Picture
Vitanda vikiwa tupu bila ya wagonjwa katika wodi ya Sewahaji, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana mgomo wa madaktari wa Hospitali hiyo kama inavyoonekana katika picha hii iliyopigwa leo
Nashindwa niandike nini na niache nini, na hata nitakachoandika hapa kama kitaleta maana yoyote; Kwa kuwa nimejawa na huzuni isiyo kifani; Huzuni kiasi cha kushindwa hata kufanya shughuli za kawaida. Namaanisha hata kula, hamu sina.

Kila mara inanijia kichwani picha moja baada ya nyingine ya ama mtoto, au mwanamke au mwanaume, amelala katika kitanda cha wagojwa Muhimbili, Mbeya, Moshi, Morogoro, Mwanza n.k. anapumua ile pumzi ya mwisho "gasping for air" ya kiumbe hai anapokaribia kukata roho.

Nina huzuni kubwa zaidi kutokana na jinsi ambavyo viongozi na watu wenye dhamana wameshindwa kabisa kufikia muafaka wa kuokoa roho za Watanzania ambao ndiyo wanasema wanawaongoza na kujali maslahi yao. Maslahi makubwa kuliko kuunurusu uhai pale inapowezekana siyafahamu.

Ni nyakati kama hizi unafikia hatua ya kujiuliza Mungu yupo wapi na kama anaikumbuka Tanzania.

Nyakati za kuwaza kama kufa ni jambo baya kama wengi tulivyoaminishwa, au ni jambo zuri na la kawaida kabisa isipokuwa tu tunatengana na wenzetu wanaotangulia kwenda ambako walio hai hawawezi kwenda hadi wafe.

Nyakati kama hizi nawaza kuwa Mungu anaikumbuka Tanzania kweli na anaipenda isipokuwa ameruhusu yanayotokea yatokee kwa kuwachukua waja wake wamrejelee kwa maana hata uhai wao ungeokolewa kwa siku kadhaa na Madaktari au/na Wauguzi, bado maisha yake yangeendelea kuwa ya taabu na maumivu. Kumbe pengine kufa ni pumziko kwao.

Ni nyakati kama hizi ninaamini ile kauli ya viongozi wetu wanazotoa punde zinapotokea ajali na majanga yakachukua roho nyingi za watu kuwa, "Ni mipango ya Mungu" "Ni mapenzi ya Mungu" basi huenda ni hayo hayo mapenzi na mipango ya Mungu kuwa mgomo wa wahudumu wa afya utokee na Viongozi wa Serikali wapungukiwe akili ya kutatua ili watu wafe.

Kimya cha Jumuiya za Kimataifa na ukimya wa vyombo vya habari vya Kimataifa umeniongezea simanzi. Pengine ni kwa kuwa hii ni nchi ya bara la Afrika, bara ambalo hakuna jema lolote linalotarajiwa na hata watu mamia kwa maelfu wakipoteza uhai, si habari mpya masikioni mwao, wamezoea kusikia hahari za vifo, lipi jipya? Hivyo hawatilii maanani kwa kuwa hakuna umuhimu huo. Mkidharauliwa na hata viongozi wenu wenyewe mliowachagua, mwanadamu gani anapaswa kuwathamini?

Mahakama ya The Hague huwa inahusika na vifo vinavyotokana na machafuko na vita baada ya chauguzi za kisiasa tu? Kwa hivyo "neglect" ya wananchi kupata huduma ya msingi ya afya haimhusu Ocampo sivyo?

Mungu anaikumbuka Tanzania na anaipenda na mapenzi yake yanatimizwa! Amin.
 


Comments

alledros
03/02/2012 10:40

Hapo ni ukweli mtupu! Maneno na mawazo yako yananikuta kabisa. Uchungu gani kuona wabunge kugombania kama mbwa kwa mfupa kwa kujadili posho yao wakati wananchi wanakufa bila huduma! Ukiona machozi ya watu wengi na kusikia vilio hospitalini kweli unajisikia vibaya mno: tumetenda dhambi gani kwa kupata haya yote?

Reply
belinda habibu
08/02/2012 04:34

sijajua mizengwe inatoka wapi watendaji wamezoea kutisha walio chini bila kutimiza wajibu kama kila mmoja wetu anatimiza wajibu wake haya yote tungeyasikia kwa wenzetu.jamii inaweza wawalaumu madaktari na wahudumu wote wa afya,lkn wao hawana maisha binafsi niliwahi kwenda hospital ya mawenzi Moshi niliangalia,kuna mazingira magumu ya kazi basi walau walipwe stahiki zao,jamani hata kama kitanda ulichokilalia hujui kunguni wake kumbuka watendaji wote mmewekwa na wananchi,nina uchungu

Reply



Leave a Reply