Bunge halina mguso na Wananchi ‘out of touch’ - Zitto Kabwe
Leo wabunge kwa mara nyingine wamesimama kutaka mjadala huu wa dharura. Naibu Spika wa Bunge akatumia sababu za kiufundi kuzuia mjadala. Inawezekana wabunge hawakuwaandaa wabunge kusimama kuunga mkono hoja, lakini ni jukumu la Kiti kuona umuhimu na udharura wa mijadala.
Hii inadhihirisha kwamba sasa Bunge kama Mbunge mmoja mmoja au kwa ujumla wake na Taasisi ya Bunge imekosa mguso na Hali ya wananchi (out of touch). Hali hii ni hatari sana. Wananchi wanapoona chombo kinachowawakilisha hakitoi nafasi kwa masuala yanayowagusa, watachukua hatua zao wao wenyewe na hivyo kuhatarisha utulivu wa nchi. Bunge liache shughuli nyingine zote na kutoa fursa ya kupokea taarifa ya serikali kuhusu madai ya Madaktari, kuijadili na kuazimia kwa kuelekeza hatua za kutekelezwa na serikali.
BUNGENI LEO: Mgomo wa Madaktari na Sheria ya Bodi ya Mikopo - John Mnyika
Kwa kuwa hoja kama hiyo iliwasilishwa juzi na ikaungwa mkono lakini Spika akasema ameshakubaliana na serikali kuwa ingewasilisha kauli. Hata hivyo, jana hakukuwa na kauli ya serikali huku wananchi wakiendelea kupata madhara ya mgomo.
Hivyo nikata muongozo kwa kuwa Spika alitumia kanuni ya 49 (2) ambayo kimsingi inatoa mwanya kwa kauli ya serikali kuwasilishwa kwenye wakati atakaoona yeye kuwa na unafaa juu ya jambo linaihusu serikali na lisilozua mjadala.
Nilitaka kanuni hiyo isitumike badala yake wabunge tutimize wajibu wa kuisimamia serikali kwa kutumia kanuni ya 47 kuhusu hoja ya dharura. Kwa kuwa ilikuwa muongozo hakukuwa na hitaji la kikanuni la wabunge wengine kuunga mkono lakini akaamua kuilinda serikali kwa kuwa hawakuwa wamejiandaa.
Lakini mwishoni ameahidi kuwa kauli ya serikali itatolewa kesho.
Wabunge wana kigugumizi au...? - Beda Msimbe/Lukwangule
Waandishi wa habari waliokuwapo katika chumba cha kufuatilia mijadala ya bunge walijikuta wakisemezana imekuwaje baada ya maswali manane kwa waziri mkuu yote kukosa swali kuhusu tatizo la madaktari na posho.
Huenda tatizo la madaktari kwa kuwa linangoja tamko la mawaziri husika, lakini suala la posho bado lingeweza kuulizwa kwa kuwa kuna kutupiana mpira kati ya Ikulu na ofisi ya Spika juu ya kuridhiwa kwa posho hizo.
Maswali aliyoulizwa waziri Mkuu jana mengi hayakuwa ya kisera na kumfanya Spika wa Bunge Anne Makinda kuwakumbusha wabunge kwamba Waziri mkuu anahitaji maswali ya kisera na wala si ya kiutendaji, mambo ambayo yanatakiwa kujibiwa na mawaziri.
Lakini hata kabla spika hajasema hayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda naye alisema kiungwana kwamba maswali ambayo ni specific (mahususi) hawezi kuyajibu kwa kuwa yeye atakuwa anajua masuala ya kijumla ambayo yanagusa sera.
Katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo wabunge wengi walizungumzia majimbo yao na matatizo binafsi kuliko masuala ambayo ni ya kitaifa na yenye mwelekeo wa kuchanganua sera zilizopo.
Hata hivyo Waziri Mkuu ambaye alijibu maswali kutoka kwa wabunge wanane kati ya 26 walioomba kupewa nafasi kwa Spika, aligusia tatizo la kuyumba kwa uchumi ambako alieleza ni kwa dunia nzima.
Akijibu swali la mbunge Diana Chilolo (Viti maalum - CCM) kuhusu mkakati wa serikali wa kukabiliana na tatizo la kuharibika kwa uchumi wa nchi Waziri Mkuu alisema taifa lipo katika msukosuko mkubwa unaotokana na mfumuko wa bei unaosababishwa na bei kubwa ya chakula na mafuta.
Aliwatafadhalisha watanzania kutambua kwamba tatizo la kuyumba kwa uchumi si la watanzania pekee bali ni la kidunia ila kinachostahili ni kutekeleza mipango itakayowezesha kuongeza tija na kuboresha uchumi.
Pia alizungumzia uboreshaji wa kilimo ambapo alisema serikali inajitahidi kilimo kuwa chepesi na chenye manufaa ili vijana wasikimbilie mijini na pia kutanua sekta nyingine kwa kuwa na mazao ya kusindika na kuyaongezea thamani.
Alisema ni kweli kuwa ni wajibu wa serikali kuweka mazingira mazuri ya uzalishaji mali lakini pia ni wajibu wa wananchi kuwajibika.
“Serikali imejitahidi kusaidia… tumeshusha bei ya matrekta kutoka India kati ya asilimia 15-30 ili kukiinua kilimo” alisema waziri Mkuu.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema kwamba mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa Kigamboni na Kurasini unachelewa kutokana na haja ya wananchi kushirikishwa.
Akijibu swali la Mriam Kisangi (viti maalumu – CCM) aliyetaka kujua miradi hiyo inaanza lini kwa kuwa inawachelewesha wananchi kupata mikopo katika benki kwa kukosa hati, alisema kamati imeundwa ili kuzungukia wananchi.
Akizungumzia suala la fidia Mabwepande, Waziri Mkuu alisema kwamba serikali inajipanga ili wale wanaostahili kulipwa waweze kulipwa fidia zao.
Aidha alisema kwamba mpaka sasa viwanja 300 vipo tayari kwa ajili ya waathirika wa mafuriko na kwamba watu waliokusudiwa ni kaya 500.
Alisema hata hivyo wanachangamoto kubwa ya kuwapatia viwanja wapangaji kama Rais Jakaya Kikwete alivyoelekeza.
Taarifa ya mambwepande ilitokana na swali la mbunge wa Kawe Halima Mdee (CHADEMA).
Akizungumzia masuala ya magari ya serikali kuwekewa bima, Waziri Mkuu alisema kwamba kupanga ni kuchagua na kusema zipo sababu kwanini magari yote hayo hayawezi kuwekewa bima. Swali la Bima liliulizwa na mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed (CUF).
Swali jingine ambalo liliulizwa lilikuwa la wastaafu ambalo nalo lilikuwa mahusisi na Waziri Mkuu kumtaka mbunge awasiliane na waziri wa mambo ya ndani.
Wabunge wengine ambao waliuliza maswali mahsusi ni mbunge wa Vunjo Agustino Mrema (TLP) aliyeulizia soko la Himo, Profesa Kulikoyela Kahigi (CHADEMA) aliyeuliuzia wastaafu jimboni kwake, mbunge wa Kasulu Mjini Moses Machali (NCCR-Mageuzi) na mbunge wa Kilwa kaskazini, Muntazi Ali Mangungu (CCM).


RSS Feed