Hakuna maneno matamu zaidi ya kusema kuwa Elimu yetu iko kwenye mkwamo mkubwa sana kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu. Isipo kuwa ukisikiliza wanasiasa wakisifia idadi ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa pamoja na idadi ya wanafunzi walio andikishwa shule unahamasika na kufarijika bila chembe ya shaka kuwa tumepiga hatua kubwa sana katika sekta ya elimu.
Lakini ukweli mchungu unabaki kuwa Elimu yetu iko kwenye mkwamo mkubwa sana na hakika tunaandaa taifa la vilaza wenye vichwa nazi. uzuri wa bahati ni kwamba wakubwa wamelijua hili mapema sana ndio maana wao hawasomeshi watoto wao kwenye hizi shule za kina Kayumba zilizosheheni ukanjanja wa kila aina, Wao watoto wao wana wasomesha kwenye shule zenye mazingira bora kwa afya ya akili ya watoto wao ili waje kushika nafasi zao na kuendelea kuwatawala watoto wa maskini wasio kuwa na uwezo wa kupata elimu bora.
Matatizo ni mengi kwenye sekta ya Elimu lakini kubwa ni namna ya kumpata na kumuandaa mwalimu bora atakae fungua milangao ya fahamu ya mwanafunzi. Walimu wengi wa sasa hasa wale wa shule za msingi ni walimu waliofauli kwa viwango vya chini (Div IV), hawa wamefeli na wanatakiwa kuandaa watoto watakao faulu, halika dhalika sekondari, mfumo wa kuandaa walimu kwa njia ya Vodafasta nao umekuwa na madhara makubwa kwani kwa kipindi cha mwezi mmoja au mitatu bado hakitoshi kumuuandaa mwalimu bora atakae kuwa mahiri kwenye nyanja zote za ufundishaji, kitakacho fuata hapo ni kushindwa kumudu mchakato wa ufundishaji na matokeo yake ufaulu duni wa watoto.
Lakini pia baya zaidi kwa sasa ni la walimu kutokuwa na ari ya kufanya kufundisha kutokana na mazingira magumu na ki mshahara kidogo kisicho endana na gharama za maisha, Nina mfano wa Mwalimu aliye ajiriwa kwa ngazi ya Stashada tangu mwaka 2006 akianza na mshahara wa shilingi 124,000/= (take home) mpaka leo hii analipwa 280,000/= (take home) ana barua ya kupandishwa daraja mkononi lakini hajabadilishiwa ngazi ya mshahara na wako wengi wa namna hii. Hebu tujiulize, kwa shilingi 280,000/= Mwalimu huyu ataishi maisha ya namna gani kwenye mfumuko huu wa bei yeye na familia yake? Ari yake ya kufundisha kwenye darasa lenye watoto 70 - 80 itakuwaje?
Mdororo wa elimu yetu unaanzia kwenye kuto kuwajali walimu kimaandalizi na ki-maslahi, majengo kwangu si tija maana mwalimu aliye andaliwa vizuri ki saikolojia na kimaslahi akipatiwa vifaa bora anaweza kufundisha hata kwenye darasa mithili ya banda la kuku kama haya tuliyo kuwa nayo na bado wanafunzi wakapata maarifa yaliyokusudiwa. Kinacho tugharimu leo ni kukosa viongozi wenye utashi wa dhati kusimamia elimu kwa dhati ya kusimamia na matokeo yake imekuwa vurugu mechi na uchakachuaji wa mitihani.


RSS Feed