
Akasema kuwa hadi sasa, tayari Wizara imeshawalipa Madaktari wote husika, stahiki ya kiasi cha fedha walichokuwa wanadai.
Kwa mantiki hiyo, Serikali imepuuza madai yote mawili ya yaliyotolewa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kutaka kurejeshwa kwa madaktari wote waliokuwa wakifanya mazoezi ya vitendo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kupitiwa upya uamuzi wa kuhamisha madaktari bingwa 61, kutoka hospitali hiyo ya taifa.
Madaktari 194 waliokuwa wakifanya kazi Muhimbili waliondolewa na kupelekwa katika vituo mbalimbali baada ya kuibuka mgomo huku madaktari hao bingwa nao wakipelekwa kwenye vituo mbalimbali.
Naibu Waziri pia alitetea uamuzi wa kuwahamisha na kuwapangia vituo vipya vya kazi. Katika tamko hilo, Dk Nkya alisema tathmini iliyofanywa na wizara ilibaini kuwa idadi ya madaktari waliokuwa katika mafunzo kwenye hospitali ya Muhimbili ni kubwa kuliko uwezo wake akisema wingi wao ungeathiri mafunzo ya taaluma yao.
Alisema madaktari hao hawakufukuzwa kazi, bali walirejeshwa wizarani ili kupangiwa vituo vingine vya kazi kumalizia muda wao wa mazoezi kwa vitendo, baada ya kuvunja mkataba na uongozi wa hospitali hiyo.
“Kitendo cha madaktari hao kugoma licha ya Serikali kuwaeleza bayana kuwa ilikuwa inaendelea na hatua ya kushughulikia madai yao, si cha kiungwana na kilikiuka mkataba walioingia na uongozi wa hospitali unaokataza kugoma,” alisema na kuongeza kwamba kitendo hicho pia kilikiuka kiapo chao kinachowataka kutetea uhai wa watu muda wote.
“Kwa kuzingatia hatua zilichokuliwa na wizara na jinsi wahusika walivyotekeleza maagizo ya Serikali, hadi sasa ni dhahiri kuwa tamko la MAT kuhusu kunyanyaswa kwa madaktari walioko mazoezini halina msingi wowote,” alisema.
Baada ya mgomo Nkya alisema baada ya madaktari hao kugoma, wizara ilichukua hatua za haraka za kuziba pengo kwa kuwaingiza madaktari 51 kwenda kufanya mazoezi ya vitendo Muhimbili huku akisema hadi kufikia juzi, Jumatatu madaktari hao 194 waliogoma walikuwa wamepokea barua za kuripoti katika vituo hivyo vipya vya kazi.
Alisema madaktari hao walipangwa katika vituo vingine na waliorejeshwa Muhimbili ni 86 huku wengine wakihamishiwa katika vituo vya Temeke, Amana, Mwananyamala, Mgulani na Aga Khan. MAT kiliitaka Serikali kuwarejesha wataalamu hao Muhimbili ili wamalize mafunzo yao na kwamba kitendo cha Serikali kuwahamisha madaktari bingwa 61 mwaka jana hakikufuata taratibu hali inayosababisha wengi kushindwa kuendelea na kazi.
Hadi taarifa hii inachapishwa hapa wavuti.com leo Januari 18, 2012, saa tano adhuhuru Chama cha Madaktari Tanzania, MAT, kinaendele na mkutano na wanachama wake ili kuamua hatua za kuchukua.


RSS Feed