Majaribu vumilia, naona yashindikana,
Hasira zinanijia, furaha yakosekana,
Hebu sasa fikiria, hawa wana wa rabana,
Serikali na waganga, wapi mnatupeleka?

Waganga mwajitahidi, roho zetu kuziponya,
Hata sikuu ya Iddi, waganga mwapatikana,
Kumbe nanyi mna dhiki, mnashindia makana! (pumba za mahindi au mtama)
Serikali na waganga, wapi mnatupeleka?

Maisha haya magumu, nani asiyeyajua,
Waganga mwawahukumu, vinono mnajilia,
Wapeni hata chandimu, nadhani watachezea, (mpira wa makaratasi)
Serikali na waganga, wapi mnatupeleka?

Wadanganyika fukara, Temeke twategemea,
Msifanye masihara, sisi tunaangamia,
Amana zetu nyembamba, hazitoshi enda Indya, (mshiko)
Serikali na waganga, wapi mnatupeleka?
 

Waganga namalizia, kama kweli mna nia,
Wekeni chini SILAHA, pasiwe wa kubakia,
Gogoro mwalirefusha, kwa kuwa mnapingana,
Serikali na waganga, wapi mnatupeleka?

Haya kama hayafai, basi jaribuni hili,
Wote rudini kazini, mpunguze makaburi,
Mola wetu si bahiri, pepo mtaikabiri,
Serikali na waganga, wapi mnatupeleka?

NA MGHANI WENU MZEE MTWANGAMBATE

Dkt. Mtwangambate G.C; (M.D.)
 


Comments




Leave a Reply