashid ‘Mwalala’ na Fadhila Hamad.
Namibia - Susanna Eises, Uerikondjera Kasaona, Lovisa Mulunga, Esther Amukwaya, Stacey Naris, Alberta Dakies/Juliana Skrywer (69), Shirley Cloete, Leticia Manga, Thomalina Adams, Elmarie Frederick and Lydia Eixas.


RSS Feed